Jaji mkuu amaliza ziara kanda ya songea na kuahidi neema kwa watumishi
Na. Faustine Kapama-Mahakama, Songea.
Jaji Mkuu wa
Tanzania, Mhe. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 3 Machi, 2022 amemaliza ziara yake
ya kikazi ya siku nne ya Mahakama, Kanda ya Songea kwa kutembelea Mahakama ya
Mwanzo Songea, Mahakama ya Wilaya Songea, Mahakama ya Hakimu Mkazi Songea na
Mahakama Kuu Songea kabla ya kuongea na watumishi kwenye kikao cha majumuisho
na kuahidi kuchukua hatua zitakazosaidia kurahisisha utoaji wa haki kwa
wananchi.
Baadhi ya hatua hizo
ni kuzitazama Mahakama za Mwanzo kwa jicho la kipekee kibajeti, kuimarisha
miundombinu mbalimbali katika ngazi zote ikiwemo ujenzi wa majengo ya Mahakama,
hususani Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki na kushughulikia changamoto mbalimbali
zinazowakabili watumishi kwa lengo la kuimarisha ufanisi kazini. Aidha, Mhe.
Prof. Juma amewapongeza watumishi wote katika Kanda hiyo kwa kufanya kazi kwa
bidii, uaminifu na kutoa haki kwa wananchi kwa wakati.
Akiwa katika Mahakama hizo, Jaji MKuu alipokea taarifa za utendaji kutoka kwa Mahakimu Wakazi Wafawidhi, kabla ya kupata taarifa jumuishi iliyotolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea katika Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Sekela Moshi.
Katika taarifa yake
iliyosheheni mambo mengi, Mhe. Moshi amesema, pamoja na mambo mengine, “Mkoa wa
Ruvuma unasimamiwa na Mahakama Kuu moja, Mahakama ya Hakimu Mkazi Songea moja,
Mahakama za Wilaya tano (Songea, Nyasa, Namtumbo, Mbinga na Tunduru) na
Mahakama za Mwanzo 47 katika utekelezaji wa majukumu ya Mahakama katika utoaji
haki kwa wananchi. Kati ya Mahakama za Mwanzo 47, zinazofanya kazi ni 35.”
Akizungumzia
usikilizaji wa mashauri, Jaji Mfawidhi huyo amemweleza Jaji Mkuu kuwa katika
ngazi ya Mahakama Kuu kati ya Januari na Desemba 2021 mashauri 214
yalifunguliwa, mashauri 233 yaliamuliwa na yaliyobaki yalikuwa 94, wakati
katika kipindi cha Januari hadi Februari, 2022 mashauri 23 yamefunguliwa,
yaliyoamuliwa ni 32 na yaliyobaki ni 85.
Amesema katika ngazi
ya Mahakama ya Hakimu Mkazi, kati ya Januari na Desemba mwaka 2021
yalifunguliwa mashauri 32, yaliyoamuliwa yalikuwa 40 na yaliyobaki yalikuwa 36,
ambapo katika kipindi cha Januari na Februari 2022, mashauri
yaliyofunguliwa yalikuwa sita, yaliyoamuliwa ni mashauri nane
na yaliyobaki yalikuwa 34, huku mashauri mawili yakionekana ni ya
mlundikano.
Kwa upande wa Mahakama
za Wilaya, Mhe. Moshi amesema kuwa kati Januari na Desemba mwaka
2021 yalifunguliwa jumla ya mashauri 1,048, yaliyoamuliwa yalikuwa 969 na yale
yaliyobaki ni 479, wakati katika kipindi cha Januari na
Februari 2022, jumla ya mashauri ambayo yamefunguliwa ni 132, yaliyoamuliwa ni
127 na yamebaki mashauri 510.
