MAJIPU YATAONDOKA NA CCM YENYEWE,SOMA HAPO KUJUA
WIKI iliyopita, Rais John Magufuli aliitisha mkutano
wa ghafla kukutana na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ngazi ya mikoa na
wilaya zote nchini, anaandika Ansbert Ngurumo.
Mwaliko huo ulikuwa wa ghafla
na uliambatana na sharti moja kuu la viongozi hao kutofika Dar es Salaam wakiwa
wamevaa sare za chama.
Gharama
za safari zililipwa na Ikulu na makada hao waliondoka wakifurahia jinsi Ikulu
ilivyowakarimu kwa chakula safi, kingi na cha kusaza!
Mkutano
huo ulifanyika Ikulu na ilionekana wazi kuwa, waandaaji walikuwa ni maofisa wa
Ikulu. Abdulrahmani Kinana, Katibu Mkuu na vijana wake wa makao makuu, hawakuwa
na raha.
Walionekana
wazi kuchoka na kusubiri mkutano huo uishe ili waendelee na shughuli zake
nyingine.
Baada
ya kufika katika ukumbi wa mkutano huo, hata itifaki za kawaida za mikutano ya
ndani ya CCM zilikuwa hazieleweki, jambo lililomfanya Kinana kusimama mara
kadhaa kurekebisha hapa na pale ili mambo yaende.
Kinana
alikuwa na ujumbe mmoja kwa washiriki – kwamba mwezi Juni mwaka huu, Rais
Magufuli atakabidhiwa chama kama mwenyekiti.
Kabla
ya mkutano huo, nje ya ukumbi wa mikutano Ikulu na kwenye hoteli walikofikia
makada, gumzo kuu lilikuwa ni kama CCM itakuwa salama chini ya Magufuli.
Wapo
waliojidanganya kuwa Jakaya Kikwete, mwenyekiti wa sasa, hawezi kukabidhi chama
mpaka 2017. Mashabiki hao wa Jakaya walisema Rais Magufuli aachwe aendelee na
kazi ya kutumbua majipu serikalini, chama kibaki na Jakaya, ili kibaki salama.
Pale
ukumbini, baada ya Kinana kutangaza kuwa Rais Magufuli atakabidhiwa chama mwezi
Juni, kundi dogo la makada mashabiki wa Magufuli walishangilia, huku
wakijishtukia wenyewe kwa wenyewe.
Walio
wengi hawakuona sababau ya kushangilia kwa sababu kwanza ni utaratibu wa
kawaida kufanya hivyo, na pili, kushangilia ni sawa na kusema wamechoka na
uongozi wa Jakaya.
Baada
ya mgongano ya kiitifaki, Rais Magufuli alipata nafasi ya kuwahutubia. Kwa
kusudi la makala hii nitataja machache ya aliyozungumzia.
Kwanza,
alisema amewaita viongozi hao kuwashukuru kwa kumpigania hadi akachaguliwa kuwa
rais. Alikiri kuwa bila wao, asingekuwa hapo alipo. Pili, aliwaeleza kuwa
amewaita kuwahakikishia kuwa nchi iko salama na chama kitakuwa salama.
Tatu,
alisema amewaita kuwahakikishia wale wenye mashaka na kasi yake ya utumbuaji
majipu, na walioanza kupinga hatua hizo waache kumkatisha tamaa. Akatumia muda
mrefu kueleza baadhi ya hisia zinazoenezwa kuwa anakiuka haki za binadamu, kuwa
mizigo bandarini imepungua, na kuwa atadhalilisha CCM.
Mpaka
hapa kuna mambo mawili makuu ya kutazamwa kwa umakini. Kwanza, Rais Magufuli
alifanya kampeini kwa kusisitiza, “Tanzania ya Magufuli” itafanya hili na lile.
Alikuwa mwangalifu sana kutotanguliza CCM mbele ya umma uliokuwa umekata tamaa
na CCM.
Hata
baada ya kuapishwa, mara mbili ametofautiana na Kikwete katika vikao vya kamati
kuu. Mara ya mwisho walitofautiana kuhusu suala la uchaguzi wa Meya wa Jiji la
DSM.
Katika
kikao hicho, baadhi ya wajumbe wa kamati kuu walilalamika kuwa kuna mawaziri na
watumishi wa serikali wanashabikia uchaguzi ufanyike na meya atoke Ukawa (Umoja
wa Katiba ya Wananchi).
