KAPINGA:WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA KUKUZA MAENDELEO YA VIWANDA,SEKTA YA BIASHARA NA MASOKO.
Na Moses Mashala.
Waziri wa Viwanda na Biashara Judith Kapinga amesema kuwa Serikali kupitia Sekta ya Viwanda na biashara imepanga kujikita katika maeneo matatu muhimu katika Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 20250 ambayo ni maendeleo ya Viwanda,Sekta ya biashara na masoko,pamoja na Sekta binafsi na ujasiriamali.
Waziri Kapinga amesema hayo leo Desemba 18,2025 wakati akizungumza na Waandishi wa habari kuelezea mafanikio na mipango mikakati ya Wizara hiyo katika Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Akizungumzia Maendeleo ya Viwanda,amesema kuwa dira ya 2050 inaweka viwanda na uzalishaji kama msingi wa mabadiliko ya kiuchumi, ikitambua kwamba Tanzania itafikia kwa urahisi maendeleo ya kudumu kwa kuongeza mnyororo wa thamani.
"Mnyororo wa thamani unaongeza thamani ya bidhaa,unazalisha ajira, unapunguza uagizaji wa bidhaa nje ya nchi,unavutia uwekezaji,na hapa ndipo viwanda vinapozalishwa na mwisho una kuza uchumi shirikishi,tunapanua wigo wa watanzania kushirki katika biashara" amesema Waziri Kapinga
Kuhusu Sekta ya Biashara na Masoko ya Nje amesema kuwa katika sekta ya biashara,Dira ya 2050 inasisitiza kuimarisha ushiriki wa Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Aidha amesema takwimu za biashara za nje zinaonyesha kuwa thamani ya jumla ya mauzo ya nje ya bidhaa na huduma nchini imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 9.8 kufikia takriban dola 14.72 bilioni mwaka 2024 ikilinganishwa na mwaka wa kabla yake,japokuwa wanakabiliwa na upungufu wa biashara (trade deficit), ambapo uagizaji wa bidhaa unaendelea kuwa juu kuliko mauzo nje ya nchi.
Halikadhalika kuhusu Sekta Binafsi na Ujasiriamali amesema Dira ya 2050 inaeleza wazi kuwa sekta binafsi ndiyo injini kuu ya ukuaji wa uchumi,huku serikali ikibaki kuwa mwezeshaji kupitia sera bora,sheria rafiki kwa wafanyabiashara na miundombinu imara.
"Dira pia inasisitiza ukuaji jumuishi wa biashara kwa kuhamasisha ushiriki wa wafanyabiashara wadogo,wa kati na wakubwa,na kutoa kipaumbele kwa vijana,wanawake na watu wenye ulemavu,ili kuhakikisha maendeleo yanawafikia Watanzania wote."amesema.
Nakusisitiza kuwa"Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050 inaweka wazi kuwa viwanda imara,biashara yenye ushindani na sekta binafsi yenye nguvu ni nguzo kuu za ustawi wa taifa na msingi wa kujenga uchumi imara,shirikishi na wa kipato cha kati,cha juu."

No comments
Post a Comment