Hata hivyo, Jaji
Mfawidhi huyo amemweleza Mhe. Prof. Juma kuwa Mahakama Kanda ya Songea ina
mashauri mengi ya uhujumu uchumi kutokana na baadhi ya Wilaya kuzungukwa na
Hifadhi ya Taifa ya Julius Nyerere (zamani ikiitwa Selous Game Reserve) na
kwamba Kanda hiyo inapakana na nchi jirani, jambo linalosababisha wahalifu
kuingia nchini pamoja na mashahidi na washtakiwa kukimbilia kwenye nchi hizo.
“Tumejiwekea mikakati
mbalimbali ya kuhakikisha mashauri ya muda mrefu mahakamani yanaisha na kuzuia
mlundikano (Backstopping). Mikakati hiyo ni usikilizwaji mfululizo na
kuahirisha kwa muda mfupi mashauri yaliyokaa muda mrefu, kuwa
na kikao maalum cha kuondosha mashauri ‘special clean up session’
kila baada miezi miwili,” amesema.
Mhe. Moshi ametaja
mikakati mingine ni kupanga mashauri mengi ya kusikiliza kupitia kwa Majaji
waliopo na Mahakimu wanne wenye mamlaka ya ziada waliopo (extended
jurisdiction), kuwa na vikao vya Kamati za Kusukuma Mashauri ya jinai (Case
Flow Management Meetings) na Kamati za Kusukuma Mashauri ya madai (BenchBar
Management Meetings).
Katika kikao hicho
cha majumuisho, Jaji Mkuu alitoa fursa kwa watumishi wa kada zote kueleza
changamoto zinazowakabili wakati wanapotekeleza majukumu yao ambapo viongozi
walioambatana naye katika ziara yake waliweza kutoa ufafanuzi wa hoja
zilizoibuliwa na kuamsha furaha kutoka kwa watumishi hao mara kwa mara kufuatia
majibu mazuri na ya kina yaliyotolewa.
Kabla ya kutembelea
Mahakama hizo, Mhe. Prof. Juma alitembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
ambapo alipokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mhe. Pololet Mgema na kufanya
naye mazungumzo mafupi. Mkuu huyo wa Wilaya amemhakikishia Jaji Mkuu kuwa
Serikali katika Mkoa huo itaendelea kushirikiana na Mahakama katika kutatua
changamoto mbalimbali zilizopo ili kuharakisha utoaji wa haki kwa wananchi.
Katika ziara yake ya
siku nne, Jaji Mkuu alitembelea maeneo mbalimbali, ikiwemo Wilaya ya Songea,
Mbinga, Nyasa, Namtumbo na Tunduru. Katika maeneo yote aliyopitia, Mhe. Prof.
Juma amekagua shughuli mbalimbali za kimahakama, ujenzi wa miundombinu pamoja
na kuongea na watumishi wa kada zote.
Jaji Mkuu aliambatana
na viongozi mbalimbali kutoka Makao Makuu, wakiwemo Msajili Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma, Msajili wa Mahakama ya rufani, Mhe. Kevin Mhina,
Mtendaji wa Mahakama ya Rufani, Bw. Solanus Nyimbi na Mtendaji wa Mahakama Kuu
ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha.
Wengine ni Mkurugenzi
wa Ukaguzi wa Huduma za Kimahakama, Malalamiko na Maadili, Mhe. Annah Magutu,
Mkurugenzi Msaidizi wa TEHAMA wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Machumu Essaba,
Katibu wa Jaji Mkuu Adrean Kilimi, Katibu wa Msajili Mkuu, Bw. Jovin
Constantine, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bi Beatrice Patrick na
mwakilishi wa Chama Cha Majaji na Mahakimu Tanzania, Mhe. Nemes Mombury.
Kwa upande wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, yupo Jaji Mfawidhi, Mhe. Sekela Moshi, Naibu
Msajili, Mhe. Warsha Ng’umbu, Mtendaji wa Mahakama Kuu wa Kanda,
Bw. Geofrey Mashafi, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Songea,
Mhe. Livin Lyakinana, Afisa Utumishi, Bw. Brian Haule, Mhasibu, Bw. Japhet
Komba na Afisa TEHAMA, Bi. Catherine Francis.
No comments
Post a Comment