CHAMA CHA WAKUNGA TANZANIA (TAMA) CHAWAFUNDA WANAHABARI
Chama cha Wakunga Tanzania (Tanzania Midwives Association-TAMA) imefanya mkutano maalum wa kuhamasisha waandishi wa Habari kuhusu kazi za wakunga katika kuelekea siku ya Wakunga Duniani inayotarajiwa kufanyika Mei 5 mwaka huu.
Katika mkutano huo uliofanyika jana Aprili 28, TAMA ilibainisha kuwa, wanahabari wengi wamekuwa wakichanganya habari za wakunga wataalam ambao wapo chini ya Chama hicho na wale wakunga wa jadi ambao hawana taalum pamoja na kiapo cha kufanya kazi hiyo kitu ambacho kinaleta usumbufu mkubwa kwa jamii.
Mratibu wa TAMA, Bi. Martha Rimoy katika mkutano huo, ameeleza kuwa, shughuli za Wakunga wataalam ni wale tu ambao wamesomea taaluma hiyo pamoja na kula kiapo katika kumsaidia Mama na Mtoto na na huyo ndiyo anaitwa Mkunga na si wale ambao hawajapata mafunzo wala kula kiapo.
Aidha, aliomba wanahabari na vyombo vya habari kuzipatia nafasi/Kipaumbele habari za Wakunga kwani zitaondoa woga kwa jamii iliyojenga Imani potofu kwa wakunga.
“Jamii imekuwa ikijenga Imani potofu namna ya Wakunga buka kujua mkunga huyo ni yupi. Tunaomba ifahamike Mkunga ni yule aliyepata mafunzo yake kitaalam na pia kula kiapo pamoja na kusajiliwa na taasisi husika kama ilivyo taratibu za Nchi.
Tuondoe Imani zingine kwa Wakunga pia tunawaomba wanahabari kuweza kutoa elimu ya kutosha kuhusiana na mambo ya Wakunga hasa wakunga wataalam ambao wamepatiwa mafunzo yote ya kuhakikisha wanamuokoa Mama na mtoto wakati wa uzazi” alieleza Bi. Martha Rimoy.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa TAMA, Dkt Sebalda Reshabari ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mkutano huo, ameeleza kuwa, Wakunga wataalam wanao wajibu wa kumsaidia Mwanamke na mtoto katika kukabiliana na vifo vitokanavyo na Masuala ya Uzazi vinavyozidi kuwatesa akina mama wengi, hasa inapokuja wakati wa tendo la kujifungua.
Aidha, Dkt. Sebalda amebainisha kuwa, pamoja na Changamoto mbalimbali, vifo vya watoto walio chini ya umri wa miaka 5, imepungua kwa asilimia 81, huku akitaka muendelezo wa elimu utolewe kwa Jamii.
Kwa upande wake, Afisa Mipango wa Afya ya Mama na Uzazi wa Shirika la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA)nchini, Bi. Felista Bwana ameelezea kuwa, upo umuhimu wa Mkunga mtalaam katika kuokoa Uhai wa Mama na mtoto kwani bila wao Dunia ingekuwa kwenye matatizo makubwa.
Siku ya Ukunga Duniani Inatarajiwa kuadhimishwa katika Viwanja vya Mnazi mmoja Jijini Dar es Salaam, Mei 5 mwaka huu huku ikibeba ujumbe wa kauli mbinu ya “Wanawake na Watoto wachanga ni muhimili wa Ukunga”.
Aidha, mkutano huo ulieza changamoto wanazokabiliana nazo wakunga ni nyingi hivyo wameiomba Serikali kuangalia namna ya kukabiliana nayo ili kila Mkunga kufanya kazi yake kwa uhuru na haki kwa dhama za sasa huku wakiomba jamii kuondoa dhana potofu dhidi yao pindi wawaonapo katika vituo vya Afya, Zahanati na Hospitali zote.
Mkutano huo maalum wa TAMA, ulihusisha wanahabari mbalimbali kutoka katika vyombo vya Habari nchini ikiemo, Magazeti, Radio, Televisheni na magazeti ya mtandaoni.
Afisa Mipango wa UNFPA, hapa nchini, Bi.Felista Bwana akitoa maelezo mafupi juu ya wakunga hapa nchini
Hakuna maoni
Chapisha Maoni