KUFUKUZWA CHADEMA KWAMTESA ZITTO,SASA ASINGIZIA MAFISADI WA ESCROW SOMA HAPA KUJUA
Takribani miezi
mitatu na ushei tangu sakata la uchotwaji wa fedha zaidi ya Sh. bilioni 200
katika akaunti ya Tegeta Escrow kutikisa nchi huku mawaziri wawili na
mwanasheria mkuu wa serikali wakiondoka madarakani na katibu mkuu mmoja
akichunguzwa, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto
Kabwe, amefichua kuwa wajumbe wote wa kamati hiyo wataadhibiwa vibaya kwenye
majimbo yao kama njia ya kulipiza kisasi kutokana na kuwaumbua wote
walionufaika na fedha hizo.
Katika
mahojiano na kituo cha ITV kwenye kipindi cha Dakika 45, kilichorushwa jana
usiku, Zitto amesema kuwa wakati PAC wakiendelea kuchambua ripoti ya Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) juu ya Escrow, mjumbe mmoja wa
kamati hiyo aliitwa na ‘wakubwa’na kuelezwa kwamba akifika bungeni awageuke
wenzake na aseme kuwa mgogoro wa ripoti ya Escrow iliandikwa kwa shinikizo la
mfanyabiashara mmoja.
“Mmoja wa wajumbe
wangu aliitwa kuombwa aingie bungeni aseme kwamba kuna mfanyabiashara mmoja
mkubwa amewapa wajumbe wa PAC fedha ili watengeneze hiyo ripoti ya PAC,”
alisema.
Aliongeza kuwa
mjumbe huyo alipokataa aliambiwa: “ Umekataa kutekeleza hili? Sasa tumetenga
Sh. milioni 500 kwa kila jimbo kwa kila mjumbe wa PAC ili kuhakikisha hawarudi
bungeni.”
Hata hivyo, Zitto hakutaka kumtaja mfanyabiashara huyo.
Zitto alifafanua
kwamba maana ya fedha hizo ni kwamba watu hao watatafuta wagombea wa kupambana
na waliokuwa wajumbe wa PAC kwa nguvu ya fedha ili wahakikishe wanakwama
kutetea majimbo yao katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Aliongeza kuwa
kitendo cha kutaja wanufaika wa Escrow wazi wazi, kama vile majaji, mawaziri na
wengine wote alijua kuwa hawawezi kukubali jambo hilo lipite hivi hivi tu.
“Kuna watu wana
fedha nyingi bwana. Kwa mfano IPTL kwa mwezi wanalipwa capacity charge Sh.
bilioni nne,” alisema.
Kwa hiyo,
kitakachoendelea kwenye uchaguzi mkuu wajumbe wa PAC watawekewa watu wa
kupambana nao kuanzia kwenye kura za maoni, hata wakishinda watawekewa
wapinzani katika majimbo yao na fedha nyingi zitatumika kuhakikisha
wanaangushwa. Wajumbe walioshirikia uchambuzi wa ripoti ya Escrow ndani ya PAC
walikuwa 17.
Wajumbe hao ni
Zitto, Deo Filikunjombe, Desderius Mipata, Asha Jecha, Lucy Owenya, Ester
Matiko, John Cheyo, Zaynabu Vulu, Ally Keissy, Zainab Kawawa, Kheri Ali Khamis,
Faida Mohammed Bakar, Ismail Aden Rage na Modestus Kilufi.
Walioongezwa ni
Kangi Lugola, Luhaga Mpina na Dk. Hamisi Kigwangalla.
Hata hivyo,
Zitto alisema hadi sasa hana ushahidi kwamba kesi yake dhidi ya Chadema
imetupwa mahakamani kwa sababu za Escrow, ingawa anasisitiza kwamba mkakati wa
kutengeneza majungu na mambo ya ovyo ovyo dhidi ya wajumbe wa PAC ulianza
wakati wa kujadili ripoti yao bungeni mwaka jana.
JE, AMENUFAIKA NA MGAWO WA ESCROW?
Zitto anasema kuwa
tuhuma kwamba naye alinufaika na fedha za Escrow hazina msingi wowote na
alikwisha kusema kuwa suala hilo lichunguzwe baada ya kuibuliwa maneno ya
kuokoteza na kuwasilishwa bungeni.
Alitoboa siri nyingine kwamba usiku wa kuamkia siku ya PAC kuwasilisha
ripoti yake kuhusu Escrow bungeni, kila mbunge anakoishi chini ya mlango wake
lilipenyezwa kabrasha lililokuwa limejaa habari za kupika, nia ikiwa ni
kubadili upepo ili kuonyesha kuwa naye (Zitto) alikuwa amenufaika na fedha
hizo.
