ZITTO KABWE AMPOPOA VIBAYA JPM,NI KUHUSU UTAWALA WAKE,SOMA HAPO KUJUA
CHAMA
Cha Mapinduzi (CCM) kimepoteza mvuto hivyo kinatumia nguvu ya Jeshi la Polisi
na hata Jeshi la Wananchi dhidi ya vyama vya upinzani, anaandika
Charles William.
Ni kauli la Zitto Kabwe, Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT
Wazalendo akizungumza na waandishi wa habari leo katika Makao Makuu ya ofisi za
chama hicho Kijitonyama, jijini Dar es Salaam.
Kwenye
mkutano huo Zitto amesema, kutokana na CCM kukosa mvuto kwa wananchi, sasa
wanamsukuma Dk. John Magufuli, mwenyekiti wa chama hicho pia Rais wa Tanzania
kutumia vyombo vya dola ili kuokoa taswira ya chama hicho.
Lifuatalo
ni tamko la chama hicho (ACT Wazalendo), lililotolewa na Zitto kwa waandishi wa
habari leo.
Tamko Rasmi la Kamati Kuu ya Chama cha ACT-Wazalendo kuhusu HALI
YA NCHI
Dar Es Salaam, Jumanne, 06 Septemba 2016
Utangulizi
Jana
Jumatatu, 5 Septemba 2016, Kamati Kuu ya Chama cha ACT-Wazalendo ilikutana
katika kikao chake cha kawaida. Pamoja na mambo mengine, Kamati Kuu ilipokea,
kujadili na kuidhinisha Taarifa kuhusu HALI YA NCHI. Taarifa hii sasa inatolewa
rasmi kwa umma. Taarifa ipo katika maeneo makubwa manne: Hali ya kisiasa, hali
ya kiuchumi, umoja wa kitaifa na hitimisho.
Hali ya Kisiasa
Kamati
Kuu imezingatia kuwa Kikatiba, nchi yetu inafuata mfumo wa demokrasia ya vyama
vingi. Katiba na Sheria mbalimbali zimeanisha utaratibu wa kazi na shughuli za
vyama vya siasa. Ili kuhakikisha kwamba kazi na shughuli za vyama vya siasa
zinakuwa endelevu, vyama vyenye kukidhi vigezo hupewa ruzuku kupitia Bajeti ya
Serikali inayopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania.
Hata
hivyo, katika awamu hii ya tano, Serikali ya Chama cha Mapinduzi imeamua kuzuia
shughuli za siasa kwa kutumia nguvu ya Jeshi la Polisi na hata Jeshi la
Wananchi. Kwa mujibu wa serikali ya CCM, shughuli za kiuenezi za vyama vya
siasa kama vile mikutano ya hadhara, maandamano, makongamano, mijadala na hata
mikutano ya ndani inapaswa kukoma mapema baada ya uchaguzi. Kisheria, huu ni
uvunjifu wa Katiba na Sheria za nchi.
Kisiasa,
tunatambua kwamba Viongozi wa CCM wamepoteza mvuto kwa wananchi na sasa
wanamsukuma Mwenyekiti wao Rais Magufuli kutumia jeshi katika kuokoa taswira ya
Chama cha Mapinduzi mbele ya umma.
Kwa
kuzingatia hali ya kisiasa nchini kwa sasa, Kamati Kuu ya chama chetu:
i)
Tunalaani na kupinga kwa nguvu zetu zote hatua za Serikali ya Chama cha
Mapinduzi za kuvunja Katiba na kujaribu kuweka pembeni utawala wa sheria.
ii)
Tunapinga vitendo vinavyozidi kushamiri katika serikali hii ya CCM ya kujaribu
kuendesha nchi kwa ubabe na matamko ya viongozi badala ya utawala wa sharia.
iii)
Tutasimama imara, na tutaungana na vyama vingine vya siasa pamoja na taasisi
zingine za kiraia katika kulinda mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, uhuru wa
maoni, na utawala wa sheria katika nchi yetu
Hali ya Kiuchumi
Katika
miaka 10-15 iliyopita, nchi yetu imejenga uchumi ambao umekuwa ukikua kwa
kiwango cha asilimia 6-7 kwa mwaka katika kipindi chote hiki. Ukuaji huu wa
uchumi ulitokana na juhudi za nchi katika kuvutia wawekezaji na kuchochea
shughuli za uzalishaji mali kwa wananchi wenye kipata cha chini. Awamu ya tano
ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi imerithi changamoto ya uchumi unaokua bila
kuwafaidisha wananchi wa kawaida. Hili ndilo tulitegemea Serikali mpya
ishughulike nalo.
