Mgimwa azushiwa kifo, Kikwete apasua kichwa
WAKATI
mawaziri wanne wameng’olewa na wengine walioitwa mizigo wanatarajiwa
kutimuliwa wakati wowote, Rais Jakaya Kikwete yupo katika wakati mgumu
wa kusaka warithi wa nafasi hizo, fullhabari limegundua
Ugumu wa kusaka warithi wa mawaziri hao, umeongezeka zaidi jana baada
ya Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk. William Mgimwa kuzushiwa kifo
kutokana na afya yake kuzorota.
Hata hivyo, uvumi huo ulioenezwa kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu za
mkononi na kupitia mitandao ya kijamii, haukuwa sahihi, lakini taarifa
zaidi kuhusu afya za Waziri Mgimwa zinasema kuwa atahitaji muda mrefu
kupumzika, hivyo nafasi yake lazima izibwe na waziri mwingine kutokana
na unyeti wake.
Mawaziri walioondolewa madarakani ni Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na
Jeshi la Kujenga Taifa), Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii),
Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani) na David Mathayo (Mifugo na Maendeleo
ya Uvuvi).
Kuondolewa kwa mawaziri hao pia kunaelezwa kumelenga kumnusuru Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda ambaye amekuwa akitajwa kwa kushindwa kuwasimamia
mawaziri walio chini yake.
Kuondoka kwa mawaziri hao, kutamsaidia au kumwongezea mzigo Rais
Kikwete kutimiza mapendekezo ya Kamati Kuu (CC) ya CCM iliyotaka
awaondoe mawaziri saba iliyowaita ‘mizigo’.
Wadadisi wa mambo ya siasa, wanasema kuwa mazingira ya kupata baraza
jipya la mawaziri, yanampa wakati mgumu sana Rais Kikwete kufanya uamuzi
wa nani aingie na nani atoke.
Jina la mbunge mpya wa kuteuliwa na rais, Dk. Asha Rose Migiro,
limekuwa likitajwa mara nyingi kwamba hatua ya kuingizwa ndani ya Bunge
hivi karibuni, huenda kuna nia ya kutaka kumteua kuwa mmoja wa mawaziri,
na sasa baada ya kutemwa kwa mawaziri hao wanne turufu inaelekezwa
kwake kuwa miongoni mwa watakaoziba moja ya nafasi.
Hata hivyo, duru nyingine za siasa zinasema nafasi ya Dk. Migiro
kuteuliwa kushika wizara yoyote ni finyu kutokana na ukweli kwamba Chama
Cha Mapinduzi (CCM), kinamhitaji sana kwenye sekretarieti ambako
anaongoza Idara ya Mambo ya Nje.
Chini ya utaratibu mpya, mjumbe wa sekretarieti, haruhusiwi kuwa
waziri na ndiyo maana Januari Makamba, Naibu Waziri wa Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia, alilazimika kuachia nafasi ya ujumbe wa
sekretarieti mara baada ya kuteuliwa kuingia katika Baraza la Mawaziri.
Inaelezwa kuwa tangu alipoingia kwenye sekretarieti, Dk. Migiro kwa
kutumia uzoefu wake mambo ya kimataifa amekuwa kiungo kikubwa kwa CCM na
mataifa ya nje.
Mjumbe mwingine wa sekretarieti anayetajwa kuwamo kwenye baraza jipya
ni Mwigulu Nchemba ambaye kwa sasa ni Naibu Katibu Mkuu CCM Bara.
Majina mengine yanayotajwa miongoni mwa wabunge ni pamoja na Dk.
Khamis Kigwangala, Peter Serukamba ambaye ameonyesha uwezo mkubwa tangu
alipochaguliwa kuongoza Kamati ya Bunge ya Miundombinu, ingawa nafasi
yake kwenye baraza jipya inaelezwa kuathiriwa na uhusiano wake na Mbunge
wa Monduli na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
Katika majina hayo, yapo pia majina ya waliojiita wapambanaji wa
ufisadi kama Anne Kilango Malecela, James Lembeli na wabunge wengine
mwiba kwa CCM kama Kangi Lugola na Deo Filikunjombe
No comments
Post a Comment