Dk. Slaa azidi kuchanja mbuga; atoa maagizo nchi nzima 'waraka' wa uasi
Katibu Mkuu Dk. Willibroad Slaa ameendelea na ziara yake kwa kutembelea
vijiji vya majimbo mawili Bukene na Nzega, wilayani Nzega, Mkoa wa
Tabora, ambapo ametumia mkutano mkubwa wa hadhara mjini Nzega kutoa
maagizo kwa viongozi wa chama nchi nzima kuhusu waraka unaosambazwa nchi
nzima ukidaiwa kutoka Makao Makuu.

Akihutubia maelfu ya wananchi wa Nzega mjini akiwa ametokea eneo la Lusu
ambako 'kulikuwa' na Mgodi wa Resolute, Dk. Slaa amesema kuna waraka
unasambazwa kwa viongozi wa wilaya huku matapeli wa kisiasa wakiwalaghai
viongozi hao kuwa umetolewa Makao Makuu kutoka Ofisi ya Katibu Mkuu wa
chama.
"Nimeletewa taarifa hapa kuna watu wamepeleka fomu zao wakitaka watu
watie saini kitu kinaitwa petition...kwa sababu wanajua wanachofanya ni
muendelezo wa uasi, juu ya ile fomu hakujaandikwa kichwa cha habari
chochote. Wanawadanganya watu kuwa fomu hizo zimetoka Makao Makuu.
"Si kweli...Makao Makuu kwa maana ya Ofisi ya Katibu Mkuu haijatoa kitu
cha namna hiyo. Wasidanganyike. Tunawapongeza wengi wao wameshtuka na
wametupigia simu wakihoji kitu hicho. Tunaujua mchezo unaotaka
kufanyika. Lakini tunawaambia wahusika huo ni uasi.
"Tunawaambia watu wote waliopelekewa hizo barua zikiwa na fomu, fomu
ambazo hazina kitu, lakini wanaambiwa wajaze kwa kutia saini kwa sababu
zimetoka taifa, wakatae. Mfano watu wa Lindi na Mtwara ambao wametupigia
simu baada ya kugutuka. Watu wanasainishwa vitu wasivyovijua. Makao
Makuu wala ofisi ya Katibu Mkuu haijatuma kitu cha namna hiyo.
"Wamepeleka pesa watu wanalipwa hela, najiuliza hizo hela malengo yake
nini na nani amezitoa na kwa maslahi ya nani. Hawa watu wanaochochea
uasi ofisi yangu inaagiza wawe makini sana, watajikuta matatani.
Tunaujua mpango huo wote," alisema Dk. Slaa huku akishangiliwa na umati
wa watu kabla hajakaribisha maswali kutoka kwa wananchi.
No comments
Post a Comment