“Wanadai kwamba
eti nami nilimtumia dada mmoja… alikwenda kuomba fedha kwa niaba yangu ili
nimuuguze mama yangu,” alisema Zitto na kuongeza kuwa:
“Huu ni uongo tu
mama yangu alikuwa mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, matibabu yake na gharama
zote za matibabu yake zilikuwa zinalipwa na Bunge hilo. Sasa mimi niombe hela
ya kumtibu wakati gharama zilikuwa zinalipwa zote?”
ESCROW NA BARAZA LA MAADILI
Hata hivyo, Zitto
anasema kuwa sakata la Escrow kwa mara nyingine tena limeibua hoja nzuri kwamba
bado taifa hili lina vyombo vya kuthibiti uwajibikaji kwani wote waliotajwa
kwenye mgawo wameitwa na Baraza la Maadili kwa njia ya wazi kabisa na mashauri
yamesikilizwa.
Anakumbusha kwamba miongoni mambo yaliozungumzwa na Tume ya
Rushwa ya Jaji Warioba ni tatizo kubwa la ufisadi na rushwa na kwamba hali hiyo
imezidi kustawi nchini kwa kuwa hakuna mfumo madhubuti wa uwajibikaji.
Alieleza kwamba kuibuka kwa Baraza la Maadili na kuwahoji
wanufaika wa mgawo wa Escrow ni kielelezo kingine kwamba mifumo ya uwajibikaji
nchini inaweza kufanya kazi.
MAGUMU KATIKA SIASA
Katika mahojiano hayo, Zitto alisisitiza kwamba bado ni mbunge
wa Kigoma Kaskazini kwa sababu anaamini mchakato wa kumvua uanachama ndani ya
Chadema kwa mujibu wa katiba na kanuni za chama chake haujafuatwa.
Anaamini kwamba baada ya kesi yake kutupwa na mahakama atapata
fursa ya kuitwa, ajitetee na ikibidi akate rufani kama taratibu za chama
zinavyosema.
Hata hivyo, anasema ni makosa kwa chama cha siasa kinachotafuta
madaraka ya dola kuzuia wanachama wake kwenda mahakamani kwani kufanya hivyo ni
sawa na kuikataa katiba ya nchi ambayo imesema wazi kwamba chombo cha juu
kabisa ndani ya nchi cha kugawa haki ni mahakama.
Anatamani aibuke mwanachama wa Chadema aende mahakamani kupinga
kanuni hiyo kwani ni kinyume cha katiba ya nchi na kwa kweli inakinzana na haki
za msingi za binadamu.
Katika mahojiano hayo, Zitto anataja miaka ya 2007 na 2014 kama
miaka migumu kwake kisiasa akiwa amepita katika mabonde na milima mingi.
Anautaja mwaka 2007 kwamba ndipo aliposimamishwa ubunge na Bunge
kwa madai ya kusema uongo baada ya kusema kwamba aliyekuwa Waziri wa Nishati na
Madini, Nazir Karamagi, alikuwa amesema uongo bungeni kuhusu mkataba wa
Buzwagi.
Anasema pamoja na ukweli huo, kufukuzwa kwake kulikipa chama
chake fursa ya kutembea nchi nzima na kueleza wananchi juu ya matatizo ya
mikataba ya madini, hatimaye mwaka 2008 Rais Jakaya Kikwete aliunda kamati ya
Jaji Bomani kuchunguza sheria na sera ya madini ambavyo vilipatikana
vipya.
Mwaka wa 2014 anautaja kuwa wa changamoto nyingi zaidi kwake
kwani ndiyo aliopoteza mama yake mzazi, Bibi Shida Salum. Alifariki dunia
Jualai mwaka jana baada ya kuugua kwa muda.
Zitto anasema mwaka jana unakuwa wa kumbukumbu kwake kwa sababu
katika hali ambayo hakutarajia alijikuta anakipeleka chama chake mahakamani ili
kupata haki yake baada ya kuvuliwa nyadhifa ndani ya chama hicho, lakini bila
kwanza kusikilizwa.
Anaamini kwamba alichaguliwa na wananchi wa Kigoma Kaskazini
siyo kwa sababu tu ya kuwa mwanachama wa Chadema kwani idadi ya wanachama hao
haizidi 3,000 wakati kura zake zilikuwa ni zaidi ya 27,000. Katika mazingira
hayo ni lazima atafute haki yake na kuheshimu uamuzi wa wananchi wa Kigoma
Kaskazini.
Magumu mengine ni jinsi alivyoshughulikia suala la Escrow,
ingawa lilikuwa ni jambo zito, anafarijika kwamba amefanikiwa kusaidia taifa
kujenga uwajibikaji kwani wapo watu wameachia ngazi kwa sababu ya ripoti ya
PAC.
