SAT YAFUATILIA MRADI WA VIUNGO MUHEZA, YAFIKIA WAKULIMA ZAIDI YA 1,550
MUHEZA-TANGA.
Mfumo wa vikundi vya wakulima unaotumiwa na Shirika la Kilimo Endelevu Tanzania (SAT) katika utekelezaji wa Mradi wa Viungo umewezesha kuwafikia wakulima zaidi ya 1,550 katika Halmashauri ya Wilaya ya Muheza mkoani Tanga, huku vikundi 62 vikiwa vimeanzishwa tangu mradi huo ulipoanza mwaka 2025.
Mafanikio hayo yameelezwa wakati SAT ikifanya ziara ya siku mbili ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa mradi huo, iliyolenga kukagua shughuli za vikundi, kutathmini maendeleo ya uzalishaji, kubaini changamoto na kuweka mikakati ya kuboresha utendaji wa wakulima.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Meneja wa Mradi wa Viungo wa SAT, Joel Paulo, alisema mradi huo unatekelezwa katika halmashauri tatu ambazo ni Morogoro Vijijini, Mvomero na Muheza Mkoani Tanga, kwa kushirikiana na wakulima wawezeshaji, maafisa ugani na maafisa maendeleo ya jamii katika kata na vijiji husika.
Paulo alisema SAT imeamua kutumia mfumo wa vikundi kwa kuwa unasaidia kufikisha elimu kwa wakulima wengi zaidi kwa wakati mmoja, tofauti na mfumo wa kutembelea na kutoa mafunzo kwa kila mkulima mmoja mmoja.
Alisema kupitia mfumo huo, shirika limefanikiwa kuwafikia wakulima zaidi ya 1,550, huku wakulima wawezeshaji wakiwa kiungo muhimu katika kusambaza elimu na mbinu bora za uzalishaji katika maeneo yao.
Alifafanua kuwa wakulima wanaochaguliwa kuwa wawezeshaji hupatiwa mafunzo ya takribani siku tano katika Kituo cha Wakulima Vianzi kilichopo wilayani Mvomero mkoani Morogoro, ambako hujifunza mbinu za uwezeshaji, mnyororo wa thamani wa mazao ya viungo na namna ya kuweka akiba.
Baada ya mafunzo hayo, wakulima hurejea katika maeneo yao na kuanzisha vikundi kwa kushirikiana na viongozi wa vijiji na wataalamu wa kilimo na maendeleo ya jamii. Vikundi hivyo hupatiwa vitendea kazi na mbegu na kuanzisha vitalu vya uzalishaji huku vikiendelea kupata ushauri wa kitaalamu kutoka SAT.
Hata hivyo, Paulo alisema baadhi ya vikundi walivyotembelea leo katika siku ya kwanza ya ziara wamebaini bado vinakabiliwa na changamoto za mahudhurio yasiyoridhisha na uendeshaji wa kiutawala, hali inayohitaji kuimarishwa kwa usimamizi na ushiriki wa wanachama.
Alisema SAT kwa kushirikiana na maafisa kilimo, maafisa maendeleo ya jamii na wakulima wawezeshaji inaendelea kutoa ushauri na kuweka mikakati ya kuongeza wanachama, kuimarisha uongozi na kuboresha uzalishaji wa miche.
Kwa upande wake, Mwezeshaji wa Kikundi cha Mlinga,kilichopo kijiji cha Tongwe William Makame, alisema ushirikiano na SAT umewasaidia kupiga hatua katika uzalishaji wa mazao ya viungo na kujifunza mbinu rafiki kwa mazingira, tofauti na hali ya awali ambapo walikuwa wakilima bila kufikia kiwango cha kuridhisha.
Alisema kikundi hicho kimejikita katika uoteshaji wa miche ya mdalasini, iliki, karafuu na pilipili manga, ambapo awali walizalisha takribani miche 4,000 na kugawana kwa ajili ya kuanzisha mashamba yao, ikiwemo kutoa miche 30 ya pilipili manga kwa kila mwanachama.
Aliongeza kuwa kwa sasa kitalu chao cha kwanza kina takribani miche 5,600 ya pilipili manga na wanatarajia kuongeza hadi miche 10,000, huku wakiendelea na maandalizi ya uzalishaji wa miche 10,000 ya kakao.
Makame alisema kupitia mafunzo hayo wamejifunza pia kutengeneza mbolea na viuatilifu vya asili kwa kutumia mimea kama mwarobaini, utupa na mpapai kwa ajili ya kudhibiti wadudu na kuboresha afya ya mimea bila kutegemea zaidi kemikali za viwandani.
Naye Mwenyekiti wa Kikundi cha Zimbiku, Mohamedi Adamu Chamiwa, alisema kikundi hicho kilichoanzishwa Mei 2025 katika Kata ya Tongwe, Kijiji cha Masimba, kinajihusisha na upandaji wa miti ya kakao na pilipili manga, kilimo cha bustani pamoja na uwekaji wa akiba na hisa.
Alisema kupitia shughuli hizo wamefanikiwa kuweka akiba inayofikia takribani Sh 500,000, ambayo imekuwa msaada kwa wanachama wanapokumbwa na changamoto za kiafya na kiuchumi, sambamba na kusaidia baadhi ya wanajamii wenye uhitaji.
Katika kuonesha namna elimu inayotolewa kupitia vikundi inavyoweza kuwafikia wakulima wengine katika jamii, ziara ya SAT ilipata fursa ya kumtembelea mkulima binafsi, Robert Mgelwa, mkazi wa Kijiji cha Tongwe, kitongoji cha Masiwa, ambaye licha ya kutokuwa mwanachama wa kikundi, amekuwa akishirikiana kwa karibu na Kikundi cha Mlinga kinachoongozwa na Makame.
Mgelwa alisema tayari alikuwa akijihusisha na kilimo cha kakao na pilipili manga kwa muda mrefu, lakini kupitia mafunzo aliyopata kwa kushirikiana na wakulima wa kikundi hicho, ameongeza uelewa kuhusu uandaaji na uzalishaji wa miche, jambo lililomsaidia kuboresha shughuli zake.
Alisema kwa sasa analima kakao katika eneo la ekari tatu na pilipili manga ekari mbili, huku pia akijihusisha na uzalishaji wa miche ya mazao hayo kwa ajili ya kuuza.
Alieleza kuwa msimu uliopita aliweza kuuza takribani miche 3,000 ya kakao na miche 1,500 ya pilipili manga, lakini changamoto kubwa inayomkabili ni kukosekana kwa soko la uhakika kwa wakati, hali inayosababisha baadhi ya miche kubaki kwenye vitalu kwa muda mrefu na kuhitaji kuhamishwa ili iendelee kustawi.
Kwa upande wa mavuno, Mgelwa alisema kwa mwaka mzima huvuna zaidi ya kilo 1,000 za kakao na kati ya kilo 1,500 hadi 2,000 za pilipili manga, huku bei ya kilo moja ya mazao hayo ikiwa kati ya Sh 10,000 na Sh 12,000.
Aliongeza kuwa baadhi ya mimea ya pilipili manga iliwahi kuathiriwa na ukame na ugonjwa wa mnyauko, hali iliyomlazimu kupanda upya katika baadhi ya maeneo, huku akieleza kuwa analenga kuongeza uzalishaji wa miche hadi kufikia angalau 6,000 na kuboresha usimamizi wa shughuli zake.
Akitoa ushauri kwa mkulima huyo, Paulo alisisitiza umuhimu wa kuweka kumbukumbu sahihi za uzalishaji, gharama, mauzo na thamani ya uwekezaji ili kumwezesha kufuatilia faida na hasara kwa mwezi na mwaka.
Alimshauri pia kupanga miche katika makundi yenye idadi maalumu, ikiwemo makundi ya miche 100, ili kurahisisha ufuatiliaji wa ukuaji, kubaini miche iliyokufa na kuhakikisha inapata huduma stahiki, akieleza kuwa shughuli zake zimefikia kiwango cha uwekezaji unaohitaji usimamizi wa kitaalamu.
Kwa mujibu wa Paulo, SAT itaendelea kufuatilia vikundi na wakulima wawezeshaji ili kubaini maeneo yanayohitaji maboresho, kuandaa mafunzo rejea na kuimarisha uzalishaji wa mazao ya viungo pamoja na mnyororo wake wa thamani.

No comments
Post a Comment