Zinazobamba

MAMBO YAANZA KUHARIBIKA ZANZIBAR,OFISI ZA CUF ZACHOMWA MOTO HOVYO HIVYO,SOMA HAPO KUJUA


Moja ya ofisi za CUF, Zanzibar baada ya kuteketea na moto

Moja ya ofisi za CUF, Zanzibar baada ya kuteketea na moto



MAMBO yameanza kwenda mrama visiwani Zanzibar baada ya Ofisi za Chama cha Wananchi (CUF) kuchomwa moto jana, anaandika Mwandishi Wetu.

Wakati wananchi wakisubiri kuona hatma ya mgomo wa Chama cha Wananchi (CUF) na vyama vingine tisa dhidi ya uchaguzi wa marudio uliotangazwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) tarehe 20 Machi mwaka huu; chuki, visasi na hali ya hatari vyaanza kudhihiri.

Ikiwa ni matokeo ya chuki za muda mrefu baada ya maridhiano kufikiwa miaka zaidi ya sita iliyopita, ofisi tano za CUF Pemba na Unguja tayari zimeteketea.

“Si haya tu, mengine mengi yanaweza kutokea. Waliambiwa wakapuuza na sasa hii ni ishara tosha kwamba tuendako mambo ni magumu,” anasema Bakari Maalim Salum wa Michenzani Zanzibar.

Uchomaji ofisi hizo umefanyika siku moja baada ya Maalim Seif 
Sharif Hamad, Katibu Mkuu wa CUF kuwasili visiwani humo akitokea India kwenye matibabu.

Maalim Seif ambaye alikuwa mgombea urais kupitia CUF visiwani humo, alililaumu Jeshi la Polisi kwa kushindwa kukabiliana na vitendo viovu vinavyofanywa na wale wanaoitwa mazombi.

Tukio la uchomaji moto ofisi za CUF limetanguliwa na uchomaji moto wa maskani ya CCM ya Sauti ya Kisonge, Unguja.

Hata hivyo, zipo taarifa zinazoeleza kwamba ni wanaofanywa hivyo ni kundi moja lenye mrengo wa kisiasa ambalo limekuwa likivuruga upande wake na kudai kulipiza kisasa upande wa pili.

Matawi ya CUF yaliyochomwa moto ni Kilimahewa,  mjini Unguja Wilaya ya Magharibi, Mkanyageni, Kiwapwa, Kiuyu Minungwini, Wingwi na Kinowe yote ya Kisiwani Pemba.

Wachambuzi wa kidiplomasia, wananchi, wanasiasa na kada zingine zimeeleza kwamba, hatua ya serikali kukalia kimya mgogoro wa kisiasa Zanzibar utaibua mengi.
 
Zanzibar imekuwa kwenye mkwamo na chuki za kisiasa kwa muda mrefu. Hata hivyo, Serikali Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaonekana kusuasua kutatua mgogoro huo kisiasa hususani kati ya CUF na CCM.
Habari hii kwahisani ya Mwanahalisi oline

Hakuna maoni