KUMENUKA CCM,VIJANA WAKE WAANZA KUSHIKANA UCHAWI,SOMA HAPO KUJUA
TUHUMA za Lengai Ole Sabaya, Mwenyekiti wa Umoja wa
Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Mkoa wa Arusha, kufanya utapeli na
kujipatia fedha kwa kujitambulisha kama ofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa
(TISS), limezidi kukivuruga chama hicho, anaandika Charles William.
Mapema leo asubuhi, baadhi ya
wanachama wa UVCCM wametwangana makonde, baada ya baadhi yao kutaka kuifunga
ofisi ya chama hicho, wakidai mwenyekiti wao, Sabaya ambaye pia ni diwani wa
kata ya Samabashi wilaya ya Arumeru, hana tena uhalali wa kuungoza umoja huo.
Sabaya anadaiwa kujihusisha na vitendo vya utapeli
mkoani Arusha kwa muda sasa huku akilindwa na baaadhi ya vigogo wa CCM sambamba
na Jeshi la Polisi mkoani humo ambalo linalaumiwa kutomkamata wala kumfikisha
mahakamani kila anaposhitakiwa.
Watoaji wa tuhuma hizo wamesambaza katika mitandao
baadhi ya nyaraka zinazoonesha vitambulisho ‘feki’ vinavyomtambulisha Sabaya
kama ofisa usalama wa taifa, lakini pia wameonyesha kile wanachodai kuwa ni
‘RB’ za Jeshi la Polisi ili kijana huyo akamatwe.
Hata hivyo, Sabaya amemwambia mwandishi wa Chanzo Changu kwa
kifupi kuwa, tuhuma hizo zinasambazwa na wasiopenda kazi yake ya kukinyoosha na
kukirudisha chama hicho katika misingi mkoani Arusha, hata hivyo hakufafanua
undani wa tuhuma hizo.
“Wanaonituhumu wanafanya kazi kwenye karakana ya
ibilisi, hivi karibuni ngano na magugu vitatengwa. Mimi sitoacha kupambana na
rushwa za kihalifu ndani ya miradi ya UVCCM Mkoa na viongozi wote waliohusika
na hili lazima wawajibishwe,” amesema Sabaya na kuongeza;
“Utasikia makubwa zaidi hadi nitakapomaliza kazi ya
kuileta CCM anayoitaka Rais Magufuli hapa Arusha.”
Sabaya hakuwa tayari kueleza kuhusu kitambulisho cha
idara ya usalama wa taifa kinachodaiwa kuwa chake, hakutaka pia kufafanua
kiundani kuhusu watu mbalimbali kumshitaki kwa utapeli huku kesi hizo zikidaiwa
kuzimwa na Jeshi la Polisi mkoani Arusha.
Chanzo changu kilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Arusha Charles Mkumbo kwa kumpigia simu zaidi ya mara nne ili atoe ufafanuzi wa
suala hilo, hata hivyo simu yake iliita bila kupokelewa.
Alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi ‘SMS’ hakuweza
kujibu ujumbe huo licha ya kumfikia.
Shaka Hamdu, Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM taifa, amesema
kuwa tayari yupo mkoani Arusha, kutafutia ufumbuzi wa vurugu baina ya vijana wa
umoja huo ikiwa ni pamoja na kufungwa kwa ofisi kwa nguvu na mwenyekiti wa
umoja huo kudaiwa kukataa kumpokea Katibu wa UVCCM Mkoa aliyepangiwa kazi hivi
karibuni.
“Nipo Arusha tayari, nashughulikia suala hili na
nitalitolea tamko leo leo,” amesema Shaka kwa njia ya simu.