Kikwete
aliunga mkono na kutaka hatua zichukuliwe dhidi ya wote walio serikalini na
wanashibikia jiji liende Ukawa. Kabla ya kuhitimisha ajenda hiyo, Rais Magufuli
akaomba kuzungumza.
Katika
mchango wake, akakiri kuwa wapo wanaounga mkono na yeye ni mmoja wao. Akasema
kama ni kosa lilifanyika pale CCM iliporuhusu uasi ndani yake na kusababisha
mkoa wa Dar es Salaam uwe na madiwani wengi wa Ukawa.
Akakumbusha
kuwa hata yeye wakati wa kampeni alifika mahali akaacha kwenda kwenye vikao vya
usiku vya kufanya tathmini ya kampeini kwa sababu ya fitina na uasi.
Akasisitiza
kuwa kama CCM haitaacha majungu, yeye hatakuwa tayari kuitetea. Akahitimisha
kwa kusema, ni vizuri “tuwaache Ukawa watutawale Dar es Salaam ili tuonje
uchungu wa kutawaliwa kwa sababu ya uasi wetu”.
Baada
ya mchango wa Magufuli, Jakaya Kikwete aliahirisha kikao kwenda kunywa chai.
Mgongano huu wa Kikwete na Magufuli hauwezi kuiacha CCM ikawa salama.
Hii
ni kwa sababu huwezi kusifia hatua anazochukua Magufuli bila kulaani uongozi wa
Jakaya. Mpaka sasa Magufuli hajaanzisha jambo jipya serikalini, bali
anachofanya ni kukosoa utendaji wa Rais Kikwete.
Kwa
hiyo, tangazo kwamba Magufuli atakabidhiwa CCM mwezi Juni si tangazo la heri
kwa CCM ya Kikwete. Ni tangazo la kutumbua majipu ndani ya CCM yakiwamo yale
yaliyomwezesha Magufuli kuingia madarakani.
Hata
kama Magufuli anatamba hadharani kuwa hakuna mfanyabiashara yeyote
aliyemchangia hata senti moja, lakini CCM na vyombo vyake vilifanya madudu
makubwa kumwezesha Magufuli “kushinda” urais.
Matajiri
walichangia CCM iliyokuwa inamnadi yeye. Je, yuko tayari kufumua hata jipu
hilo?
Jambo
la pili ni ukweli kuwa majipu anayoyatumbua Magufuli si ya wapinzani bali
watendaji wa serikali ya CCM. Kwa hiyo, majipu yanayotumbuliwa ni matawi
lakini. Mashina ya majipu ni CCM.
Je,
uking’oa shina mti utapona? Huu ndiyo wasiwasi unaoikumba CCM ikiwa mikononi
mwa Magufuli. Kwa hiyo, wana CCM wanaoijua CCM wanajua kuwa CCM haitakuwa
salama, ingawa yeye aliwahakikishia kuwa itakuwa salama.
Kwanini
alilazimika kuwahakikishia usalama? Magufuli anaishi kwenye nadharia kuwa
mafisadi ndani ya serikali na ndani ya chama, hawakutumwa na chama kufanya
uchafu.
Magufuli
anaishi katika njozi kuwa anaweza kutumbua majipu yaliyo katika sehemu nyeti –
tena bila ganzi – halafu mgonjwa akabaki kuchekelea na kushangilia.
Wenye
hekima na wazee wa chama wanajua majipu mengine yameumbwa ndani ya CCM, na
ndiyo yanashikilia uhai wa CCM. Ukiyatumbua, umeitumbua CCM. Hata kwa hekima
ipi, hayatumbuliki. Na yakitumbulika, yanaondoka na CCM.
Ufisadi
wa mabilioni na mikataba feki ndiyo imeifikisha CCM na serikali yake hapa
ilipo. Hata kwa kitendo cha Magufuli kuita makada wa CCM kwa kutumia fedha ya
serikali wakati akidai kubana matumizi, tayari ametengeneza kipere
kitakachogeuka jipu.
Uzoefu
pale Ikulu na Lumumba – makao makuu ya CCM – ni kuwa mikutano ya namna hiyo
hutumia mara tatu ya gharama halisi.
Hiyo
ndiyo CCM atakayokabidhiwa Magufuli mwezi Juni. Magufuli hajui CCM. Kama
angeijua, asingeikaribisha Ikulu kwa ajili tu ya kuihakikishia kuwa itakuwa
salama yake.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni