Zinazobamba

Auawa kwa kukutwa uchi mgodini


MKAZI wa Kijiji cha Kapanda, wilayani Mlele, Katavi, Yunge Maboja (70), amefariki dunia baada ya kushambuliwa na wananchi kwa kupigwa na silaha za jadi, ngumi na mateke baada ya kukutwa akiwa uchi kwenye shimo la kuchimba dhahabu.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Dhahili Kidavashari, alisema Maboja alishambuliwa juzi, saa 7 usiku  katika Kijiji cha Kapanda wakimtuhumu alikuwa akiroga ili mwenye shimo hilo asipate dhahabu.
Alisema wiki tatu kabla ya tukio hilo, Maboja alimuazimisha Idd Kipara shoka alilokuwa akitumia katika shughuli zake, alipokuwa akimtafuta mtu aliyemuazimisha alichungulia ndani ya shimo ambalo walikuwemo watu wawili wakichimba madini.
Kamanda Kidavashari alisema watu hao walishitushwa na kitendo cha kuchunguliwa muda huo, hivyo iliwalazimu marehemu akiwa mtupu.
Alisema ndipo watu hao; Abui  na Hassan walipoanza  kumshambulia kwa maneno ya kashfa kuwa ni mchawi na ndiyo maana amefika kwenye shimo lao akiwa uchi, hali inayochangia  wasipate madini kwa muda mrefu.

Kidavashari alieleza kuwa walimshambulia kwa fimbo na mateke na kumlazimisha  awapeleke kwa mwenyeji wake, Juma Ngegeshi ili awapatie uchawi, lakini walimkuta mkewe, Asha  Shabani ambaye alieleza hakuna kitu wanachohitaji, hali iliyochangia naye kuanza kushambuliwa kwa fimbo usoni na mgongoni.
“Asha alipiga mayowe ya kuomba msaada na ndipo majirani walipofika na kumkuta Maboja akiwa uchi, nao waliungana  kuwashambulia.
Kidavashari alieleza majeruhi wote wawili walifikishwa kituo cha polisi cha Mpanda na baadaye kupelekwa Hospitali ya Wilaya ya Mpanda ambako Maboja alifariki dunia  akiwa  anaendelea kupatiwa matibabu.
Jitihada za kuwasaka  wahusika wa tukio  zilifanyika  na polisi inawashikilia watu wawili ambao ni  Yunge   Hassan  (43) na  Ayub Samwel (30) kwa mahojiano.
Wakati huo huo, Raia wa China, Chen Gungson anayemiliki kampuni ya uchimbaji madini ya Got Accident on Ming Camp, amefariki dunia baada ya kutumbukia ndani ya shimo la mgodi wa dhahabu katika machimbo ya Ibidi, wilayani Mlele.
Tukio hilo lilitokea juzi, saa 3 asubuhi wakati raia huyo wa China alipokuwa akikagua maeneo anayofanyia shughuli za uchimbaji dhahabu. Mwili wa marehemu umehifadhiwa hospitali ya wilaya.

No comments