SHEIKH JALALA: "WANAOUA ALBINO KWA KIGEZO CHA UTAJIRI NI USHAMBA"
Sehemu ya walemavu wa ngozi waliohudhuria Iftari katika msikiti wa Al Ghadir Kigogo, wakifuatilia kwa makini hutba iliyotolewa na Kiongozi Mkuu wa dhehebu la Shia Ithnasheria Sheikh Hemed Jalala. |
Kiongozi Mkuu wa Waislamu
dhehebu la shia Ithnasheria amewataka jamii kufahamu kuwa hakuna njia ya mkato
ya kupata utajiri na kwamba wale wote ambao wanaamini katika kuua watu wenye
ulemavu wa ngozi ili wanufaike wanapaswa kuacha tabia hiyo kwani ni kwenda
kinyume na mufundisho ya dini zote duniani.
Akizungumza katika iftari maalum
na watu wenye ulemavu wa ngozi kutoka Wilaya ya Kinondoni, Sheikh Jalala amesema
viongozi wa dini na Watanzania kwa ujumla wanapaswa kulizungumza hilo bila woga
kwani hiyo ndiyo njia pekee ya kuwasaidia watu wenye ulemavu wa ngozi.
Amesema Albino ni binadamu kama
walivyo watu wengine hapa nchini, wanahaki sawa ya kuishi, kulindwa na
nyinginezo hivyo si haki kukatiza maisha ya watu hao na kwamba dini zote za
duniani haziruhusu watu kuuana.
Aidha sheikh Jalala amefafanua
njia nzuri za kupata utajiri kuwa ni kufanya kazi kwa bidii zote na si kuwaza
Imaani potofu ya kuua watu wengine ambao hawana hatia.
Amesema kitendo cha kuua kinazima
ndoto zao, hivyo ni wakati watu wakafahamu hilo na kuachana na tabia hiyo
ambayo inatia doa Taifa la Tanzania huko Ulimwenguni.
“Nataka niseme, tendo la kuwaita
wenzetu wenye ulemavu wa ngozi na kushiriki pamoja futari ya jioni hii ni
kuonyesha kuwa hawa ni wenzetu, hawana utofauti wowote na wengine, wanahaki
sawa kama Watanzania…kuwaua ni matendo ya kishetani na hayakubariki” alisema
Sheikh Jalala
Amesema wale wote ambao bado
wana Imaani ya kuua ili watajirike ni washamba na hawajui walifanyalo, wanapaswa
kufahamu kuwa utajiri hauletwi kwa damu za watu badala yake ni kujituma kwa
kufanya kazi inayompendeza Mungu.
Katika hatua nyingine Sheikh
Jalala amewaahidi chama cha watu wenye ulemavu wa Ngozi Wilaya ya Kinondoni kuwapa
ushirikiano wowote watakaouhitaji na kwamba wanakaribishwa katika msikiti wa
Kigogo muda wowote na watapewa
ushirikiano unaostahili.
“Nataka niwaambie ndugu zangu
wenye ulemavu wa ngozi hapa Tanzania sisi hapa Kigogo tunawapenda na
tunawakaribisha hapa msikitini ,sisi hatujui kubaguana,muone kama mko nyumbani
na kwamba muda wowote mkiwa na haja ya kutuona milango iko wazi na
mnakaribishwa sana ”Alisema Sheikh Jalala.
Akizungumzia Msikiti wa Kigogo
Sheikh Jalala amesema ni kimbilio la watu wote, ni msikiti wa wakristo, watu
wenye ulemavu wa ngozi, wajane na masikini. Ni msikiti ambao unajari imaani za
watu tofauti kwani wanaamini kuwa haitokea siku moja nchi yote ya Tanzania
kukawa na dini moja hivyo si wakati wa kubaguwana.
Haitakaa itokee Tanzania kukawa
na dini moja mpaka dunia inapogota mwisho wake…lakini mtakubaliana na mimi kuwa
Mungu aliyeumba Mkiristu ndiyo huyo aliyemuumba muislamu na wale wa Dini
nyingine, Mwanzo wa binadamu ni uleule wa Adamu na hawa…tofauti zilizopo ni za
kibinadamu hatuna haja ya kubaguana.Alisema.
Ametoa wito kwa Watanzania
kupinga mauaji ya Albino kwa vitendo na kuwataka viongozi wa dini kutumia
membari zao kukemea viitendo viovu vya mauaji ya albino.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni