Uamsho Wapata dhamana baada ya Kusota Rumande kwa Mwaka Mmoja.
Baada
ya kusota rumande kwa takribani mwaka mmoja na miezi minne, viongozi 10
wa Jumuiya ya Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Uamsho) jana waliachiwa
kwa dhamana yenye masharti nafuu na kujumuika na familia zao.
Awali,
viongozi hao walishindwa kutimiza masharti waliyopewa na mahakama
ambayo yaliwataka kutoa fedha taslim Sh. milioni 25, kuwa na wadhamini
watatu wakiwa ni watumishi wa serikali wenye mali isiyo hamishika ya Sh.
milioni 25 pamoja na kutosafari nje ya kisiwa cha Unguja.
Hata
hivyo, baada ya kilio cha washtakiwa hao wakiongozawa na mawakili wao
Juma Abdallah na Salum Taufik, Jaji wa Mahakama Kuu Zanzibar, Fatma
Hamid Mahmoud, jana alipunguza masharti ya dhamana baada ya washtakiwa
hao ambao wamekuwa wakishikiliwa rumande kwa zaidi ya mwaka mmoja na
miezi minne kuanzia Oktoba 17, mwaka 2012, kulalamika kwamba masharti ya
dhamana ni magumu.
Jaji
huyo alikubali kila mshtakiwa kujidhamini kwa Sh. milioni 25 kwa
maandishi sambamba na kuwa na wadhamini wawili badala ya watatu huku
mmoja kati ya hao awe mtumishi serikali.
Kadhalika,
Jaji Fatma aliwaruhusu washtakiwa hao kusafiri kwenda Pemba, lakini
masharti ya kutosafiri nje ya Zanzibar pamoja na kutofanya mihadhara
miskitini na nje ya misikiti yanaendelea hadi kesi ya msingi
itakapoanzwa kusikilizwa.
Washtakiwa
hao ni Majaliwa Fikirini Majaliwa, Faridi Hadi Ahmed, Mselem Ali
Mselem, Mussa Juma Mussa, Azani Khalid Hamdani, Suleiman Juma Suleiman,
Khamis Ali Suleiman, Hassan Bakari Suleiman, Gharib Ahmed Juma na
Abdallah Said.
Washitakiwa
hao walishtakiwa kwa makosa ya kufanya uchochezi, ushawishi,
kuhamasisha fujo na kula njama ya kufanya kosa kulikosababisha uvunjifu
wa amani na usalama wa taifa Oktoba, 2011.
Jaji
Fatma alisema watuhumiwa hao wameshakaa rumande kwa muda mrefu, hivyo
mahakama imetafakari na kuona kuwa dhamana ni haki ya kila mshtakiwa
ambaye kosa lake linastahiki kupewa dhamana.
“Endapo
mshtakiwa atakaa rumande kwa muda wa miezi minne bila ya kesi kutokuwa
na ushahidi, mahakama ina uwezo wa kuifuta kesi na siyo halali
kumuadhibu mtu kwa kumuweka rumande bila ya ushahidi,” alisema Jaji
Fatma.
Aliwataka
washtakiwa hao kuhakikisha wanalinda amani na usalama wa nchi na kwamba
ikiwa watakiuka masharti hayo, mahakama itafuta dhamana waliyopewa.
Jaji Fatma aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 27, mwaka huu.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni