Zinazobamba

TRA YAZIDI KAMATA WAKWEPA KODI,YAWAKAMATA WAFANYABIASHARA 84 KWA MAKOSA YA EFDS,SOMA HAPO KUJUA


Pichani ni Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo, Alphayo Kidata (Picha na Maktaba)


Jumla wa wafanyabiashara kumi kati ya 84 waliokamatwa katika zoezi maalum la ukaguzi wa matumizi ya mashine za kielektroniki za kodi katika Mkoa wa Dar es Salaam wamepatikana na hatia na kuhukumiwa kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini ambapo wote wamelipa faini na serikali kukusanya jumla ya shilingi 31,500,000.

Wafanyabiashara hao walikamatwa kati ya Januari na February 2016 katika maeneo ya Kariakoo jijini Dar es Salaam kwa makosa mbalimbali ya kukiuka sheria za kodi hususan kuuza bidhaa bila kutoa risiti za kodi na kufanya udanganyifu katika thamani ya bidhaa kwenye risiti za kodi na hivyo kuikosesha serikali mapato.

Mbele ya mahakimu mbalimbali wa mahakama ya Hakimu Mkazi Ilala na kwa nyakati tofauti, wafanyabiashara waliohukumiwa walikiri makosa yote waliyosomewa na kuepuka kifungo cha jela baada ya kulipa faini.

Wakati huo huo TRA imekusanya jumla ya shilingi 27,000,000 kutoka kwa wafanyabiashara 12 kati ya 15 ambao walilipa faini ya shilingi 2,250,000 kila mmoja baada ya kupatika na makosa mbalimbali ya ukwepaji kodi na hivyo kutozwa faini na hatimaye kuepuka kufikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.

Kesi za wafanyabaishara wengine 16 bado zinafanyiwa kazi ili kuweza kubaini makosa yao na kuwatoza faini na kama watakaidi kulipa faini basi watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.

Mamlaka ya Mapato Tanzania  kwa mujibu wa sheria inayoitaka kufanya ukaguzi kwa wafanyabiashara, inaendesha zoezi la ukaguzi kwa wafanyabiashara wa Mikoa yote nchini ili kukakugua taarifa za wafanyabiashara hao, kuhakiki utunzaji wa kumukumbu za biashara na kukagua matumizi ya mashine za Kielektroniki za kodi (EFDs) ili kutambua kama mfanyabiashara ana mashine na anaitumia pamoja na kufahamu changamoto mbalimbali za biashara.

Katika ukaguzi huo jumla ya wafanyabiashara 84 katika Mkoa wa Dar es Salaam walikamatwa ambapo 34 walipatikana wana kesi za kujibu mahakamani na, 15 walipatikana na hatia na kwa mujibu wa sheria za kodi walitozwa faini na TRA na kuepuka kufikishwa mahakamani.

Zoezi la ukaguzi wa taarifa za wafanyabiashara ni endelevu na litafanyika katika mikoa yote nchini ili kuendelea kuhimiza matumizi ya mashine za kielektroniki ambazo baadhi ya wafanyabiashara wanakwepa kuzitumia na hivyo kuikosesha serikali mapato.

Ili kufanikisha zoezi hili wananchi wanashauriwa kudai risiti za kielektroniki za kodi kila wanapofanya manunuzi. Endapo muuzaji atashindwa kutoa risiti basi watoe taarifa katika ofisi yoyote iliyokaribu kwa hatua zaidi.

Endapo kila mwananchi atadai risiti yenye dhamani halisi ya bidhaa aliyonunua basi wafanyabiashara hawatakuwa na njia ya kukwepa kutoa risiti na hivyo kodi stahiki kuingia katika mfuko wa serikali.


Imetolewa na:
Idara ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi
TRA-Makao Makuu

Hakuna maoni