Wanawake wa Kiislamu wafundwa Dar
Na Bint Ally Ahmed
Amesema Allah (S.W) Enyi wanadamu hakika mimi nimewateremshia nguo, ili kwa nguo hizo muweze kusitiri miili yenu na mapambo na vazi hilo la ucha Mungu ndio bora.
Lengo la Allah kuwaletea mwanadamu vazi ni kustiri tupu na kumtofautisha na mnyama. Lakini pia ni pambo avae mwanadamu, ili apambe mwili wake, avutie, aonekane uzuri wake wa asili aliopewa na Mola wake.
Ukht. Fatma Musa Mdidi, alinukuu aya hiyo na kutoa ufafanuzi wakati akitoa mada yake juu ya vazi la stara kwa mabinti, katika kongamano la wanawake lililoandaliwa na TAMSIYA na kufanyika Chuo Kikuu cha Ualimu DUCE, Chang`ombe jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Ukht. