UVCCM YAWATUSI VIONGOZI WA DINI,SOMA HAPO KUJUA
LICHA ya viongozi wa dini kuepusha maafa kwa
kushauri Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kusitisha maandamano na
mikutano yake, wameonekana wapuuzi, anaandika
Dany Tibason.
Umoja wa Vijana wa Chama Cha
Mapinduzi (UVCCM) umeeleza kuwa, usuluhishi wa kisiasa kati ya Chadema na chama
tawala (CCM) si kazi ya viongozi wa dini na taasisi nyingine nchini.
Kauli hiyo imetolewa leo na Shaka Hamdu Shaka, Kaimu
Katibu Mkuu wa UVCCM mbele ya waandishi wa habari mjini Dodoma.
Shaka wamewataka viongozi hao kuacha kabisa
kumsumbua Rais John Magufuli ama kumpotezea muda kwa kutaka kujadili usuluhishi
wa kisiasa kwa kuwa, wao si wanasiasa.
Mbele ya waandishi wa habari jana, Mbowe alisema
maandamano na mikutano inayotaribiwa na chama chake chini ya mwavuli wa Umoja
wa Kupinga Udikteta (Ukawa), yape pale pale na kwamba yamesogezwa mbele mpaka
Oktoba Mosi mwaka huu.
Alisema, uamuzi wa chama hicho ni kusogeza mbele
maandamano hayo ni kupisha mazungumzo baina ya Rais Magufuli na taasisi
mbalimbali nchini zilizoomba maandamano na mikutano hiyo kusogezwa mbele.
Alisema, Chadema kimeridhia maombi ya kusitisha
maandamano na mikutano hiyo nchi nzima yaliyotolewa na viongozi wa dini
mbalimbali pamoja na viongozi wa taasisi za kirai.
Tarehe 27 Julai, mwaka huu Chadema kupitia Mbowe
kilitangaza kuwa, Septemba 1 mwaka huu, kitazindua operesheni ya Umoja wa
Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta), ikiwa ni maazimio ya kikao cha Kamati Kuu ya
chama hicho kilichoketi wa siku mbili.
Akizungumza na wanadishi wa habari Dodoma mbali na
kushambulia viongozi wa dini pia wamezitaka asasi mbalimbali na mashirika ya
hiyari kuachana na mawazo ya kumtafuta rais kwa lengo la kufanya mazungumzo ya
kisiasa.
Wameshauri taasisi hizo kutumia muda huo kwa ajili
ya ya kuzungumzia masuala ya maendeleo tofauti na masuala ya kisiasa.
Pia UVCCM wamesema, serikali haitakuwa na
mazungumzo, majadiliano kati ya Serikali ya CCM na Chadema.
“UVCCM tunatamka bayana kuwa, hakuna mazungumzo,
mijadala itakayojadiliwa kati ya Serikali ya CCM na Chadema.
“Tunaomba Serikali ya Rais John Magufuli iendelee na
mikakati yake ya kisera ili kushamirisha maendeleo ya kiuchumi na juhudi za
utekelezaji wa kuiletea mabadiliko nchi yetu ili kuwa ya viwanda sanjari na kupambana
na maadui umasikini, ujinga na maradhi,” amesema.
Kwa mujibu wa Shaka, Tanzania ni nchi ya amani
ambayo haihitaji kuwepo kwa mazungumzo yoyote ambayo yanalenga kuleta amani.
Shaka mbele ya waandishi wa habari amesema, hoja
zilizotolewa na Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa ChademaTaifa wakati akisitisha
Ukuta hazima mashiko.
“Hoja za Mbowe ni utapeli wa kisiasa, usanii na
mwendelezo wa tamthilia ya kisiasa inayoendelea kufanywa na viongozi wa chama
hicho kwa dhumuni la kujitafutia umaarufu wa kisiasa,” amesema.
Kiongozi huyo amesema, kauli iliyotolewa na Mbowe
kuwa wamesitisha maandamano kwa ajili ya kusikiliza ushauri wa viongozi wa dini
na asasi mbalimbali si ya kweli.
“Sisi UVCCM tunajiuliza ni lini Chadema wamekaa na
viongozi wa dini wakati viongozi hao wa Chadema walikuwa wakimbeza Rais
Magufuli kuwa ni dikiteta? walishariana na viongozi wa dini?
“Kwetu UVCCM wakiwemo wananchi wema wapenda amani na
utulivu, viongozi wa mashirika ya hiari na kiraia na kijamii na viongozi wa
madhehebu mbalimbali ya dini, hatuwezi kusimama hadharani na kuithibitishia
dunia kwamba, Tanzania kuna jambo ambalo linaitwa mgogoro wa kisiasa ambao
unahitaji yafanyike mazungumzo, majadiliano hadi kufikia mapatano” amesema
Shaka.