LOWASSA AMLIPA TAMKO KALI,SOMA HAPO KUJUA

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa
ameandika barua kuhusu operesheni ya chama chake iliyopewa jina la Ukuta na
jinsi ambavyo jeshi la Polisi na Serikali lilivyopanga ‘kuubomoa’.
Katika waraka huo, Lowassa ameeleza kuwa ameamua
kushika kalamu na kuandika masikitiko yake kuhusu hali ya amani nchini akidai
Serikali imekata mkono wa amani.
Ameeleza kuwa Serikali imekandamiza upinzani na
demokrasia na ndio chanzo cha wao kuanzisha UKUTA kupinga ukandamizaji huo.
“Binafsi nafurahishwa na kutiwa moyo na
jinsi watanzania walivyoipokea Operesheni hii, pamoja na vitisho vya dola,”
ameandika. “Siku zote sisi Chadema na Ukawa kwa ujumla ni wenye kulitakia amani
na utulivu Taifa letu. Maandamano haya ya Septemba 1 ni ya amani, lakini
vitendo vya jeshi la polisi vimewapa wasiwasi Watanzania,” Lowassa
ameongeza.
Katika andiko hilo, Lowassa amedai kuwa amekuwa
akipigiwa simu na viongozi wastaafu pamoja na watu mashuhuri wakimshauri
kushawishi wakae na Serikali kuzungumza ili kuepusha taifa kujiingiza katika
machafuko. Aliongeza kuwa kukutana na Rais John Magufuli katika Jubilee ya
miaka 50 ya ndoa ya Rais Mstaafu, Benjamini Mkapa ni sehemu ya juhudi hizo.
“Nyote ni mashahidi wa tukio la kukutana
na Rais Magufuli katika Jubilei ya miaka 50 ya ndoa ya mzee Mkapa. Ulikuwa ni
mwanzo wa juhudi zetu za kuwanyooshea mkono wa amani. Lakini tunashangazwa
wenzetu hawako tayari kuupokea mkono huo,” ameandika.
Aliongeza kuwa katika kikao cha juzi cha ndani cha
chama hicho kilichofanyika katika Hotel ya Giraffe jijini Dar es Salaam
walipanga kuzungumzia jinsi ya kuunyosha zaidi mkono wa amani lakini Jeshi la
Polisi ‘liliukata’.
“Kitendo kile kwangu binafsi kimezidi
kuniimarisha na kunipa nguvu zaidi ya kudai demokrasia na kuheshimu katiba
ambayo viongozi wetu waliapa kuifuata na kuitetea,” unasomeka
waraka wa Waziri Mkuu wa zamani, Lowassa.