Zinazobamba

MSAJILI WA VYAMA AONYWA,WABUNGE WA CUF WAMJIA JUU,SOMA HAPO KUJUA



WABUNGE wa Chama cha Wananchi (CUF), wamemtaka Jaji Francis Mutungi kutotumika kukiyumbisha chama hicho kwa maslahi ya serikali na chama tawala, anaandika Charles William.

Riziki Shari Mngwali, Kiongozi wa wabunge wa CUF
Katika tamlo la wabunge hao lililotolewa leo mjini Dodoma, wameeleza kuwa, taratibu zote za kumuweka kando Profesa Ibrahim Lipumba aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho kabla ya kujiuzulu zilifuatwa na kuwa ni vyema msajili, akajihadhari na kutumika kukiingilia chama hicho.

Lifuatalo ni tamko kamili la wabunge hao;
Ndugu waandishi wa habari,
Sisi wabunge wa THE CIVIC UNITED FRONT (CUF- Chama Cha Wananchi) tunatumia fursa hii kumsihi Msajili wa vyama vya siasa nchini, Jaji Francis Mutungi kutokubali kutumika kukiyumbisha chama chetu cha CUF, kutokana na baadhi ya wanachama wenye nia ovu dhidi ya CUF wakishirikiana na vyombo vya dola na serikali ya CCM kutaka kuitumia ofisi yake kwa madhumuni hayo.


