WATANZANIA HAWA KUPANDISHWA ICC,NI BAADA YA UCHAGUZI MKUU,SOMA HAPO
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Tanzania, Bahame Nyanduga (katikati) akizundua Ilani ya Uchaguzi. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendani wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Hellen Bisimba. Kulia ni Mratibu wa Mtandao wa Watetea Haki za Binadamu, Onesmo Ngurumwa
MTU yeyote, awe mpigakura, mwanasiasa mgombea kura na wapambe
wake au mwandishi wa habari, atakayebainika kupanga vurugu na kuvunja sheria
hivyo kuwa chanzo cha ghasia wakati na baada ya uchaguzi, atastahili
kushitakiwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC).Anaandika Pendo
Omary … (endelea).
Tamko hilo limetolewa na Mwenyekiti wa
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Tanzania, Bahame Nyanduga katika
hotuba ya uzinduzi wa Ilani ya Uchaguzi ya asasi za kiraia (AZAKI) kwenye
ukumbi wa Millenium Tower, Kijitonyama, Dar es Salaam.
Nyanduga ambaye ni mwanasheria amesema
kupanga vurugu na kuvunja sheria ni mambo yanayochochea uvunjaji wa haki za
binadamu, msingi hasa wa mashitaka mbele ya mahakama hiyo ambayo Tanzania
imesaini mkataba wa kuanzishwa kwake.
AZAKI zimeandaa Ilani mahsusi ambayo
ni muongozo kwa vyama vya siasa na wagombea katika kuomba ridhaa ya kuongoza
taifa.
Nyanduga amesema tayari kuna
viashiria vya uvunjifu wa amani ikiwemo kuwepo vikundi vya ulinzi vya vyama vya
siasa kinyume na Katiba.
Ametaja viashiria vingine kuwa ni
kauli zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa ambazo zinaelekeza kutokea kwa
matendo yaliyo kinyume cha sheria na taratibu wakati wa uchaguzi.
Baadhi ya kauli ametaja ile
iliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape
Nnauye, ya kwamba chama chao kitapata ushindi ikibidi hata kwa “goli la mkono.”
Kauli nyingine ni “tukiibiwa kura
patachimbika,” “ushindi ni lazima,” “serikali haitolewi kwa vikaratasi,”
“tutapata ushindi wa tsunami” na “ushindi saa nne asubuhi.”
“Tunashuhudia matukio ya matumizi ya
lugha zisizo na staha katika kampeni zinazoendelea nchini. Tume inawakumbusha
wanasiasa na wafuasi wao kuzingatia maadili ili kudumisha siasa safi, amani na
utulivu wa nchi.”
Amesema kwa kuwa Tanzania ni
mwanachama wa Mkataba wa Roma ulioanzisha ICC kupitia mwamvuli wa Umoja wa
Mataifa, ieleweke vema kwamba yakitokea makosa yanayotajwa na mkataba huo
wakati au baada ya uchaguzi mkuu Tanzania, watakaothibitika kuyatenda, ndio
watakaoshikwa na kushitakiwa katika mahakama hiyo kwa makosa ya uchochezi au
kupanga njama hizo.
“Kwa nafasi yangu kama
mwanasheria niliyehusika katika kesi inayohusu mauaji ya halaiki ya nchini
Rwanda katika Mahakama ya Mauaji ya Kimbari nchini Rwanda (ICTR) jijini Arusha,
na nimekuwa mdau wa masuala ya ICC, napenda kutoa indhari kwamba viongozi wote
watakaochochea vurugu, wawe ndani au nje ya serikali, raia wa kawaida au
waandishi wa habari, watachukuliwa hatua.
“Wale watakaodhihirika kutumia
lugha za uchochezi ama kushiriki kupanga vurugu na uvunjifu wa haki za
binadamu, kwa kiwango ambacho kitailazimu ICC kuchunguza makosa hayo hapa
Tanzania, waweza kufikishwa mbele ya mahakama ya ICC,” amesema Nyanduga.
Katika kuhakikisha haki
inatendeka wakati wa uchaguzi mkuu, Nyanduga amehimiza Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kuhakikisha taratibu za
uchaguzi zinaendeshwa kwa uwazi, haki, kwa misingi ya sheria na pia wasimamizi
wa uchaguzi wasijaribu kuingiza ushabiki wala hi sia binafsi.
Habari hii
kwa hisani ya Mwanahalisi oline
Hakuna maoni
Chapisha Maoni