SERIKALI YA AWAMU YA SITA IMEWEKA MSINGI IMARA MAGEUZI YA KIUCHUMI.KAPINGA.
Waziri wa Viwanda na Biashara,Judith Kapinga,amesema Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imeweka msingi imara wa mageuzi ya kiuchumi kupitia ajenda ya ujenzi wa Tanzania ya viwanda.
Hatua hiyo inalenga kuongeza uzalishaji, kupanua masoko,kuboresha mazingira ya biashara na kuhakikisha kila Mtanzania,hususan vijana,anapata fursa ya kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kisasa.
Hayo ameyasema leo Desemba 18,Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na Waandishi wa habari kuelezea,mafanikio na mipango mikakati ya Wizara hiyo katika kuinua sekta ya Viwanda na biashara katika Serikali ya awamu ya sita.
Akizungumza kuhusu fursa za ajira zitokanazo na uwekezaji katika sekta za viwanda na biashara,Waziri Kapinga amesema Serikali imeweka mkazo mkubwa katika kukuza sekta hizo ili kuongeza ajira,hususan kwa vijana, kupitia uwekezaji mkubwa pamoja na maboresho ya sera,sheria na mifumo ya biashara.
Aidha amesema Wizara ya Viwanda na Biashara ina jukumu la kusimamia maendeleo ya viwanda,biashara,viwanda vidogo na vya kati,ubora wa bidhaa, ushindani wa haki,usajili wa biashara pamoja na kukuza masoko ya ndani na nje ya nchi.
"Kupitia taasisi 13 zilizopo chini ya Wizara,Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na kuvutia uwekezaji wa ndani na nje ya nchi,jambo lililosaidia kuchochea ukuaji wa sekta binafsi na uanzishwaji wa ajira"amesema.
Amesema kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inaweka viwanda imara,biashara shindani na sekta binafsi yenye nguvu kama nguzo kuu za kufikia uchumi wa kipato cha kati cha juu.
Waziri huyo wa Viwanda na biashara amesema kuwa kuongeza thamani ya malighafi,kukuza mauzo ya nje na kuimarisha ujasiriamali kutachochea ajira na kujenga uchumi jumuishi.
Amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya Sita,sera muhimu zimehuishwa na sheria zaidi ya 12 kurekebishwa ili kuondoa vikwazo vya biashara,hatua iliyoongeza kwa kiasi kikubwa usajili wa kampuni,majina ya biashara,leseni za viwanda na hati za bishara,kuimarika kwa mazingira ya biashara nchini.
Amesema kuwa uzalishaji wa viwandani umeongezeka na baadhi ya bidhaa ikiwemo saruji, mabati, vioo na tiles(malumalu)sasa zinauzwa nje ya nchi,hatua inayosaidia kuongeza mapato ya taifa na kupanua masoko ya bidhaa za Tanzania.
"Ndugu Waandishi wa habari,Serikali pia imeendelea kuhamasisha uchakataji wa mazao ya kilimo ili kuuza bidhaa zilizoongezwa thamani badala ya kuuza malighafi pekee"amesema.
Waziri Kapinga amesema Katika masoko ya kimataifa,Tanzania imenufaika na Soko huru la biashara barani Afrika (AfCFTA) pamoja na masoko ya Ulaya na Asia,ambapo mauzo ya nje yameongezeka kwa kiwango kikubwa.
Aidha aliwahimiza vijana kuchangamkia fursa hizo kwa kuanzisha biashara za kuuza nje,hususan katika kilimo biashara na viwanda vidogo.
Akizungumzia miradi ya kimkakati, Waziri Kapinga ameitaja miradi ya Mchuchuma na Liganga,Magadi Soda Engaruka,Maganga Matitu na Katewaka kuwa ni vyanzo vikubwa vya ajira kwa vijana katika nyanja za uhandisi,ufundi, uchimbaji na biashara.
Aidha amebainisha kuwa uanzishwaji wa kongani 34 za viwanda nchini unatarajiwa kuzalisha maelfu ya ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.
Hata hivyo kuhusu uwezeshaji,amesema Serikali kupitia taasisi kama SIDO,TIRDO na TEMDO inaendelea kutoa mafunzo, teknolojia, mitaji na huduma za ubora kwa vijana na wajasiriamali wadogo.
Amemaliza kwa kusema kuwa mikopo ya riba nafuu kupitia mifuko ya NEDF, dhamana za mikopo na ushirikiano na benki imetajwa kuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa biashara na uanzishwaji wa ajira nchini.

No comments
Post a Comment