Zinazobamba

KC KIVULE YAADHIMISHA SIKU YA MWANAMKE DUNIANI KWA KUTOA ELIMU YA UKATILI WA KIJINSIA KWA WANAFUNZI WA ABUUY JUMAA SEKONDARI.

Katika kuendelea kuhenzi siku ya Mwanamke duniani ambayo uhadhimishwa kila mwaka ifikapo Machi 8, Kituo cha Taarifa na Maarifa kata ya Kivule kimekutana na wanafunzi wa shule ya sekondari ya Abuuy Jumaa iliyopo ndani ya kata hiyo na kuwapa elimu ya masuala ya kijinsia.

Picha ikionyesha kongamano la maadhimisho ya siku ya wanawake katika shule ya Sekondari Abuuy Jumaa.

Akiongea na mtandao wa full Habari Mwenyekiti wa Kituo hicho Bi. Zahara Omary Mzee amesema kuwa lengo la kituo hicho kuamua kuadhimisha siku hiyo Pamoja na wanafunzi hao, ni kuweza kuwashirikisha mambo mbalimbali yanayohusu Afya, Uchumi Pamoja na elimu ya Ukatili wa kijinsia.

Aidha ameongeza kuwa wanafunzi Zaidi ya 300 wamepata elimu hiyo ambapo kwa upande wa uchumi wameweza kuwafunza jinsi ya kufanya kilimo cha mjini, ambapo mboga uoteshwa kwenye viroba, lakini pia wameweza kuwafundisha namna ya kugeuza taka taka kuwa nishati mbadala ya kupikia na kuokoa gharama za kununua mkaa.

Ameendelea kusema kuwa katika elimu ya ukatili wa kijinsia wamewapa wanafunzi hao mbinu mbalimbali za kukabiliana na ukatili huo, lakini pia njia za kuzuia ukatili usitokee au kutoa taarifa endapo watakabiliwa na vitendo vya aina hiyo.

Na mwisho amelipongeza shirika la TGNP kwa kuweza kuwawezesha kwa kuwapa elimu mbalimbali za ukatili wa kijinsia Pamoja na ujasiriamali ambazo wao kama kituo wamekuwa wakizisambaza kwa watu na makundi mengine ndani ya jamii.

Kwa upande wake Mratibu wa chanjo kutoka hospitali ya Wilaya ya Kivule Dr. Helfrid Mpolo amesema kuwa wamewapa wanafunzi elimu juu ya saratani ya kizazi Pamoja na tezi dume ili wafahamu namna ya kujilinda na kuepuka visababishi vya maradhi hayo.

Ameongeza kuwa kundi lililopo hatarini Zaidi kupata maradhi haya ya Saratani ya Shingo ya mlango wa kizazi ni umri kuanzia miaka 14 na kuendelea na kuwataka Watoto hao kuweza kuacha ngono zembe kwani ni moja ya kisababishi kikubwa cha ugonjwa huu.

Na mwisho ameendelea kuwataka wazazi na walezi kuacha tabia za kuwakataza Watoto kuchoma Chanjo ya Saratani ya shingo ya mlango kizazi kwa kufananisha chanjo hii na ile ya Uviko 19, na kuwahakikishia kuwa chanjo hii haina madhara yotote na ni salama kwa Watoto wao.

Kwa upande wake Mkuu wa shule hiyo ya Abuuy Jumaa Bi. Floida K. Nkya amesema kuwa wao kama uongozi wa shule wamefurahishwa sana na elimu hiyo iliyotolewa shuleni hapo, kwani itawasaidia Watoto wao kuweza kujitambua na kupambana na changamoto mbalimbali za kiafya na ukatili wa kijinsia ndani ya jamii.

Ameendelea kutoa wito kwa wadau na Taasisi zingine kuweza kuiga mfano wa Kituo cha Taarifa na Maarifa Kivule kwa kuweza kushiriki siku ya Wanawake Duniani na Watoto wa shule hiyo ikienda sambamba na elimu nzuri ya kujitambua, na kuendelea kukitaka kituo hicho kiwe na programu za mara kwa mara katika shule hiyo.

Mwenyekiti wa kituo cha Taarifa na Maarifa kata ya Kivule Bi. Zahara Omary Mzee akiongea na Wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Abuuy Jumaa iliyopo Kivule jijini Dar es salaam.
Baadhi ya wajumbe kutoka Kituo cha Taarifa na Maarifa Kivule wakijadili jambo fulani.
Mratibu wa chanjo kutoka hospitali ya Wilaya ya Kivule Dr. Helfrid Mpolo akitoa maelekezo wa wanafunzi namna ya kujikinga na saratani za aina mbalimbali.
Mwanafunzi wa shule ya Abuuy Jumaa akionesha kipeperushi chenye ujumbe katika Maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani yaliyofanywa na KC Kivule shuleni hapo.
Mzee maarufu kata ya Kivule Joseph Gasaya akitoa wosia kwa vijana wa shule ya Sekondari Abuuy Jumaa kuhusu vitendo vya ukatiliwa kijinsia.
Mkuu wa shule ya Abuuy Jumaa Bi. Floida K. Nkya akiongea na wanafunzi wa shule yake kuhusu elimu waliyopewa na wataalamu mbalimbali.
Vijana wa skauti wakionyesha ukakamavu na uzalendo wao kwa wageni na wanafunzi wenzao katika maadhimisho ya siku ya Mwanamke duniani.
Baadhi ya wajumbe wa Kituo cha Taarifa na Maarifa Kivule wakiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi, walimu na wageni waalikwa wengine.


 

No comments