UMOJA WA MATAIFA KUHUSU BIASHARA NA MAENDELEO (UNCTAD) YAZINDUA RIPOTI YA KIUCHUMI BARANI AFRIKA JIJINI DAR ES SALAAM LEO
Ofisa habari Umoja wa Mataifa Kitengo cha Mawasiliano (UNIC),Stellah Vuzo,akizungumza katika uzinduzi wa ripoti hiyo ya maendeleo ya kiuchumi barani afrika. Kushoto ni
Ofisa Uchumi wa Idara ya Afrika wa Nchi Zinazoendelea kutoka Geneva (Unctad), Claudia Roethlisberger.
Mtafiti wa Shirika linalojishughulisha na masuala ya utafiti wa masuala ya uchumi (REPOA),Stephen Mwombela,akichangia mada katika mkutano huo.
Wadau mbalimbali wa masuala ya uchumi nchini wakifuatilia kwa makini uzinduzi wa ripoti hiyo
NA ELISA SHUNDA,DAR
SERIKALI za Afrika zimeshauriwa kuchukua hatua ya
kuzuia ukuaji wa madeni ya mataifa yao ili kuepusha migogoro inayoweza kutokea kama
iliyowahi kutokea miaka ya mwishoni mwa 1980 na 1990.
Pia zimetakiwa kuongeza vyanzo vipya vya mapato
kwaajili ya kugharamia maendeleo ya nchi zao.
Kauli hiyo imetolewa jijini hapa jana na Ofisa
Uchumi Idara ya Afrika,Nchi zinazoendelea ambaye ni mwakilishi kutoka Geniva,
Claudia Reothlisberger, wakati alipokuwa akizindua Ripoti ya Maendeleo ya
Kiuchumi Barani Afrika.
“Ripoti hii ya UNCTAD inayozinduliwa leo(jana) inayohusu
Maendeleo ya Uchumi barani Afrika, lakini tufahamu imekuwa ikichapishwa kila
mwaka kuanzia mwaka 2000,lengo likiwa ni kuzisaidia nchi za Afrika kukabiliana
na hasara ya uwezekano wa ushirikiano mkubwa wa kiuchumi na uchumi wa dunia kwa
kufanya utafiti na uchambuzi sambamba na kujenga maridhiano na ushirikiano wa
kiufundi,
“Ripoti hii ambayo imezinduliwa chini ya Umoja wa
Mataifa kuhusu Biashara na Maendeleo (UNCTAD), inasisitiza kuwa kukopa inaweza
kuwa sehemu muhimu ya kuboresha maisha ya wananchi wa afrika lakini lazima
kupata uwiano kati ya wakati wa sasa, na baadaye kwa sababu madeni ni hatari
yanapokuwa sio endelevu” alisema.
Aidha alisema kwa mujibu wa ripoti hiyo ilibaini
kuwa angalau dola za kimarekani bilioni 600 zinahitajika kila mwaka ili kufikia
Malengo ya Maendeleo endelevu(SDGs) barani Afrika.
Alisema licha ya ripoti hiyo kubaini pia kwa sasa
nchi nyingi za afrika zimeanza kuondokana na utegemezi wa misaada rasmi ya
maendeleo kutokana na kutumia vyanzo vyake vipya vya fedha na vyenye ubunifu
lakini zinapaswa kuangalia vyanzo vya mapato vya nyongeza ambavyo vitasaidia
afrika kufikia malengo yake.
“Ripoti hii ambayo pia imepewa kichwa kidogo kuwa
Mienendo ya Madeni na Fedha za maendeleo barani afrika ilionyesha kuwa zipo
nchi kadhaa za Afrika zilikopa sana katika masoko ya ndani, na nchi hizo ni
Nigeria, Ghana, Kenya,Tanzania na Zambia” alisema.
Kwa upande wake Mchumi kutoka Benki ya Maendeleoa
ya Afrika(AfDB), Prosper Charles alisema kuwa ni wakati sasa serikali kuwa
macho na hatari za kukopa kutokana na masharti magumu yaliyopo katika kipindi
hiki.