Kamati
Kuu imeshtushwa na hali ya kuanza kudorora kwa shughuli za uchumi katika
kipindi cha miezi kumi ya utawala wa awamu ya tano. Kwa mfano:
a)
Taarifa za Benki Kuu zilizopo kwenye tovuti yake (Quarterly Economic Review na
Monthly Economic Review) kwa robo ya mwisho ya mwaka 2015 (Oktoba – Desemba
2015 ) zinaonesha kuwa kasi ya ukuaji wa Pato la Taifa ilikuwa 9%. Katika robo
ya kwanza ya mwaka 2016 (Januari – Machi 2016) kasi ya ukuaji wa Pato la Taifa
ilishuka hadi kufikia 5.5%. Kiuchumi, hii inamaanisha kuwa ukuaji wa shughuli
za kiuchumi katika kipindi cha miezi 6 ya mwanzo ya utawala wa awamu ya tano
chini ya Rais Magufuli umepungua kwa 4%.
b)
Shughuli za uchumi zinazohusu wananchi masikini zimeshuka kutoka kasi ya ukuaji
ya 10.20% robo ya mwisho ya mwaka 2015 mpaka 2.7% katika robo ya kwanza ya
mwaka 2016, ikiwa ni punguzo la 8% ndani ya kipindi kisichozidi miezi sita. Hii
ina maanisha kwamba Wananchi wetu wanazidi kudumbukia kwenye ufukara kwa kasi
tangu awamu ya tano ya Serikali ya Chama Mapinduzi iingie madarakani
c)
Ukuaji wa sekta ya ujenzi katika robo ya mwisho ya mwaka 2015 ilikuwa 13.8%
lakini ukuaji wa sekta hii katika robo ya kwanza ya mwaka 2016 ilikuwa ni
4.30%, ikiwa ni tofauti ya takribani -10%. Hii ni kwa sababu uwekezaji katika
sekta hii umeanza kushuka.
d)
Kasi ya ukuaji wa sekta ya usafirishaji imeporomoka kutoka kukua kwa 14.50%
robo ya mwisho ya 2015 mpaka kukua kwa 7.9% robo ya kwanza ya 2016, ikiwa ni
kuporoka kwa 7% katika kipindi cha miezi 6 tu ya kwanza ya utawala wa Rais
Magufuli. Kuporomoka kwa sekta ya usafirishaji itaathiri watu wengi, wakiwemo
madereva, matingo, pamoja na mama Ntilie wanaowauzia chakula. .
Kwa
kuzingatia mwenendo wa hali ya uchumi katika nchi, Kamati Kuu:
a)
Tunaitaka serikali izingatie sayansi ya uchumi katika kuendesha uchumi wa nchi.
Uamuzi wa CCM wa kuitelekeza serikali yake kwa mwanasiasa mmoja anayedhani
ndiye anayejua kila kitu na yeye kugeuka kuwa mshauri wa washauri wa uchumi
itasambaratisha uwekezaji nchini na kuua kabisa juhudi za miaka 20 za kuvutia
wawekezaji na kujenga uchumi shirikishi.
b)
Inahimiza wananchi kuzingatia kuwa msingi wa uchumi wetu ni uwekezaji kutoka
ndani na nje ya nchi. Msingi wa kuvutia wawekezaji ni utawala wa sheria. Juhudi
za serikali ya CCM za kuua utawala wa sheria zitaua uwekezaji na kuangamiza
uchumi wa nchi. Tusirihusu CCM iue uchumi wa nchi kwa maslahi yake ya kisiasa
na viongozi wake.
Umoja
wa Kitaifa
Nchi
yetu imefanya juhudi kubwa katika miaka 50 iliyopita katika kujenga umoja na
mshikamano wa kitaifa kwa kuhakikisha kuwa makabila, dini na baadaye vyama vya
siasa tunaishi bila kukamiana. Juhudi za dhati za kupambana na ubaguzi ndiyo
umekuwa msingi imara wa kujenga Umoja wa Kitaifa na amani tunayojivunia.
