MAJAMBAZI WAENDELEA KUTIKISA TENA,WAFANYA UNYAMA HUU,SOMA HAPO KUJUA
Majambazi wapatao 10 juzi usiku walivamia magari
mawili yaliyobeba wafanyabiashara waliokuwa wakitokea mnadani na kumuua kwa
risasi, dereva aliyegoma kuwapa fedha na simu.
Dereva huyo, Chrispin Inyangwe (40) alipigwa risasi
ya mgongoni alipojaribu kupambana nao.
Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana eneo la
katikati ya vijiji vya Miula na Kalundi vilivyopo Kata ya Kipande wilayani
Nkasi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando
alisema wafanyabiashara hao walikuwa wakitokea mnadani na walipofika eneo hilo
walikuta mawe yamepangwa barabarani kuzuia magari.
Alisema baada ya kuona mawe hayo, magari hayo
yalilazimika kusimama na ndipo majambazi hao waliokuwa na silaha za moto,
mapanga na marungu walipoibuka na kufyatua risasi hewani na baadaye kutaka
wafanyabiashara hao wasalimishe fedha na simu zao za mkononi.
Kamanda huyo alisema baadhi ya wafanyabiashara
walisalimisha fedha na simu zao, na waliokataa walishambuliwa.
Inasemekana kwamba Inyangwe ambaye alikuwa dereva wa
gari aina ya Mitsubishi Canter alikaidi kutoa fedha na kutaka kupambana nao,
ndipo watu hao waliokuwa na bunduki aina ya SMG walipomfyatulia risasi
iliyompata mgongoni na kufariki dunia papo hapo.
Kitendo hicho kiliwafanya wafanyabiashara wengine
waliokuwa wakikataa kutoa fedha, kuzisalimisha sambamba na simu zao, ndipo
majambazi hao walipowaachia na kukimbia.
Watu 19 waliojeruhiwa walipelekwa Hospitali ya Mkoa
mjini Sumbawanga. Kamanda Kyando alisema majeruhi 12 waliruhusiwa kurejea
nyumbani na wengine saba wanaendelea na matibabu na kwamba polisi wanaeendelea
na msako wa watu hao.