KIKWETE ATOFAUTINA NA MAGUFULI,NI KUHUSU MIKUTANO YA KISIASA,SOMA HAPO KUJUA
Jakaya Kikwete, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) aliyemaliza muda wake alipokuwa katika kampeni mwaka 2010 |
JAKAYA Kikwete, Rais mstaafu wa awamu ya nne na
mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) aliyemaliza muda wake, amewataka
viongozi wa chama hicho kufanya mikutano ya hadhara kote nchini ili
kukiimarisha chama hicho, anaandika Regina Mkonde.
Kikwete ameyasema hayo leo
wakati akitoa hotuba yake katika mkutano maalumu wa chama hicho wa kumkabidhi
Rais John Magufuli uenyekiti wa chama hicho Taifa.
“Viongozi
wetu kutofanya mikutano kwa wananchi ndiyo sababu mambo yalianza kutuharibikia
huko nyuma na hatutaki iwe hivyo tena, naomba mwenyekiti ujaye wa chama,
usiache hii hali iendelee.” Amesema Kikwete huku akiongeza;
“Viongozi
wakienda kwenye mikutano ya hadhara hushangaa namna wananchi wanavyojitokeza
kwa wingi kuwasikiliza, kwa nini mnaogopa kwenda kwa wananchi, kama
tunawatafuta wanachama wapya hivi tutawapataje bila kwenda walipo?” amehoji
Kikwete.
Rais
mstaafu Kikwete pia amempongeza katibu mkuu wa chama hicho Kanali mstaafu
Abdurahman Kinana kwa kuendesha mikutano mingi ya hadhara ili kufufua uhai wa
CCM katika kipindi chote cha miaka mitatu kama katibu mkuu wa chama hicho.
“Nampongeza
Kinana kwani katika kipindi chake, amekuwa nguzo imara ameenda katika mikoa,
wilaya na majimbo yote hapa nchini kuzungumza na wananchi na alifika mpaka
maeneo ambayo viongozi wa chama huko hawakuwahi kufika. Amesema Kikwete.
Amesisitiza
kuwa viongozi wa chama hicho kutokwenda kwa wananchi na kufanya mikutano ni
miongoni mwa sababu za CCM kuyumba na kuwa na wakati mgumu wa kupata kura za
wananchi katika uchaguzi mkuu uliopita.
Kauli
hii ya Kikwete imekuja leo, ikiwa ni miezi michache tangu kutangazwa kwa
marufuku ya mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa ambayo ilitangazwa na Rais
Magufuli na kutiliwa mkazo na Jeshi la polisi hapa nchini.
Ni
marufuku hiyo ya mikutano ya hadhara ndiyo iliyosababisha Chama cha Demokrasia
na Maendeleo kupitia Naibu Katibu Mkuu wake (Bara) John Mnyika kufungua kesi
mwanzoni mwa juma hili katika mahakama ya haki ya Afrika Mashariki kupinga zuio
hilo la serikali.
Wito
wa Rais mstaafu Kikwete kumtaka Rais Magufuli kuendeleza utamaduni wa viongozi
wa CCM kufanya mikutano ya hadhara imetafsiriwa kama ukosoaji wa wazi dhidi ya
marufuku ya serikali na Jeshi la Polisi juu ya mikutano hiyo hapa nchini