Hata
hivyo, Kamati Kuu imezingatia kuwa utawala mpya wa Serikali ya CCM, kupitia
Mwenyekiti wake mpya na Rais wa Jamhuri wa Muungo, umeanza kwa juhudi na kasi
kubwa kuchokonoa na kumomonyoa misingi ya utaifa na umoja wetu. Sasa tunaye
Rais asiyechagua maneno na asiyejua aongee nini na wapi. Vijana waliosoma kwa
bidii katika mazingira ya shule zilizotelekezwa na serikali ya CCM anawaita
VILAZA.
Katikati
ya uhasama mkubwa wa kisiasa na kijamii huko Zanzibar Rais wetu amefunga
safari, sio kujaribu kutibu majeraha yaliyosababishwa na kuchezewa kwa sanduku
la kura, bali kuchochea uhasama chini ya ulinzi wa vyombo vyetu vya dola vyenye
jukumu la kulinda na kudumisha amani. Sasa Rais wetu, kupitia kauli zake, ameanza
kuubomoa muungano wetu uliojengwa kwa unyenyekevu na katika mazingira magumu.
Kila
asimamapo kuhutubia, jambo moja la kutarajiwa kutoka katika kinywa cha Rais
wetu ni matamshi yanayodhoofisha nguzo fulani ya umoja, mshikamano na undugu
wetu kama taifa. Yote haya yakitokea chama chake cha CCM ama kimekaa kimya au
kinachekelea. Inasikitikitisha kwamba Chama kilichoasisiwa na Mwalimu Nyerere
kinamruhusu kiongozi wake kubomoa misingi ya umoja wa kitaifa na kuchochea
chuki katika jamii ya watanzania.
Kwa
kuzingatia mtikisiko mkubwa katika umoja na mshikamano wa kitaifa unaoendelea
nchini, Kamati Kuu:
a)
Tunalaani juhudi zinazofanywa na Serikali ya CCM kupitia Mwenyekiti wao za
kuchochea chuki katika jamii ya watanzania na kubomoa misingi ya umoja wa kitaifa
na amani ya nchi
b)
Tunatoa wito kwa watanzania wote waipendayo nchi yao kusimama kidete katika
kulinda misingi ya nchi yetu na kukataa chuki inayoanza kujengwa na utawala wa
CCM
c)
Tunatoa wito wa kipekee kwa viongozi wetu wa dini na wakuu wa nchi waliopita,
hususani Mzee Ali Hassan Mwinyi, Mzee Benjamin Mkapa na Mzee Jakaya Mrisho
Kikwete, pamoja na wazee wengine wanaoheshimika katika nchi yetu wavae ujasiri
wa kumuonya Mwenyekiti wa CCM kuwa juhudi zake za kuchochea chuki katika jamii
yetu ya watanzania zitasambaratisha Taifa letu.
Hitimisho
i)
Sisi kama chama cha siasa, tunaendelea kusisitiza kuwa tutaunga mkono juhudi za
serikali ya awamu ya tano katika kupambana na ufisadi na kujenga uwajibikaji
nchini.
ii)
Tunaamini kwa dhati kabisa kuwa kuheshimu na kulinda demokrasia na kuzingatia
utawala wa sheria nidyo msingi wa mapambano dhidi ya ufisadi. Tunasisitiza kuwa
mtu yeyote, wa kawaida au kiongozi, anayesema kwamba anaweza akapambana na
ufisadi kwa kukanyaga misingi ya demokrasia na utawala wa sheria mtu huyo ni
mwomgo na kwa kweli ni fisadi na anataka kujenga himaya mpya ya ufisadi. Mtu
huyo, pamoja na mambo yake yote, yafaa akataliwe na kudharauliwa haraka!
iii)
Tunasisitiza kuwa msingi wa uchumi wetu ni kuvutia uwekezaji wa ndani nan je ya
nchi. Kuzingatia utawala wa sheria ndiyo msingi wa kuvutia uwekezaji. Juhuzi za
hivi karibuni za serikali ya CCM za kujaribu kuua utawala wa sharia ni juhudi
ovu za kuua uchumi wa nchi yetu. TUZIKATAE juhudi za kuua utawala wa sheria kwa
kuwa zitaangamiza taifa letu kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto, Mb
Kiongozi wa Chama
Dar es Salaam, Jumanne 6 Septemba 2016.