NAIBU SPIKA AANZA UBABE WAKE KWA WABUNGE WA UKAWA,SOMA HAPO KUJUA
Mvutano umeibuka kati ya Naibu Spika, Dk Tulia
Ackson na wasemaji wa kambi ya upinzani walipokuwa wakisoma maoni yao kuhusu
miswada iliyowasilishwa bungeni baada ya kusoma utangulizi uliokuwa nje ya
hoja.
Katika Bunge la Bajeti lililoisha Juni mwaka huu,
upande wa Kambi ya Upinzani Bungeni uliingia kwenye mgogoro na Dk Tulia, hali
iliyosababisha wabunge kutoka vyama vinavyounda Ukawa (Umoja wa Katiba ya
Wananchi) kutoka bungeni kila Naibu Spika alipokuwa akiendesha vikao.
Jana, ilikuwa mara ya kwanza tangu wabunge wasusie
vikao vinavyoendeshwa na Dk Tulia kukubali kuwapo ndani ya Bunge, hatua
iliyotokana na viongozi wa dini kuingilia kati sakata hilo.
Tangu kuanza kwa Mkutano wa Nne wa Bunge la 11,
imepitishwa miswada miwili huku wapinzani wakisoma utangulizi wa maoni kueleza
jinsi wanavyobanwa kufanya shughuli za siasa.
Hata hivyo, jana ilikuwa ni tofauti baada ya Dk
Tulia kuwabana wawasilishaji wa miswada ya Sheria ya Uanzishaji wa Mamlaka ya
Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, ambao ulisomwa na Dk Godwin Mollel na
aliyesoma Muswada wa Uanzishaji Baraza la Watalaaluma wa Kemia ni Ester Matiko.
Katika maoni yao, Matiko na Dk Mollel walieleza
jinsi Polisi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wanavyowapiga na
kuwakamata wananchi wanaojadili masuala ya siasa. Dk Mollel alipinga watu
kunyimwa haki ya kutoa maoni, kufanya mikutano ya hadhara na maandamano.
“Tupinge unyama unaondelea dhidi ya Watanzania wenzetu,” alisema Dk Mollel.
Hata hivyo, kabla ya kumaliza kile alichokuwa
akitaka kusema Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Ajira, Kazi, Vijana
na Walemavu), Dk Abdallah Posi aliomba mwongozo kwa kutumia kifungu namba 68
(1) akitaka msemaji kujielekeza katika hoja kama kinavyotaka kifungu 86.
Baada ya Dk Tulia kutoa mwongozo wa kutaka kuacha
kusoma maneno ya utangulizi huo, Dk Mollel alitii na kuendelea na hoja
iliyokuwa mezani.
Hali ilizidi kuwa mbaya baada ya Matiko kuingia kusoma maoni ya kambi hiyo kuhusu Muswada wa Sheria ya Uanzishwaji wa Baraza la Wanataaluma wa Kemia.
Hali ilizidi kuwa mbaya baada ya Matiko kuingia kusoma maoni ya kambi hiyo kuhusu Muswada wa Sheria ya Uanzishwaji wa Baraza la Wanataaluma wa Kemia.
“Watanzania wote wenye mapenzi mema tupinge vyombo
vya dola vinavyotumika kufanya shughuli za siasa,” alisema
Matiko.
Licha ya Dk Possi kuomba mwongozo wa Spika, Matiko
aliendelea kusoma maneno ya utangulizi ambayo aliambiwa asiyasome.
Wakati mvutano huo ukiendelea, baadhi ya wabunge wa
upinzani walisimama kupinga uamuzi wa Dk Tulia wakitaka wasemaji hao kuendelea
kusoma utangulizi.
Hata hivyo, Dk Tulia aliwataka kukaa chini huku
akimtaja Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee kwa zaidi ya mara mbili akimsihi
kukaa hali aliyokubaliana nayo.