KIZIMBANI KWA KUMTISHA RAIS MAGUFULI,SOMA HAPO KUJUA
Mfanyabiasha Leonard Materu (31) amepandishwa
kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashitaka ya
kutuma ujumbe wa kumtishia Rais John Magufuli kupitia mtandao wa WhatsApp.
Materu ambaye ni mkazi wa Moshi Bar Kwadiwani,
alifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka yake na Wakili wa
Serikali, Diana Lukondo mbele ya Hakimu Mkazi Magreth Bankika.
Akisoma mashitaka Wakili Diana alidai, mshitakiwa
huyo amefunguliwa kesi hiyo ya kuchapisha taarifa za uongo kwenye mtandao wa
WhatsApp chini ya Sheria ya Mtandao ya mwaka 2015.
Ilidaiwa kuwa, Julai 17, mwaka huu jijini Dar es
Salaam, Materu aliandika ujumbe wenye lengo la kudanganya umma kupitia WhatsApp
ukisomeka; “Magu ajiandae tunaenda kupindua mpaka Ikulu.”
Inadaiwa kuwa maneno hayo yalikuwa na lengo la
kumtishia Rais John Magufuli. Baada ya kusomewa mashitaka, mshitakiwa alikana
kutenda kosa hilo, na upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi
haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Mshitakiwa aliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza
masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili ambao kila mmoja alisaini hati
ya Sh milioni tano. Kesi itatajwa tena Septemba 20, mwaka huu.