Kama tunavyofahamu, mwaka jana tarehe 5 Agosti, aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF Taifa, Prof. Ibrahimu Lipumba kwa hiyari yake alijiuzuru yake hiyo kwa kuutangazia umma wa watanzania pale Peacock Hotel na kumuandikia rasmi Katibu Mkuu wa CUF juu ya uamuzi huo na baadaye akaelekea nchini Rwanda kwa kazi aliyodai kuwa za utafiti wa kiuchumi ili aje kuisaidia serikali ijayo ambayo kwa vyovyote alitegemea kuwa itakuwa ni ya CCM.
Chama cha CUF na wagombea wake wote nchi nzima tuliendelea na kampeni bila msaada wala ushawishi wake na baada ya uchaguzi chama chetu kikaimarika zaidi kwa kupata wabunge 43, madiwani 287, kuongoza Manispaa mbili na Halmashauri za wilaya tatu. Pia  kwa ushirikiano na vyama rafiki vya UKAWA tumeweza kupata viongozi katika manispaa mbili za Jiji la Dar es Salaam pamoja na kuongoza jiji lenyewe.
Baada ya chama kupita katika wakati mgumu  chini ya uongozi wa mpito na kupata mafanikio makubwa bila Prof. Lipumba, Baraza kuu la Uongozi Taifa  katika kikao chake cha tarehe 2-3 April, 2016 liliamua kuitisha Mkutano Mkuu Maalumu wa Taifa kujaza nafasi wazi za uongozi ndani ya chama kwa mujibu wa katiba.
Maandalizi ya Kikao cha Mkutano Mkuu yalikamilika na mkutano huo kufanyika Ubungo Plaza (Blue Pearl Hotel) tarehe 21/8/2015. Mkutano Mkuu Maalum huo ulikuwa na ajenda mbili, ajenda ya kwanza ilikuwa ni kukamilisha matakwa ya ibara ya 117 (2) ya Katiba ya CUF inayoongelea mamlaka ya mkutano mkuu kukubali kujiuzulu kwa kiongozi ambaye amechaguliwa na au kuteuliwa na ngazi husika.
Wajumbe 476 sawa na asilimia 70 ya wajumbe wote waliohudhuria mkutano mkuu huo walithibitisha nakukubali kujiuzulu kwa Prof Ibrahimu Lipumba na ajenda ya kwanza ikakamilika.
Katika hali isiyotarajiwa na bila mualiko rasmi Prof Lipumba aliingia kwa nguvu ndani ya ukumbi wa mkutano na kusababisha kuzuka kwa vurugu kubwa kutoka kwa baadhi ya wajumbe wachache waliokuwa wanamuunga mkono. Hata hivyo vurugu hizo zilidhibitiwa na mkutano ukarejea na kuendelea kwa amani na ajenda kwanza ikajadiliwa na kufanyiwa maamuzi.
Kikao kiliporejea baada ya mapumziko ya mchana kiliendelea na ajenda ya pili ya kujaza nafasi wazi za viongozi ikiwemo ya Mwenyekiti wa chama Taifa. Ghafla wakati kamati ya uchaguzi ya ndani ya chama ikianza majukumu yake kundi la vijana wahuni lililokodiwa kuja kufanya vurugu kwa ajili ya kumsaidia Prof Lipumba lilivamia ukumbi na kusababisha vurugu kubwa hali iliyopelekea mwenyekiti wa mkutano kuuahirisha rasmi mkutano huo bila ya kukamilisha ajenda ya pili.
Vurugu hizo zimekisababishia Chama hasara kubwa ya takribani Shilingi milioni 600 za Kitanzania na uharibifu wa mali za hotel kiasi cha shilingi milioni 8.7. Hali hii inadhihirisha wazi kuwa Prof Lipumba hakuwa na nia njema na  alidhamiria kuvuruga mustakbali wa Chama.
Baraza Kuu la Uongozi la CUF Taifa lililokutana, kwa mujibu wa Katiba, tarehe 28/8/2016 lilifanya maamuzi ya kuwasimamisha uanachama wanachama kadhaa akiwemo Prof Lipumba na Magdalena Sakaya (Naibu Katibu Mkuu Bara) na kumvua uanachama Mhe. Shashu Lugeye baada ya kupewa nafasi ya kujitetea na kusikilizwa. Wanachama waliosimamishwa wameshaandikiwa barua za kujulishwa juu ya uamuzi huo ambao pia unawapa nafasi ya kujitetea kwa mujibu wa Katiba ya CUF.
Ndugu waandishi wa habari,
Sisi wabunge tunaotokana na chama cha CUF katika bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tunaunga mkono hatua ya Baraza kuu la uongozi Taifa kuwachukulia hatua za kinidhamu wanachama wote waliohusika na vitendo vinavyokiuka katiba ya chama chetu, malengo yake na utamaduni wake.
Baada ya hatua hizo za Baraza Kuu la uongozi la Taifa ambazo kwa kweli bado zinaendelea, tulipata taarifa kuwa Prof. Lipumba na wenzake walipeleka malalamiko yao kwa Msajili wa vyama vya siasa, lakini pia tumemshuhudia akiwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari akijitangaza kuwa yeye ndiye ‘mwenyekiti halali’ wa CUF na kwamba anasubiria tu barua ya Msajili wa vyama vya siasa ili kuthibitishiwa uenyekiti wake.
Prof. Lipumba anafanya haya huku akitambua kuwa Baraza Kuu lililokutana tarehe 28 Agosti, 2016 likiwa na akidi halali pande zote za muungano, lilikwishateua kamati ya Uongozi wa Chama Taifa ambayo inapaswa kufanya na kutekeleza majukumu ya Ofisi ya Mwenyekiti Taifa kwa mujibu wa katiba yetu. Tunataka ifahamike kwa dhati kuwa, sisi wabunge, hatumtambui tena Prof. Lipumba kama Mwenyekiti wa CUF, kwa sasa CUF inaongozwa na Kamati ya Uongozi ya CUF Taifa chini ya Julius Mtatiro. Haya yote yamefanywa kwa mujibu wa katiba ya CUF na vikao halali vya CUF.
Hata hivyo, tumepata taarifa kutoka kwa vyanzo vinavyoaminika serikalini kuwa kuna njama zinazopangwa na washindani wetu wa kisiasa Chama Cha Mapinduzi (CCM), vyombo vya ulinzi na usalama na serikali ya CCM kutaka kuitumia ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa kumtangaza Prof Ibrahimu Lipumba kuwa Mwenyekiti halali wa CUF.