NINI MAJALIWA YAKE
Zitto anaamini kwamba yote yanayotokea ni majaribio ya kisiasa,
na yana maana kubwa kwake kwani anaandaliwa kwa mkubwa zaidi.
Anataja wanasiasa wakubwa duniani ambao walipitia changamoto
kubwa na nzito kuliko zake kuwa ni pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu wa India,
Indira Gandhi. Aligombana na chama chake akiwa waziri mkuu akaenda kuanzisha
chama kipya na kureja tena kuongoza India.
Alimtaja pia Mahathir Mohamed wa Malaysia kuwa alifukuzwa akiwa
mbunge, lakini baadaye akaja kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo kwa miaka zaidi na
20 na ndiye alileta mapinduzi makubwa ya uchumi kwa kufuta umasikini kutoka
asilimia 56 ya wananchi wote hadi asilimia tatu.
Zitto pia anamtaja aliyekuwa katibu mkuu wa chama cha
Kikomunisti cha China miaka ya sitini, Deng Xiaoping, kwamba alitofautiana na
wakubwa nchini kwake na kuwekwa kizuizini mara tatu, lakini baadaye alikuja
kuwa kiongozi wa taifa hilo na anatajwa kuwa ndiye chimbuko wa maendeleo ya
China ya sasa.
Wanasiasa wengine aliowataja kuwa wamepitia tanuri la kukataliwa
na kuadhibiwa ni pamoja na Aziz Bouteflika wa Algeria, ambaye alikuwa mbunge na
kukimbizwa nchini kwake na kwenda kuishi uhamishoni Ufaransa, lakini baadaye
alifuatwa na kuomba kuja kugombea urais na kuongoza nchi hiyo.
Kwa Tanzania alimtaja Maalim Seif Sharif Hamad kwamba alifukuzwa
CCM akiwa Waziri Kiongozi, akawekwa kizuizini, akaja kuibuka na CUF na sasa ni
Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar.
Zitto aliwataka wale wote walioanza kuandika tanzia yake ya
kisiasa kuwa na subira kidogo kwa kuzingatia historia ya viongozi wengine wa
kisiasa duniani.
DEMOKRASIA NDANI YA VYAMA
Anasema demokrasia ndani ya vyama ipo na inatofautiana kati ya
chama na chama. Haiwezi kuwa sawa na fomula ya Coca Cola.
Anaamini kwamba kila chama kina mfumo na uratatibu wake, ila la
msingi ni vema kila chama kiheshimu haki za wanachama wake.
CCM ITAFUFUKA KWA KUWA UPINZANI
Zitto pamoja na changamoto zinazomkabili kwa sasa anasema kuwa
bado anamini kwamba CCM imechoka na kama inataka iwe na mabadiliko ya kweli ya
kioungozi na kuleta mabadiliko ni lazima ikae kando kwenye madaraka ya dola.
“CCM hata ifanye nini kama haitakuwa upinzani haitabadilika. CCM
imeleemewa sana uchovu,” anasema.
BVR NA KURA YA MAONI
Anaamini kuwa mchakato wa kuandikisha wapiga kura katika daftari
la wapigakura kwa mfumo wa BVR una changamoto nyingi. Hata hivyo anawataka
wananchi kujiandikisha kwa wingi zaidi kwa sababu bila kufanya hivyo watapoteza
haki yao ya kupiga kura.
Anazungumzia mchakato wa katiba mpya na maandalizi ya kura ya
maoni kuhusu katiba hiyo kwamba ni jambo linalopaswa kuwekwa pembeni kwa kuwa
kwa sasa limekaa katika mkao wa kuwagawa wananchi.
Anasisitiza kuwa mchakato wa kuandikisha katiba mpya ulivurugwa.
WENYE NACHO Vs WASIOKUWA NACHO
Anakumbusha kuwa toafuti ya kipato nchini baina ya wenye nacho
na wasio na kitu ni kubwa sana. Anaeleza kuwa hali hiyo isiposhughulikiwa taifa
halitasimama.
Alisema tofauti na Kenya kwa mfano watu wa kipato cha kati
(middle class) ni wengi, kwa maana hiyo hata pale machafuko yalipotokea Kenya
mwaka 2007 na 2008, wenyewe walikubaliana kukaa kuzungumza, tofauti na Tanzania
kundi la kati ni wachache sana na hakuna wa kuwasilikiza.
“Wasiokuwa nacho nchini ni wengi mno, wakinyanyuika hawa nchi
haitakuwako. Kwanza wana hasira na hao wachache wa kipato cha middle class,”
anaonya na kutaka mipango endelevu ipatikane kukabili tofauti ya kipato na
umasikini unaokabili jamii.
CHANZO: NIPASHE
Hakuna maoni
Chapisha Maoni