Na Mussa Augustine

Kamati  ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) imeeleza kuridhishwa na mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro.

Akizungumza  leo Machi 27, 2024 Mkoani Mororogoro Mwenyekiti wa Kamati hiyo Deus Sangu baada ya Kamati hiyo kutembelea mradi huo na kushuhudia majaribio ya treni ya mwendokasi kutoka Dar es Salaam hadi mkoani Mororogoro amesema kuwa utekelezaji wa Mradi huo unaridhisha kwa kiwango kikubwa.

"Leo tumeona kazi kubwa imefanyika,tumeridhishwa na mradi huu kwani  umetekelezwa katika viwango vizuri," amesisitiza Sangu mbele ya Waandishi wa habari.

Mwenyekiti huyo wa PIC amesema kuwa mradi huo umetoa fursa  za ajira laki moja na nusu na kwamba mradi wote wa SGR unagharimu shilingi trilioni 23 ambapo hadi sasa asilimia 40 ya fedha hizo zimeshatolewa na Serikali.

Aidha  ametaja faida za mradi huo utakapoanza kufanya kazi,ambapo  ni pamoja na  safari za abiria na mizigo nakwamba itakapoanza kufanya kazi itapunguza nusu ya muda ya ule ambao unatumiwa na mabasi na gharama za kusafirisha mizigo itapungua kwa asilimia 50.

Ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayofanya ya kuendeleza mradi huo kwa kutoa fedha za kuutekeleza.
Kadhalika Sangu amelitaka Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuendelea kusimamia mradi huo ukamilike kwa viwango vizuri na kutunza miundombinu yake.

Hata hivyo  amewataka pia wananchi kutumia fursa ya mradi huo kujikwamua kiuchumi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TRC Masanja Kadogosa amesema kuwa watahakikisha mradi huo unaanza kufanyakazi ifikapo mwishoni mwa mwezi Julai Mwaka huu.

"Tutahakikisha tunakwenda na Muda uliopangwa, hivyo kufikia mwezi julai Mwaka huu Mradi huu kutoka Dar es salaam Morogoro huu utakuwa umekamilika,ndio maana kwa sasa tunafanya majaribio ili kuona wapi bado kuna changamoto"amesema Kadogosa.