MAKAMANDA WA CHADEMA WAPATA DHAMANA,YUMO SALUM NA WENZAKE,SOMA HAPO KUJUA
Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu imewaachia kwa
dhamana Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu na wafuasi
wengine 18 wa chama hicho baada ya kukaa mahabusu kwa zaidi ya siku 12.
Kiongozi huyo wa Chadema na wafuasi hao 18 walikuwa
wakishikiliwa katika mahabusu za jeshi la polisi kwa tuhuma za kuandaa na
kuhamasisha maandamano na mikutano ya Oparesheni ya chama hicho iliyopewa jina
la UKUTA, ambayo ilipigwa marufuku na jeshi hilo.
Walifanikiwa kupata dhamana baada ya Hakimu wa
Mahakama hiyo kueleza kuwa ameridhia hoja za upande wa utetezi baada ya
kusikiliza pande zote mbili na kubaini mapungufu kwenye maombi ya upande wa
mashtaka.
Awali, Mwendesha mashtaka aliitaka Mahakama hiyo
kuwanyima dhamana washtakiwa hao kwa madai kuwa endapo wataachiwa wataendelea
kufanya kosa hilo.
Hata hivyo, Hakimu alitupilia mbali maombi hayo
akieleza kuwa wameshindwa kuthibitisha pasipo shaka kuwa endapo washtakiwa hao
wataachiwa watafanya tena kosa hilo.
Pia, Hakimu alieleza kukubaliana na hoja ya washtakiwa
hao kuwa hati ya kiapo iliyowasilishwa mahakamani hapo na mwendesha mashtaka
ilikuwa na mapungufu ya kisheria.
“Ninakubaliana na upande wa utetezi kuwa
hati ya kiapo iliyowasilishwa ina mapungufu ya kisheria,” alisema
Hakimu baada kupitia na kugundua kuwa aliyesaini hati hiyo sio anayeonekana
kuitoa.
Washtakiwa wote walitimiza masharti ya dhamana kwa
kuwasilisha wadhamini wawili kila mmoja ambaye ataweka dhamana ya shilingi
milioni 3.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alikuwa
miongoni mwa watu waliohudhuria mahakamani hapo na kuondoka na Salum na wafuasi
hao ambao walifikishwa mahakamani hapo awali chini ya ulinzi mkali. Kesi
imeahirishwa hadi Oktoba 4 mwaka huu