TAKUKURU TEMEKE YABAINI CHANGAMOTO MIRADI YA SH. BILIONI 13 TEMEKE, KIGAMBONI
Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Temeke Emma Mwasyoge akizungumza na Waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akiwasilisha taarifa ya utakelezaji wa shughuli za taasisi hiyo Kwa kipindi cha Aprili hadi Septempa 2026.
Na Mussa Augustine:Dar es salaam
TAKUKURU Mkoa wa Temeke imebaini changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa miradi mitano ya maendeleo yenye thamani ya Shilingi bilioni 13.24, iliyofuatiliwa katika kipindi cha Aprili hadi Septemba 2026.
Changamoto zilizobainika ni pamoja na kuchelewa kuanza kwa utekelezaji wa baadhi ya miradi, ucheleweshaji wa vifaa kufikishwa katika maeneo ya miradi, kuchelewa kukamilika kwa miradi, pamoja na baadhi ya wakandarasi kutokuwa na usajili kutoka mamlaka husika ikiwemo OSHA na Bodi ya Wakandarasi.
Hayo yamesemwa leo, Novemba 24, 2026, na Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Temeke, Emma Mwasyoge, wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za taasisi hiyo kwa kipindi cha Aprili hadi Septemba 2026.
Amesema kati ya miradi hiyo mitano, mitatu yenye thamani ya Shilingi bilioni 12,239,354,234 ilitekelezwa katika Manispaa ya Temeke, huku miradi miwili yenye thamani ya Shilingi bilioni 1,001,500,000 ikitekelezwa katika Manispaa ya Kigamboni.
Mwasyoge amesema katika baadhi ya miradi, pia ilibainika kuwepo kwa matofali yasiyokidhi viwango vya ubora vinavyotakiwa.
Hata hivyo amesema kuwa kutokana na changamoto hizo, maelekezo yalitolewa kwa wahusika ili kuzitatua ndani ya muda maalumu uliowekwa.
Aidha, wakandarasi waliagizwa kukamilisha taratibu za usajili katika mamlaka husika, vifaa vilivyokuwa vimechelewa vilifikishwa katika maeneo ya miradi, huku matofali yaliyobainika kutokuwa na viwango yakiondolewa na kubadilishwa na matofali yenye ubora unaokidhi viwango vinavyotakiwa.
Mwasyoge ameitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na ujenzi wa Kituo cha Afya Kata ya Tungi awamu ya pili, wenye thamani ya Shilingi milioni 710, ujenzi wa Shule Mpya ya Msingi Tundwi Songani, ujenzi wa Shule Mpya ya Msingi Sakafu Tano Mwembe Bamia, pamoja na ujenzi wa Shule Mpya ya Msingi ya English Medium Vigoa, Sakafu Tano.
Naibu Mkuu huyo wa TAKUKURU Mkoa wa Temeke amehitimisha kwa kusema kuwa miradi hiyo minne imegharimu jumla ya Shilingi bilioni 12,530,854,234.

No comments
Post a Comment