TAMKO FEKI LA MADIWANI LAMCHANGANYA "CHAPOMBE" KITWANGA,SOMA HAPO KUJUA
SIKU chache baada ya
kundi lililojiita Madiwani wa Jimbo la Misungwi kutoa tamko la kumtetea Charles
Kitwanga, tamko hilo limeelezwa kuwa feki, anaandika Antony
Sollo.
Tamko hilo lilitolewa kupinga hatua ya Rais
John Magufuli kutengua uteuzi wa Kitwanga, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani
ya Nchi. Uamuzi huo ulifanywa tarehe 20 Mei mwaka huu.
Antony Bahebe,
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi amesema kuwa, madiwani
waliojitokeza kumtetea Kitwanga ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Misungwi, halina
baraka za madiwani wa halmashauri hiyo kwa kuwa, hawajawahi kukutana katika
kikao chochote na kuazimia kutoa tamko hilo.
Kundi hilo la madiwani
‘feki’ lilitoa tamko rasmi kwa vyombo vya habari likimtetea Kitwanga ambaye
alidaiwa kuingia bungeni na kujibu maswali yaliyohusu wizara yake akiwa
amelewa.
Katika tamko lao,
kundi hilo la madiwani ‘feki’ lilieleza kushangazwa na kutoridhishwa kwao na
uamuzi wa Rais Magufuli wa kumvua uwaziri Kitwanga kwa kile kilichodaiwa na
kundi hilo kuwa, hakukuwa na uthibitisho wa kitabibu kuhusu tuhuma za ulevi
wake (Kitwanga).
Madiwani hao ‘feki’
walidai, walikuwa nyumbani kwa Kitwanga mkoani Dodoma baada ya kupewa mwaliko
na mbunge wao.
“Tulitoka na kuelekea
katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kwa lengo la kututembeza maeneo yote ya
Dodoma, lakini ilifika jioni wakati tukirejea nyumbani tukiwa naye, ghafla
tukaona habari zikisambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa Waziri Kitwanga
amevuliwa uongozi kwa kuwa, alionekana akiwa amelewa,” ilieleza sahemu ya
taarifa yao.
Kundi hilo lilidai
kuwapo kwa kundi la wafanyabiashara wa dawa za kulevya, mafisadi wakiwemo
maadui wa Kitwanga na makundi ndani ya CCM kuwa ndio waliotoa taarifa za uongo
kwa Rais Magufuli na Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu kwa maslahi yao binafsi.
Hata hivyo mwenyekiti
wa halmashauri hiyo (Bahebe) ameueleza mtandao huu, “ni kwamba sisi madiwani wa
Misungwi hatujafanya kikao cha aina yoyote ikiwemo kutoa tamko la kupinga
kutenguliwa kwa mbunge wetu katika nafasi ya Waziri wa Mambo ya Ndani.
“Tunaamini Magufuli
ndiye aliyemteua na ndiye aliyetengua uteuzi huo. Je, sisi tuna nguvu gani ya
kupinga maamuzi ya mkuu wa nchi?” amesema mwenyekiti huyo.
Mtandao huu umemtafuta
Kitwanga ili kuzungumzia tuhuma za kuunda kundi la madiwani kwa ajili ya
kumsafisha katika jamii.
“Naombeni jamani
mniache mimi nimechoka na maneno! Watu wameongea mengi, mimi sitaki maneno
sijui chochote niacheni nipumzike,” amesema Kitwanga.
Mmoja wa wanachama wa
Chama cha Mapinduzi (CCM) ambaye hakupenda kuandikwa jina lake liandikwe
ameeleza kushangazwa na nguvu ya kundi hilo la madiwani kulitaka Bunge
na Serikali kutoa ushahidi wa kikemia unaoonesha ulevi wa Kitwanga.
“Hivi hawa watu
waliojitwisha uwakilishi wa wana Misungwi wamepata wapi mamlaka ya kupingana na
rais ambaye ndiye alimteua bila ushawishi?
“Leo hii amemvua
uteule alalamikiwe na kundi dogo kama hilo? Mawaziri wangapi walishatenguliwa
mbona hatukuona kundi likijibatiza kuwa ni Madiwani?”
Hakuna maoni
Chapisha Maoni