2020 ulikuwa ni mwaka wa vilio kwa waislamu?
Ikiwa tunakaribia
kuufunga mwaka 2020 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2021, imeelezwa kuwa jamii ya
kiislamu ilipitia katika wakati mgumu kwa mwaka 2020 hasa baada ya shule zake maarufu
kukubwa na kadhia ya kuungua moto mara kwa mara huku sababu za matukio hayo
yakiwa hazijulikani.
Akitoa
tathmini zake, Mkuu wa shule wa Ilala Islamic Buhero Issa alisema ulikuwa ni
mwaka mgumu ambao hautaweza kusahaulika kwa jamii ya kiislamu kutokana na
sababu kuu mbili, mosi ikiwa ni majanga ya moto lakini pili ni maradhi ya
corona.
Majanga ya
moto yaliathiri wazazi kiuchumi lakini pia kisaikolojia, kubwa la kushukuru ni
kwamba wazazi hawakuyumba waliamini kuwa matatizo yaliyotokea ni kadari na
wameendelea kuziamini shule za Kiislamu.
Licha ya
kwamba majanga ya moto yalileta athari hasi kwa jamii lakini pia ilichangia
kuleta mwamko kwa shule nyingi ikiwemo kuongeza umakini wa kujilinda dhidi ya
majanga hayo
“Kila jambo
lina athari chanya na hasi, faida tunayoiona katika majanga ya moto ni kwamba
jamii imeongeza umakini, hivi sasa shule nyingi zimeongeza walinzi kutoka jeshi
la kujenga taifa (JKT), Walezi wakiume na wakike, zingine zimewekewa camera za
cctv,” alisema
“Nimesikitika
kuona mpaka sasa tunakaribia kufunga mwaka bado hatujaona ripoti ya sababu za
shule kuungua moto, kwetu ripoti zile ni muhimu sana kwa sababu zingetupa
mwanga wa kitu gani cha kufanya ili kadhia kama zile zisiweze kujitokeza tena.
Eneo
jingine ambalo amelitolea tathimini ni suala la maradhi ya corona, alisema
lilikuwa ni janga la kidunia na limeta athari kubwa kiuchumi katika sekta ya
elimu.
Buhero
alisema wazazi wengi walilazimika kubadili mfumo wa ulipaji ada, watoto walikaa
nyumbani muda mrefu sana, mashule mengi yalishindwa kulipa walimu/wafanya
kadhi, kwa hiyo kwa vyovyote vile itaathiri mwaka 2021, maana madeni bado yapo.
Kutokana na
watoto kukaa nyumbani muda mrefu walimu tulilazimika kutumia nguvu kubwa ili kukimbizana
na sylabasi, tarehe za mitihani zilikuwa karibu. Mtoto anarudi shule anakuwa
kama ndio anaanza upya.
Akitoa
ripoti ya Jeshi la Polisi nchini kuhusu matukio mbalimbali yaliyojiri katika
kipindi cha mwaka wa 2020, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi hilo CP
Liberatus Sabas amesema, alitaja sababu za kuungua moto kwa shule nyingi hapa
nchini.
CP Sabas
alisema sababu kubwa zilizopelekea kwa shule nyingi kuungua moto ni pamoja na migogoro
mashuleni, hitilafu za Umeme na uzembe.
Pia Kamanda
Sabas alisema Matukio ya kuungua moto kwa majengo ya shule yalishika kasi kwa
mwaka 2020 huku matukio mengine yakipungua.
Takwimu za
jeshi la polisi zinaonyesha kuwa shule nyingi za watu binafsi au mashirika ya
kidini ndio zimeongoza katika kuungua moto huku shule za serikali nazo
zikiwepo.
“Toka
Januari mpaka Novemba jumla ya shule 31 zimeungua moto huku shule za watu
Binafsi/taasisi za Kidini zikiwa 20 na za Kiserikali zikiwa 11,” alisema
Kamanda Sabas.
Akizungumzia
matukio mengine, Kamanda Sabas alisema ajali za barabarani zimeendelea kupungua
kwa asimia 33.9 ambapo kwa mwaka huu jumla ya watu 1158 walipoteza maisha na
wengine 2089 wakiwa wamepoteza viungo vyao kati ya Januari hadi Novemba 2020,
Kuanzia
Januari hadi Novemba 2020 matukio ya ajali yalikuwa ni 1800, ajali za vifo 935,
waliokufa 1158 na majeruhi 2089, na kwamba kulingana na takwimu hizo mwaka huu
ikilinganishwa na mwaka jana yamepungua matukio 922 ya ajali, sawa na 33.9%,
ajali za vifo 182 sawa na 16.3%, waliokufa 171 sawa na 12.9% na waliojeruhiwa
628 sawa na 23.1%.
Upande wa
unyang’anyi wa kutumia silaha (Ujambazi), Kamishna Sabas amesema, Jeshi la
Polisi kwa mwaka huu limefanikiwa kupunguza makosa ya ujambazi wa kutumia
silaha kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma na mwaka jana.
Amesema,
kuanzia mwezi Januari hadi Novemba (2019) kulikuwa na makosa 378 huku mwaka huu
kuanzia Januari hadi Novemba (2020) yamepatikana makosa 273 ya kutumia silaha
hii ikiwa ni tofauti ya makosa 105 sawa na asilimia 27.
Kuhusu
mauaji, Kamishna Sabas amesema, kwa kiasi kikubwa mauaji yanayotokea kwa sasa
nchini yanatokana na wivu wa mapenzi na wananchi kujichukulia sheria mkononi.
Amesema,
kutokana na hali hiyo Jeshi la Polisi limefanikiwa kutoa elimu kwa wananchi
kutokujichukulia sheria mkononi huku likiwataka viongozi wa dini kuingilia kati
katika kutoa elimu ili kusaidia kupunguza mauaji yatokanayo na wivu wa mapenzi
kwani wengi ni waumini wa madhebu yao na wanawasikiliza sana.
Kamishna
Sabas alisema mwaka 2020 kulikuwa na
wimbi kubwa la watoto kuacha shule na kwenda kujiunga na makundi ya kihalifu,
miongoni mwa waalifu hao ni wale waliokuwa Kibiti na hatimae baada ya kupigwa
na Jeshi la Polisi kwa kushilikiana na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama
walikimbilia nchi jirani ya Msumbiji.
Hadi sasa
wapo wanafunzi waliokuwa wameacha shule na kujiunga na vikundi vya kihalifu
ambao wamekamatwa wakiwa wanavuka kuelekea nchini Msumbiji na wengine tayari
wameishafanikiwa kuvuka kuingia nchini humo.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni