Zinazobamba

TAKUKURU TEMEKE YAONGEZA MAPATO YA HALMASHAURI KWA SH1.17 BILIONI

Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Temeke Emma Mwasyoge akizungumza na Waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akiwasilisha taarifa ya utakelezaji wa shughuli za taasisi hiyo Kwa kipindi Aprili hadi Septempa 2026.

Na Mussa Augustine:Dar es Salaam

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke, kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, imefanikisha kuongeza ukusanyaji wa mapato ya halmashauri hiyo kwa kiasi cha Sh1.17 bilioni kupitia ufuatiliaji wa ulipaji wa ushuru wa huduma (Service Levy) na usimamizi wa utozaji wa faini.

Taarifa hiyo imetolewa leo Novemba 24, 2026, jijini Dar es Salaam na Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Temeke, Emma Mwasyoge, wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za taasisi hiyo kwa kipindi cha Aprili hadi Septemba 2026.

Mwasyoge amesema mafanikio hayo yametokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na TAKUKURU, ikiwemo kufanya ufuatiliaji na uhakiki wa taarifa za walipakodi, kubaini kampuni ambazo hazikulipa au zililipa pungufu ya ushuru wa huduma, pamoja na kuhakikisha wahusika wanatekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria na taratibu za mapato.

Mwasyoge amesema katika ufuatiliaji huo, jumla ya kampuni 94 zilifikiwa na kufanyiwa uhakiki wa malipo ya ushuru wa huduma kwa kipindi cha Julai 2025 hadi Juni 2026.

Ameeleza kuwa kati ya kampuni hizo, 50 zilibainika kuwa na madeni au malipo pungufu na baada ya kufuatiliwa, kushauriwa na kuchukuliwa hatua stahiki, zilitekeleza wajibu wake na kulipa kiasi cha Sh1,066,020,516.90.

Aidha, amesema TAKUKURU kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Temeke na Manispaa ya Temeke iliendelea kusimamia utozaji wa faini kwa wafanyabiashara waliokuwa wakifanya biashara katika maeneo yasiyoruhusiwa, ikiwemo Tandika, Mbagala, Kongowe, Buza na maeneo mengine ndani ya Wilaya ya Temeke.

"Kupitia zoezi hilo, jumla ya Sh104,600,000 zilikusanywa na kuingizwa katika mapato ya Halmashauri kuanzia Septemba 25 hadi 31, 2026."amesema Mwasyoge 

Ameongeza kuwa ushirikiano huo haukulenga tu kuongeza mapato, bali pia kuziba mianya ya rushwa na upotevu wa mapato ya Serikali wakati wa ukusanyaji wa mapato, kuimarisha uwajibikaji wa watendaji pamoja na kuhakikisha wafanyabiashara na walipakodi wanatekeleza wajibu wao kwa usawa na haki.

No comments