KAMPUNI YA ELITE YAGUSWA NA MATATIZO YA WANANCHI WA MABWEPANDE ,YAAMUA KUFANYA HICHI,SOMA HAPO KUJUA
Mwanzilishi wa kampuni ya Elite Organizers Service, Nasra Karl
Mbululo akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kampeni ya
Declutter&Donate ambayo inalenga kuwasaidia wanawake na watoto yatima.
|
Kutokana na hali ya kimaisha kwa wananchi ambao
wanaishi eneo la Mabwepande, Kampuni ya Elite Organizers Service imefanya
uzinduzi wa kampeni ya Declutter&Donate ambayo inalenga
kuwasaidia wanawake wanaoishi eneo hilo ili kuwapatia msaada wa taulo za hedhi
(pad).
Akizungumzia kampeni ya Declutter&Donate ambayo
imezinduliwa Jumanne ya Septemba, 13, Mwanzilishi wa kampuni ya Elite
Organizers Service, Nasra Karl Mbululo alisema kuwa kampeni hiyo imezinduliwa
mahsusi kwa ajili ya kuwasaidia wanawake na watoto yatima.
Alisema kampeni hiyo itahusika na kukusanya vitu ambavyo
havitumiki nyumbani na maofisini na kisha vitauzwa na baadae watakwenda kutoa
taulo za hedhi kwa wanawake 814 ambao wanaishi eneo la Mabwepande.
Kwa upande wa watoto yatima, Nasra alisema kuwa watakusanya vitabu
na midoli kutoka kwa watu mbalimbali ambao watakuwa tayari kujitolea na baadae
watapeleka katika moja ya kituo ambacho watakichagua.
“Kuna vitu tunakuwa navyo majumbani kwetu au ofisini na
hatuvitumii, hivyo vitu sisi tunaviomba na tutakwenda kuviuza na kuwagawia
wanawake waliopo Mabwepande, ukiangalia mazingira ambayo wanaishi wengine
nyumba zao hata bati hawana kwahiyo kutumia pesa kununua pad (taulo za hedhi)
anaona bora anunue chakula au kuongeza ili ajenge kwahiyo sisi tutawapa
pad ili kupunguza gharama,
“Pamoja na hilo pia tutakuwa tunachukua na vitabu na toys (midoli)
ambayo majumbani hawaitumi na sisi tutakusanya vitu hivyo na kwenda kuwagawia
watoto yatima kwenye kituo cha kulelea,” alisema Nasra.
Aidha alisema kuwa, watatoa mafunzo kwa wanawake wa Mabwepande
ambayo yataongozwa na Mshauri Mwandamizi wa Life Style, Sadaka Gandi ambaye
atawapa mafunzo wanawake hao kuhusu mambo mbalimbali yanayohusu afya.
Pia alisema kuwa hivi karibuni watatangaza vituo ambavyo
vitatumika kukusanya vitu ambavyo vitakuwa vinatolewa na hivyo kwa yoyote
ambaye ataguswa na kampeni hiyo atakuwa akipeleka msaada wake katika vituo
hivyo.