SHEIKH PONDA AVUNJA UKIMYA,AFUNGUKA KUHUSU HALI NGUMU YA MAISHA KWA WATANZANIA,SOMAHAPO KUJUA
FURAHA tuliyokuwanayo Watanzania, sasa haipo tena.
Ni wakati wa kuhoji, kwanini maisha yamekuwa magumu kiasi hiki?, anaandika Faki Sosi.
Ni kauli ya Sheikh Ponda Issa
Ponda, Katibu Mkuu wa Jumuiya na Taaisi za Kiislam Tanzania aliyoitoa leo
akizungumza na mwandishi wa habari hii wakati akitoa salamu zake kuelekea
Sikukuu ya Eid El Hajj.
Kesho duniani kote, waumini wa Dini ya Kiislam
wanatarajia kusherehekea Sikukuu ya Eid el Hajj ikiwa ni sehemu ya ibada kwa
mujibu wa imani ya dini hiyo.
Sheikh Ponda amesema, pamoja na kuwepo kwa sherehe
hiyo lakini kuna hali ya masikitiko kwa Watanzania kutokana na vipato vya
kushukwa jambo ambalo limeonda furaha ndani ya mioyo na familia zao.
Amesema, sikukuu zilizopita katika kipindi kama hiki
watu waliweza kutoa sadaka, kulisha masikini, kuchinja kwa ajili ya ibada na
kufanya ibada zingine zilizohusisha kipato.
Lakini kutokana na maisha kubadilika, waumini wa
dini hiyo wameshindwa kutekeleza yale waliyokuwa wakiweza kuyatekeleza siku za
nyuma jambo ambalo linahitaji kutafakari upya mtindo wa maisha ulivyo kwa sasa.
“Tunaelekea kwenye sikukuu lakini jambo ninaloliona
kwa sasa ni kwamba, tunapaswa kutafakari upya, kwanini maisha yamekuwa magumu
kiasi hiki?
“Siku za nyuma kulikuwa na furaha kubwa hasa wakati
wa sikukuu kama huu lakini sasa mambo yamebadilika kwa kiwango kikubwa.
“Watu hawana furaha, maisha yamekuwa magumu. Ni
kipindi cha kutafakari kwa mwaka mzima uliopita, tatizo ni nini zaidi?” amesema
Sheikh Ponda.
Akizungumzia falsafa ya Hijja Sheikh Ponda amesema,
yapo mambo mengi yanayopatikana pale watu wanapotekeleza ibada hiyo.
Amesema, miongoni mwa hayo ni pamoja na kuonesha
umoja “kuvaa mavazi ya aina moja, ni kiashirio cha umoja kwamba, pamoja na kuwa
watu wanatoka kwenye mataifa mbalimbali, bado wanaunganisha na Uislam.
“Watu wanakutana wakiwa na wadhifa tofauti, mataifa
tofauti na uwezo tofauti lakini ndani ya mavazi yake, kila mmoja yupo sawa na mwingine,
tunapaswa kuishi maisha ya namna hii,” amesema na kuongeza;
“Falsafa ya kurusha mawe kumpiga shetani ni
kiashirio cha kujenga ujasiri katika kukabiliana na yale yote yanayoweza
kumyumbisha muumini.”
Hata hivyo amewataka Waislam na Watanzania kwa ujumla
kusherehekea sikukuu kwa njia ya amani sambamba na kuchunga miiko na taratibu
za dini hiyo popote watakapokuwa.
Akizungumzia tukio la tetemeko lililotokea jana
Kanda ya Ziwa (Kagera, Mwanza, Mara, Shinyanga) na kusababisha vifo pia hasara
Sheikh Ponda amewapa pole waliofikwa na mkasa huo.
“Nikiwa kama Katibu wa Taasisi na Jumuiya za Kiislam
Tanzania, natumia nafasi hii kuwapa pole wale wote waliofikwa na mkaza wa
tetemeko la ardhi lililotokea jana Kanda ya Ziwa na nchi jirani.
“Yote yanayotokea yanaletwa na Mungu hivyo hatuna
budi kujiandaa kwa kutenda mambo mema ili yatufae kwenye maisha baada ya dunia
hii,” amesema.