UKUTA SASA NGOMA MBICHI,TUNDU LISSU ALALA MAHAKAMANI KISUTU AKIPAMBANA ,SOMA HAPO KUJUA
JAMHURI ya Muungano wa Tanzania imempandisha
kizimbani, Denis Temu, Mkazi wa Tabata Bima, jijini Dar es Salaam kwa madai ya
kushabikia Ukuta, anaandika
Faki Sosi.
Wakati Jamhuri ikiendelea
kuwapandisha kizimbani watuhumiwa mbalimbali, Tundu Lissu, Mwanasheria Mkuu wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ameendelea kushinda mahakamani
kutetea watuhumiwa wa Ukuta.
Ukuta ni Umoja wa Kupinga Udikteta nchini, operesheni
hiyo ilitangazwa na Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema-Taifa Julai mwaka huu
kwa niaba ya Kamati Kuu ya chama hicho.
Operesheni hiyo ilipangwa kuanza kufanyika Septemba
Mosi mwaka huu lakini viongozi wa dini, taasisi za kiraia na serikali ziliutaka
uongozi wa Chadema kutofanya mikutano na maandamano chini ya Ukuta ili kuweka
mazingira sawa ya mazungumzo na Rais John Magufuli.
Temu amepandishwa kizimbani leo kwa tuhuma za
kuandika maneno yanayodaiwa kuwa ya uchochezi kwenye ukurasa wake wa kijamii wa
‘Facebook’ kuhusu Ukuta.
“Nipo tayari kwa Ukuta, naomba
mnikabidhi askari 10, nikiwashindwa Mungu anihukumu.”
Kwenye kesi hiyo iliyopo katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu, mshitakiwa huyo amefunguliwa kesi ya kulidhalilisha Jeshi la
Polisi.
Akisoma shitaka hilo Salumu Mohammed, Wakili wa
Serikali mbele ya Amillius Mchauru, Hakimu Mkazi Mkuu amedai kuwa, mtuhumiwa
huyo aliandika maneno hayo kwenye ukurasa wake wa Facebook.
Mohammed amedai kuwa, mtuhumiwa anadaiwa kutenda
kosa hilo tarehe 30 Agosti mwaka huu.
Kwenye kesi hiyo, Mohammed anawakilishwa na Tundu
Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki.
Hata hivyo, Mohammed amekana shitaka hilo ambapo
amedhaminiwa na wadhamini wawili kwa wadhamini kusaini hati ya Sh. 500,000
kila mmoja.
Upande wa Jamhuri umedai kwamba, upelelezi wa kesi
hiyo bado unaendelea. Kesi hiyo itatajwa tena tarehe 12 Oktoba mwaka huu.
Mtuhumiwa huyo ni miongoni mwa vijana waliokamatwa
na Jeshi la Polisi kabla ya Septemba Mosi.
Jeshi la Polisi na serikali walipinga kuwepo kwa operesheni
Ukuta kwa madai mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutokuwepo kwa hali nzuri ya
usalama nchini.
Wakati akiahirisha maandamano na mkutano ya Ukuta
Mbowe alisema, “tunajua uamuzi
huu utawaumiza sana wafuasi wetu, na uamuzi huu umeniumiza sana hata mimi mwenyewe.
“… lakini ni nani miongoni mwa viongozi wetu na
wanachama wetu ambaye anaweza kuombwa kuahirisha jambo na viongozi wa madhebu
na dini zote hapa nchini na akawakatalia.
“Polisi na Serikali wajue kuwa, hatuahirishi
maandamano na mikutano yetu kwa sababu ya mazoezi, risasi au mabomu ya polisi.
Hatuahirishi kwasababu ya usafi wao, wanaofanya kesho na wala hatuahirishi
kwasababu ya ndege za kijeshi zinazoruka, ila tumeamua kuwaheshimu viongozi
wetu dini.
“Tunawaomba wanachama
wetu, wapenzi wetu na wapenda demokrasia kote nchini watusamehe na wakubali
kuwapa viongozi wa dini hizi wiki tatu, watafute suluhu kwa kuonana na Rais na
ikishindikana, hatutarudi nyuma. Tutaingia barabarani.”
Siku chache baada ya kauli hiyo, Umoja wa Vijana wa
Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) ulikosoa hatua ya viongozi wa dini kuwasihi Chadema
kuendesha maandamano na mikutano ili kutafuta suluhu kutokana na mvutano
uliokuwepo kati ya chama hicho na vyombo vya dola nchini.