Zinazobamba

Chifu wa Wahehe Awakana CHADEMA na kumpigia Debe Mgimwa Uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Kalenga.

mkwawa
Chifu wa Wahehe, Abdu Sapi Mkwawa akiwakana Chadema
Wananchi wakishangilia

Mwigulu Nchemba akimuonesha aliyetobolewa jichoAkimuonesha aliyemwagiwa tindikali
 CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimefanya uzinduzi rasmi wa kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Kalenga, huku Chifu wa Wahehe, Abdu Sapi Mkwawa akikisuta Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa kutoa taarifa za uongo kwamba anamuunga mkono mgombea wao, Grace Tendega.
 
Katika uchaguzi huo, CCM imemsimamisha Godfrey Mgimwa, mtoto wa marehemu Dk William Mgimwa baada ya kushinda kwa kishindo kura za maoni za chama hicho dhidi ya wagombea wengine nane.
 
Naibu Katibu Mkuu wa CCM ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba ndiye aliyezindua kampeni hizo zilizofanyika katika kata ya Ifunda jimboni humo juzi.
 
Akishangiliwa na mamia ya wafuasi na wanachama wa chama hicho, Mkwawa alisema “ukoo wetu una historia isiyopingika ndani ya CCM, mimi ni kada wa CCM ninayehenzi historia hiyo na hata siku moja siwezi kufanya vinavyotangazwa na Chadema kwenye mitandao na magazeti.”
 
Huku akichanganya Kiswahili na Kihehe ili aeleweke vyema na watu wa jimbo hilo, alisema kama Chifu hakuwa na hiyana pale mgombea wa Chadema na viongozi wa chama chake walipokwenda kumjulia hali na kumuomba awe pamoja nao katika uzinduzi wa kampeni zao.
 
“Ilikuwa Februari 22 siku ambayo chama hicho kilikuwa kinazindua kampeni zake za uchaguzi; kama ambavyo angefanya kiongozi yoyote anayeheshimu mila za kabila lake, nami sikuwa na sababu ya kuwakatalia, nilichofanya ni kudumisha mila kwa kuzingatia kwamba mgombea wao ni mhehe pia” alisema.
 
Alisema “nafahamu kwamba uchaguzi huu ni huru na wa kidemokrasia, nilipoombwa kupanda katika jukwaa lao sikuona tatizo pia na nilipopewa fursa ya kuwasalimia nilisisitiza vyama vilivyosimamisha wagombea Kalenga viendeshe kampeni zao kwa amani na utulivu na huo ndio ujumbe ulionisukuma kupanda katika jukwaa lao.”
 
Alisema baada ya wananchi waliohudhuria uzinduzi wa kampeni hizo kuitikia mwito wake huo aliondoka jukwaani kwa kumtaka mgombea wao huyo aendelee na kampeni kwa amani na utulivu.
 
“Sikutoa baraka za kumtakia ushindi mgombea wa Chadema kwasababu mimi ni CCM na wao wanajua hivyo, wanajua pia kwamba sina ugomvi na chama changu; nilichowaomba ni kufanya kampeni zao kwa amani kwasababu kama Chifu nataka kuona uchaguzi huu hauwi na machafuko,” alisema.
 
Akizindua kampeni hizo, Nchemba alisema CCM imetawala nchi hii kwa miaka 37 na hakuna mtu hata mmoja aliyeuawa katika mikutano yake kama inavyotokea kwa Chadema.
 
“Katika kipindi cha miaka mitatu, watu nane wamafariki kwenye mikutano tofauti tofauti ya chama hicho,” alisema.
 
Akidhihirisha kwa umma wa Kalenga vurugu zinazofanywa na chama hicho, Nchemba aliwapandisha jukwaani watu wawili, mmoja akiwa ni yule aliyemwagiwa tindikali katika uchaguzi mdogo wa Igunga na wa pili aliyetobolewa jicho katika uchaguzi mdogo wa udiwani Kahama.
 
Nchemba alipongeza hekima na busara alizonazo Rais Jakaya Kikwete akisema zinasaidia sana kuifanya nchi hii iendelee kuwa ya utulivu na amani vinginevyo uvumilivu wa chokochoko dhidi ya CCM usingevumilika.
 
Kwa masikitiko makubwa, Katibu wa CCM Wilaya ya Mufindi, Miraji Mtaturu alionesha vibao virefu vitatu vye misumari alivyodai vilivyowekwa na wafuasi wa Chadema katika moja ya barabara za jimbo hilo ili kutoboa tairi za magari ya kampeni ya CCM.
 
“Tunawajua kwa majina wahusika wa tukio hili la kidhalimu; na taarifa hii tumekwishawasilisha Polisi, wanaendelea kuifanyia kazi; hii ni hatari kuendelea kushabikia chama kinachoshindwa kuwaeleza wananchi kitawafanyia nini na badala yake kuhamsisha vurugu,” alisema.
 
Akiomba kura kwa wapiga kura wa jimbo hilo, Godfrey Mgimwa alisema “mimi sio mropokaji kama wenzetu wa Chadema, mimi ni mtendaji, nipeni kura zenu nikamalizie kazi iliyoanza kutekelezwa na marehemu baba yangu.”
 
Alisema alikuwa mshauri mkuu wa marehemu baba yake wakati wa uhai wake kwasababu ya uwezo wake mkubwa kitaaluma.
 
“Mimi ni mtaalamu wa biashara, masoko na fedha; na mpaka nakuja kugombea ubunge nilikuwa mwajiriwa wa benki, kwahiyo marehemu mzee alikuwa anaujua uwezo wangu kichwani na alikuwa akitaka ushauri wa mara kwa mara kutoka kwangu,” alisema.
 
Alisema analifahamu vyema jimbo lake la Kalenga na amafanya utafiti uliomuwezesha kuyajua vyema matatizo ya wana Kalenga.
 
“Nipeni kura zenu zote, nazifahamu changamoto katika sekta ya elimu, afya, maji, barabara, mawasiliano na kilimo; nitazifanyia katika kwa kushirikiana na nyinyi kuzitatua kwa kupitia Ilani yetu ya CCM,” alisema.
 
Wengine waliopata fursa ya kuhutubia mkutano huo ni pamoja na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa Jesca Msambatavangu na wabunge mbalimbali wa chama hicho mkoani hapa.
 
Wabunge hao ni pamoja na Naibu Waziri wa Wanawake Jinsia na Watoto, Dk Pindi Chana, Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa, Leadiana Mng’ongo na Ritta Kabati na Mbunge wa Mufindi Kusini Medrad Kigola

Hakuna maoni