SACP MULIRO AONYA POLISI KUJIHUSISHA NA MAJUKUMU YA TRA
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Jumanne Muliro, amewataka askari wa Jeshi la Polisi kuacha mara moja kuingilia majukumu ya mamlaka nyingine, ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kufuatia malalamiko ya wafanyabiashara wa Kariakoo kuhusu kunyanyaswa.
Akizungumza wakati wa ziara yake katika eneo la Kariakoo, Kamanda Murilo amekutana na wafanyabiashara wa Jumuiya ya Raha Square kwa lengo la kusikiliza na kutatua changamoto za kiusalama.
Amesisitiza kuwa si jukumu la polisi kukagua mizigo ya wafanyabiashara wala kushughulikia masuala ya kodi, na kuonya kuwa askari watakaokiuka maelekezo hayo watachukuliwa hatua kali.
Awali, wafanyabiashara walilalamikia tabia ya baadhi ya askari kusimamisha mizigo yao katika makutano ya barabara na kukagua risiti za biashara, wakieleza kuwa hali hiyo imekuwa kero na chanzo cha usumbufu mkubwa.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara, Mwenyekiti wa Kijiwe cha Raha Square, Rweyemamu Erasto, amesema licha ya changamoto hiyo, pia wanakabiliwa na hali duni ya usalama hasa nyakati za usiku wanapofunga biashara zao.
Amebainisha kuwa baadhi ya barabara bado hazijafunguliwa ipasavyo, hali inayochangia vitendo vya uporaji, huku biashara zinazofanyika barabarani zikiziba njia na kuongeza hatari ya ajali.
Aidha, wafanyabiashara walieleza wasiwasi wao kuhusu ongezeko la watoto wa mitaani wanaozagaa nyakati za usiku pamoja na uwepo wa watu wasiokuwa na utambulisho unaoeleweka, wakidai hali hiyo inahatarisha usalama wao na mali zao.
Katika mapendekezo yao, waliomba kufunguliwa kwa barabara zote za Kariakoo, kuondolewa kwa biashara zisizo rasmi barabarani, pamoja na kufungwa kwa mifumo ya kamera za ulinzi (CCTV) ili kusaidia kudhibiti uhalifu.
Akijibu hoja hizo, Kamanda Murilo amesema Jeshi la Polisi linaendelea kushirikiana na mamlaka mbalimbali kuhakikisha eneo la Kariakoo linakuwa salama. Aliahidi kufanyia kazi changamoto zote zilizotolewa na wafanyabiashara.

No comments
Post a Comment