Zinazobamba

*TANESCO YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA MTOA HUDUMA BORA MAONESHO YA MADINI.*


Na Gloria Kalist.

Ruangwa, Lindi

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeibuka mshindi wa kwanza wa tuzo ya utoaji wa huduma bora kwa wateja katika Mkoa wa Lindi kwenye maonesho ya madini (Mining Expo 2025) yaliyofanyika katika viwanja vya maonesho Wilayani Ruangwa.

Tuzo hiyo imekabidhiwa kwa TANESCO na Naibu Waziri wa Madini Mhe. Dkt. Steven Kiruswa katika hafla ya kilele cha maonesho hayo na kupokelewa na Kaimu Meneja wa TANESCO Bw. Theodory Hall.

Maonesho hayo yaliyoandaliwa na Wizara ya Madini, yalianza rasmi Juni 11, 2025 na kuhitimishwa  tarehe 14 Juni, 2025 yalilenga kuwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya madini ikiwemo wachimbaji wadogo na wakubwa, wawekezaji, taasisi za Serikali, taasisi binafsi, watoa huduma pamoja na wananchi.

TANESCO kama mmoja wa washiriki wa maonesho hayo, ilitumia jukwaa hilo kuonesha utekelezaji wa miradi yake ya kimkakati ya uzalishaji na usambazaji wa umeme pamoja na kutoa elimu kuhusu huduma zake kwa wananchi na wadau mbalimbali ikiwemo nishati safi ya umeme ya kupikia.

Maonesho hayo ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuimarisha sekta ya madini na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kupitia ushirikiano kati ya wadau mbalimbali wa sekta hiyo, zikiwemo taasisi zinazotoa huduma muhimu kama TANESCO.

Aidha kupitia ushiriki wake, TANESCO imedhihirisha dhamira yake ya dhati katika kusogeza huduma karibu na wananchi, na kuendelea kuwa mshirika muhimu katika safari ya maendeleo ya uchumi wa Taifa.

No comments