Dhumuni la yote hayo ni kutaka kukiyumbisha chama chetu na kutupandikizia mgogoro usiopaswa kuwepo. Kama kitendo hicho kikifanyika kitakuwa kinyume kabisa na katiba, kanuni na taratibu za chama chetu, lakini kitakuwa kinyume na sheria ya Vyama vya siasa namba 5 ya mwaka 1992 ambayo haitoi mamlaka yoyote kwa Msajili wa vyama vya siasa kukipangia chama cha siasa viongozi wake.
Ndugu waandishi wa habari,
Sisi kama wabunge na wawakilishi wa wananchi, tunatoa tahadhari kwa Msajili wa vyama vya siasa na wale wote wanaotaka kutumika kukiingiza chama chetu cha CUF katika mgogoro usiopaswa kuwepo na kurudisha nyuma jitihada za kudai haki na demokrasia ndani ya nchi yetu, kuacha njama hizo mara moja kwa sababu tumekwishazibaini na kwa gharama yoyote tuko tayari kukilinda chama chetu na kushirikiana na uongozi halali uliopo dhidi ya maadui wa ndani na nje. Tunawahakikishia watanzania kwamba maadui hawa hawatafanikiwa kutuyumbisha.
Tuna uhakika kuwa, chama chetu kimefuata taratibu zote za kikatiba kushughulikia suala hili na kwamba katiba ya CUF haitoi nafasi kwa kiongozi aliyejiuzuru kwa hiyari yake mwenyewe kutengua maamuzi yake ya kujiuzulu. Mamlaka iliyomchagua kwa mujibu wa ibara ya 117(2) ya Katiba ya CUF imekamilisha wajibu wake katika Mkutano Mkuu Maalumu uliofanyika Blue Pearl hotel tarehe 21/8/2016.
Tunashangazwa ni katiba ipi ya CUF ambayo vyombo vya ulinzi na usalama, CCM na serikali yake vinataka kuitumia ili kumuuzia Msajili kesi ya kumrejesha Prof Lipumba madarakani?
Tunamtahadharisha Msajili wa vyama vya siasa atakapotoa maoni yake kuhusu malalamiko yoyote yaliyopelekwa kwake asikubali kujivunjia heshima yake kubwa akiwa Jaji aliyehudumu katika Mahakama Kuu ya Tanzania.
Kwa vyovyote vile maoni na ushauri wa Msajili juu ya jambo hili, hayapaswi kwenda kinyuma na katiba ya CUF, Sheria ya vyama vya siasa na kanuni na taratibu za uendeshaji wa shughuli za vyama vya siasa nchini.
Katika kile kinachoonekana kuwa Msajili anaweza kushiriki katika njama hizo ovu, tayari Prof. Lipumba na timu ya watu wachache wanaomuunga mkono wameanza maandalizi mbalimbali ya kuchapisha fulana za kumpokea katika Ofisi Kuu ya CUF muda wowote kuanzia sasa na kinachosubiriwa ni tangazo la Msajiri wa vyama vya siasa kama ambavyo Prof. Lipumba amekuwa akitangaza kwenye vyombo vya habari.
Mpango wa kuendelea kumlinda Lipumba (kama ambavyo Polisi walikubali kutumika na kumlinda yeye na makundi ya vijana waliovamia na kuufanya mkutano mkuu maalumu wa Agosti 21 uahirishwe bila kumaliza ajenda ya pili kwa sababu za kiusalama) unasukwa kwa njama za juu na tunazo taarifa kuwa wanaandaliwa watu watakaovamia na kuiteka Ofisi Kuu ya CUF Buguruni, kufanya vurugu na kumsimika Prof. Lipumba kwenye nafasi ya uenyekiti na baadaye kusaidiwa na serikali ya CCM kuzunguka nchi nzima kufanya vikao vya ndani ili kujaribu kuimaliza CUF. Njama zote hizi tunazijua.
Sisi wabunge wa CUF ambao ni wawakilishi wa wananchi tutasimama imara kukilinda na kukitetea chama chetu dhidi ya njama zote hizo. Tutaendelea kupambana na yeyote ambaye ataonekana anataka kutumiwa kukivuruga chama na hatutakubali kuyumbishwa. Tunatambua umuhimu wa kuheshimu katiba za vyama na kuheshimu maamuzi halali ya vikao halali vya vyama vya siasa.
Kwa vyovyote vile hatutegemei kuwa Msajili wa vyama vya siasa atakubali kutumika katika mkakati huu uliojaa uovu. Pamoja na kumheshimu sana, tunatumia fursa hii kumtahadharisha kwamba CUF iko macho, inajua yanayoendelea kila pembe ya nchi na tuko tayari kuyakabili.
Ndugu waandishi wa habari,
Tunatumia fursa hii pia kumshauri Prof. Lipumba na kumjulisha kuwa tunamheshimu sana na aliyokitendea chama hiki yanatosha. Haiwezekani Prof. Lipumba huyu huyu tumjuaye na ambaye huko nyuma amewahi kusimamia maamuzi ya Baraza Kuu na mikutano mikuu kadhaa ya CUF, leo aanze kuzunguka huku na kule kupinga maamuzi ya mikutano hiyo.
Ni Prof. Lipumba huyu huyu ndiye alisimamia vikao vya Baraza Kuu vilivyopitia madai na tuhuma kwa baadhi ya viongozi wa chama na akasimamia maamuzi ya hatua za kinidhamu dhidi ya viongozi hao. Mmoja wa viongozi waliowahi kuchukuliwa hatua kali mtakumbuka ni Ndugu. Chief Lutayosa Yemba.
Hiyo ina maana kuwa katiba ya CUF inayo mamlaka juu ya wanachama wote akiwemo yeye Lipumba. Kwa sababu hivi sasa ameshasimamishwa uanachama ni vema atoe ushirikiano kwa chama katika hatua zinazofuata za kusikiliza utetezi wake na kuheshimu maamuzi ya vikao halali vya chama. Chama cha CUF ni taasisi kubwa ya kisiasa nchini na kamwe haitakubali kuyumba wala kuyumbishwa kwa namna yeyote ile.
Tunatoa wito kwa wanachama wenzetu wote na viongozi kwa ujumla kuwa wastahamilivu katika kipindi hiki na tuelekeze nguvu zetu katika kukiimarisha zaidi chama chetu ili kwa kushirikiana na vyama rafiki ndani ya UKAWA tuweze kupigania haki na demokrasia inayoonekanwa kutaka kubanwa na utawala wa serikali ya awamu hii ya tano.
“HAKI SAWA KWA WOTE”
IMETOLEWA NA WABUNGE WA CUF LEO TAREHE 15 SEPT 2016.
RIZIKI SHAHARI MNGWALI   –
KIONGOZI WA WABUNGE WA CUF
JUMA KOMBO HAMAD – KATIBU WA WABUNGE WA CUF.