LHRC yataja Chanzo cha mauaji yatokanayo na wivu wa mapenzi
Mwandishi wetu
KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimesema chanzo cha mauaji yatokanayo na wivu wa mapenzi kinatokana na migogoro isiyokoma ndani ya ndoa.
Hayo yamebaibishwa leo Mei 31,
2022 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC Wakili Anna Henga
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa mambo kadhaa ya Haki za
Binadamu yaliyojitokeza mwezi Aprili na Mei mwaka 2022.
“Chanzo cha mauaji yatokanayo na
wivu wa mapenzi kinatokana na migogoro isiyokoma ndani ya ndoa licha ya kifungu
cha 102 cha Sheria ya Ndoa No. 29 ya Mwaka 1971 kama ilivyofanyiwa marekebisho
mwaka 2019 kuwa na chombo cha usuluhishi wa migogoro ya ndoa kabla ya Mahakama
kutoa talaka,” amesema Wakili Henga.
Amesema mauaji haya huchangiwa na
ukosefu wa usawa wa kijinsia na kuwepo kwa vitendo vya ukatili baina ya wenza.
Kwamba kwa mujibu wa taarifa ya
haki za Binadamu ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu takwimu zinaonesha
kwamba kimekuwa na ongezeko kubwa la vitendo vya ukatili.
Wakili Henga ameeleza, kwa mwaka
2019 yalikuwa matukio 39,365 mwaka 2020 matukio 42,414 na kwa mwaka 2021
matukio 29,373.
“Katika matukio hayo Wanawake
waliathirika zaidi ambapo katika matukio yote 111,152 Wanawake walikuwa 66139
sawa na asilimia 60,” amesema Wakili Henga.
Aidha ameeleza kuwa mauaji ya
wenza pia yamekuwa yakiripotiwa zaidi ambapo kwa mwaka 2021 taarifa hiyo
iliripoti matukio 35 ya mauaji ya wenza ambapo Wanawake walikuwa 31 sawa na
asilimia 89 huku wanaume wakiwa wanne.
Hivyo amesema vitendo vya ukatili
vimekuwa vikiendelea kuathiri Wanawake zaidi kwamba ndani ya kipindi cha Mei
pekee LHRC imepokea visa saba vya mauaji ya wenza yatokanayo na wivu wa mapenzi
ikiwemo tukio lililotokea Jijini Mwanza hivi karibuni.
Akizungumzia kuhusu mauaji
yatokanayo na wananchi kujichukulia sheria Mkononi, amesema hivi karibuni
kumeibuka wimbi la matukio hayo ambayo yalisababisha vifo 473 kwa mwaka 2021
pekee huku mikoa ya Mwanza, Pwani, Rukwa, Lindi, Songwe na Katavi ikiwa kinara.
Kuhusu ukatili wa kingono dhidi ya
Watoto Henga amesema hivi karibuni kumekuwepo na taarifa za matukio ya Watoto
wadogo kufanyiwa vitendo hivyo vya unyanyasaji wa kingono ikiwemo kibakwa na
kulawitiwa.
Kwamba kwa mujibu wa taarifa ya
haki za Binadamu ya LHRC ya mwaka 2021 matukio 11,499 ya ukatili dhidi ya
Watoto yameripotiwa huku matukio ya kingono yakishamiri zaidi ambapo asilimia
89 ya matukio hayo yalikuwa yakingono na mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Tanga,
Shinyanga, na Mwanza ikiibuka kinara wa matukio hayo.
No comments
Post a Comment