WAPINZANI WAENDELEA KUWEKEZA PINI TANZANIA,CUF YAPIGWA STOP PEMBA,KISA NI MAGUFULI,SOMA HAPO KUJUA
Jeshi la Polisi Wilaya ya Chakechake, Pemba limezuia
kufanyika mkutano na vyombo vya habari wa Chama Cha Wananchi (CUF) uliokuwa
umepangwa kufanyika leo wilayani humo, kupisha ziara ya Rais John Magufuli
itakayoanza leo.
Rais Magufuli anatarajia kuanza leo ziara yake ya
kwanza visiwani humo tangu achaguliwe kuwa Mwenyekiti wa CCM.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya
Ikulu, Rais Magufuli atazulu Pemba leo na kesho atakuwa Unguja.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba, Shekhani
Mohamed Shekhani amesema kuwa zuio hilo la mkutano wa CUF ni kwa sababu eneo
wanalotarajia kutumia liko jirani na eneo la uwanja atakaokuwa akihutubia Rais
Magufuli
.
Hata hivyo, Katibu wa CUF wilaya ya Chake Chake,
Saleh Nassor Juma alilalamikia maamuzi hayo ya Jeshi la Polisi kwa madai kuwa
wao walitaka kufanya mkutano na vyombo vya habari na sio mkutano wa hadhara.
Alisema kuwa tayari walishawaeleza Idara ya Habari Maelezo na waliridhia.
Alisema mkutano huo na waandishi wa habari ulilenga
katika kutoa tamko lao kuunga mkono uamuzi uliochukuliwa na Baraza Kuu la chama
hicho kumsimamisha uanachama aliyekuwa Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba
pamoja na viongozi wengine 10.
“Niliwakatalia kwa hoja kwamba mkutano
na waandishi wa habari ni haki yetu ya kikatiba na tulikwishawataarifu watu wa
Idara ya Habari Maelezo juu ya kikao hicho halali ambacho wao pamoja na
waandishi wa habari walithibitisha kuwa watahudhuria,” alisema
Nassor.
Idara ya Habari Maelezo ilithibitisha kuwa
walikubali kufanyika kwa mkutano huo wa CUF na vyombo vya habari lakini baadae
walipokea taarifa ya kuahirisha kupisha ugeni wa Rais Magufuli.