RAIS MAGUFULI AONYWA TENA,NI KUHUSU KAULI ZAKE,SOMA HAPO KUJUA
BARAZA la Wazee wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) limeonya kauli zinazotolewa na Rais John Magufuli katika mikutano
yake, anaandika Pendo Omary.
Baraza hilo limeeleza kuwa,
kauli hizo zinaweza kusababisha matatizo kwa nchi hususani wakati huu.
Kauli hiyo imetolewa leo na Roderick Lutembeka,
Katibu Mkuu wa Baraza mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Amesema, Rais Magufuli akiwa katika ziara Zanzibara
tarehe 2-3 mwezi huu, alitoa matamko yaliyolenga kuchochea uhasama na chuki na
kutishia ustawi wa umoja wa kitaifa.
“Rais alisikika akiupongeza ukiukwaji wa demokrasia
uliofanyika visiwani Zanzibar kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka jana na kudhihaki
kwa kupendekeza msimamizi wa uchaguzi aliyehusika kuvurugu uchaguzi apewe tuzo
na Rais Ali Mohammed Shein.
“Rais anapaswa kutafuta suluhisho na mwafaka kwa
ajili ya Wanzanzibari na Watanzania wote,” amesema Lutembeka.
Pia amesema, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji
Francis Mtungi kupitia Kamati ya Uongozi ya Baraza la Vyama vya Siasa
anakihujumu chama hicho.
Lutembeka amesema, kulingana na mtiririko wa matukio
kadhaa yaliyojitokeza hivi karibuni ikiwemo kuandaa mitego haramu ya kisiasa
ili hatimaye yatolewe mapendekezo ya kukifuta Chadema katika orodha ya vyama
vya siasa.
“Tarehe 15 Agosti mwaka huu Jaji Mtungi alitangaza
kuwa, Baraza la Vyama vya Siasa lilikuwa limeitisha kikao ambacho kingefanyika
tarehe 29-30 Agosti kujadili masuala hali ya kisiasa nchini. Siku mbili kabla
ya kikao Mwenyekiti wa baraza akatangaza kukiahirisha hadi tarehe 3-4 mwezi
huu.
“Jambo la kushangaza baada ya busara kutumika
kupitia viongozi wa dini kushawishi Chadema kuahirisha kwa kutoa mwanya wa
mazungumzo hadi tarehe 1 mwezi huu, Kamati ya Uongozi wa Baraza la Vyama vya
Siasa ikaibuka tena na kutangaza kuahirisha kikao cha baraza hadi
itakapotangazwa tena.
“Wakati taarifa zote hizo zikitolewa na viongozi wa
baraza, ofisini hapa (Chadema) hakuna hata barua moja kutoka kwa msajili ya
kutuita katika kikao chochote kati ya hivyo. Kuanzia kile cha tarehe 29-30
Agosti, tarehe 3-4 Septemba wala hiyo ya kuahirisha.
“Katika mazingira haya nani ambaye hatashawishika
kuamini ofisi ya msajili inatii maagizo ya watawala,” amehoji Lutembeka.