MAJAMBAZI YAENDELEA KUTIKISA NCHI,SOMA HAPO KUJUA
Majambazi zaidi ya 15 yamevamia Chuo Kikuu cha
Kumbukumbu ya Sebastian Kolowa (Sekomu) kilichopo Kata ya Magamba, Lushoto
mkoani Tanga na kuua mlinzi mmoja, kumjeruhi mwingine baada ya kumpiga risasi
begani, kuchoma mabweni na kuharibu mali za wanafunzi waliokuwepo chuoni hapo.
Tukio la majambazi hao kuvamia chuo hicho limetokea
usiku wa kuamkia jana wakati hali ya taharuki ikiwa bado haijasahaulika kwa
wakazi wa Vikindu wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani baada ya usiku wa kuamkia
Ijumaa ya wiki iliyopita Kikosi Maalumu cha Jeshi la Polisi cha Kupambana na
Uhalifu kupambana na genge la watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi au magaidi
waliokuwa wakiishi katika nyumba iliyopo eneo hilo.
Wakati tukio la chuoni hapo nalo likiibua shaka,
hofu na maswali baada ya majambazi hayo kutoiba chochote licha ya kutekeleza
uhalifu huo, lile la Vikundi ambalo msingi wake ulikuwa ni operesheni ya
kuwasaka majambazi waliowaua askari wanne wiki iliyopita waliokuwa
wakibadilishana zamu ya kulinda Tawi la Benki ya CRDB lililoko Mbande wilayani
Temeke jijini Dar es Salaam, likiwa limegubikwa na utata na sintofahamu huku
Kamanda wa Kikosi Maalumu cha Kuzuia Uhalifu, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Thomas Muniko, akiuawa kwa kupigwa risasi.
Licha ya majambazi hayo kutekeleza tukio hilo baada
ya kuvamia na kufunga milango kwa nje na kumwaga mafuta na kuchoma moto mabweni
huku baadhi ya wanafunzi wakipiga kelele za kuomba msaada na wengine kufanikiwa
kutoka kupitia madirisha ya vyoo, lakini Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga,
Benedict Wakulyamba, amesisitiza kuwa kilichotokea chuoni hapo ni ujambazi na
si ugaidi.
Akizungumzia tukio hilo jana kwa waandishi wa habari
akiwa chuoni hapo, Wakulyamba, alithibitisha kuwa lilihusisha majambazi kati ya
10 hadi 15 waliovamia chuoni hapo na kuchoma vyumba vya mabweni mawili tofauti
ya wanafunzi.
“Tukio hilo ni la ujambazi na si ugaidi.
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa itakaa kikao na kulijadili tukio hilo kisha
tutatoa taarifa,” alisema.
Wakulyamba alisema katika tukio hilo mlinzi mmoja wa
chuo hicho, Yohana Shemzigwa (34), aliuawa kwa kupigwa na kitu kizito mgongoni
na kichwani huku mlinzi mwenzake, Abuu Rajabu, naye amejeruhiwa na majambazi
hayo baada ya kupigwa risasi begani.
Pia alisema kuwa majambazi hayo yaliteketeza kwa
moto mabweni mawili na kusababisha magodoro, nguo na simu za viganjani za
wanafunzi wa chuo hicho kuungua.
Wakulyamba alisema mmoja kati ya majambazi hayo
alijeruhiwa vibaya wakati akitekeleza unyama huo baada ya walinzi wa chuo hicho
kutaka kumkamata na amepelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Lushoto chini ya
ulinzi wa polisi huku akiwa mahututi.
Katika hatua nyingine, alitangaza msako wa kuwasaka
majambazi hayo ili kuwafikisha katika vyombo vya sheria ili kujibu tuhuma
zinazowakabili.
“Niseme kuwa sisi kama Jeshi la Polisi
tutawatafuta wahusika wa tukio hili popote walipo usiku na mchana, wawe
mapangoni au nchi kavu lazima tutawakamata na kuwafikisha katika vyombo vya
kisheria ili waweze kujibu tuhuma zinazowakabili,” alisema
Wakulyamba.
Tukio lilivyotokea
Akisimulia tukio hilo jana mmoja kati ya wanafunzi
wa chuo hicho, Elizabeth Thobias, alisema lilitokea saa tano usiku wakati
wakiwa mabwenini huku wengine wakijiandaa kwenda kujisomea na kulazimika
kutoroka ndani ya mabweni hayo kwa kupitia madirisha ya vyoo.
Elizabeth alisema majambazi hayo yalifika chuoni
hapo saa nne usiku na kuanza kuondoa vifaa vya kupoozea moto na kufunga milango
kwa nje jambo lililowapa wakati mgumu walipotaka kujiokoa.
“Majambazi hayo yalipofika chuoni kabla
ya kuanza kutekeleza ujambazi wao walisikika wakijadiliana kwa kuambiana
watuchinje kwanza au watuchome moto, mmoja kati yao alisikika akisema moto tu
unawatosha. Baada ya kuanza kuchoma moto ndipo tukaanza kukimbilia na kujiokoa
kupitia madirisha ya vyoo vya mabweni,” alisema
Elizabeth.
Tanga imekumbwa na matukio kadhaa katika siku za
nyuma likiwamo lililotokea Februari, mwaka huu baada ya vikosi vya polisi na
vile vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kupambana na majambazi
yaliyojificha katika Mapango ya Amboni na tukio jingine lilitokea Mei, mwaka
huu baada ya polisi kuwaua majambazi wanne walioweka kambi katika mapango hayo.
Pia wakazi wengine wanane wa jijini Tanga
walichinjwa na watu wasiojulikana katika tukio lililotokea Juni, mwaka huu
katika Kitongoji cha Kibatini kilichopo Kata ya Mzizima