KAMPUNI YA MAFIA BOXING PROMOTION YAWAPIMISHA UZITO MABONDIA NA KUGAWA MITUNGI YA GESI KWA MAMA LISHE
Na Mussa Augustine
Pambano la tatu la Kimataifa la Knockout ya Mama limeanza rasmi kwa zoezi la kupima uzito na face-off kwa mabondia wanaotarajiwa kushuka ulingoni kesho, Februari 28, 2025, katika mapambano ya raundi sita na nane katika ukumbi wa Magomeni Sokoni Jijini Dar es Salaam
Katika tukio hilo lililofanyika Magomeni Sokoni, Mafia Boxing Promotion pia wametoa mitungi ya gesi kwa wanawake wajasiriamali ili kuwawezesha kuachana na matumizi ya nishati chafu na kuhamasisha matumizi ya Nishati safi ikiwa ni kuunga mkono agenda ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha Watanzania wanatumia Nishati safi na salama.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo Mkurugenzi wa Mafia Boxing Promotion Ally Zayumba amesema kuwa Dkt Samia Suluhu Hassan ameupa heshima mchezo wa Masumbwi kama ilivyo kwenye Michezo mingine ikiwemo mpira wa miguu,hivyo Kampuni ya Mafia Boxing Promotion imekua ikimuunga mkono katika jitihada zake ikiwemo masuala ya kusaidia wakinamama kuachana na matumizi ya Nishati chafu( kuni na mkaa) nakutumia Nishati safi ikiwemo gesi ya kupikia.
"Hatua hii ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuhakikisha Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia kama gesi na umeme badala ya kuni na mkaa."amesema Zayumba
Baadhi ya wanawake waliopokea mitungi hiyo akiwemo Amina Mtama,Anna Showo,Shufa Brasti,na Zubeda Idd kwa nyakati tofauti wameishukuru Kampuni ya Mafia Boxing Promotion kwa kuona umuhimu wa kusaidia jamii na kuunga mkono Sera ya Serikali ya awamu ya sita kuhusu agenda ya nishati safi ya kupikia.
Pia wajasiliamali hao wameishukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wa shupavu nakuahidi kuwa wapo pamoja nae nakwamba watahakikisha wanampa ushindi mnono katika uchaguzi mkuu unaofanyika mwezi Oktoba Mwaka huu.
Katika zoezi la kupima uzito,bondia mstaafu Rashid Matumla ambaye ni baba wa Amiri Matumla, anaepigana kwenye main card hapo kesho, amesema kuwa mtoto wake amejiandaa vizuri na ana nidhamu ya hali ya juu ndani na nje ya ulingo,hivyo anamatumaini makubwa ya kushinda pambano hilo.
Kwa upande wake, Amiri Matumla ameahidi kushinda kibabe dhidi ya mpinzani wake, Paul Amavila kutoka Namibia, huku Amavila akijigamba kuwa Matumla bado ni mdogo kwake na hana nafasi ya kushinda pambano hilo.
Naye Promota mkongwe wa Masumbwi J. Msangi, ameipongeza Kampuni ya Mafia Boxing Promotion kwa jitihada zake za kuendeleza na kikuza mchezo wa ngumi,nakubainisha kuwa Kampuni yake ilifungua njia na sasa Mafia Boxing wanaendeleza kwa kiwango cha juu, huku akitabiri Tanzania kupaa zaidi kimataifa katika masumbwi.
Pambano hili la Knockout ya Mama litakuwa na mapambano kumi na nne (14) ya kusisimua, yakihusisha mabondia wa ndani na nje ya nchi hivyo mashabiki wa mchezo wa ngumi wanatarajiwa kufurika kwenye pambano hilo ili kushuhudia.
Vingilio katika pambano hilo ni 50000, 20000 na 10000.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni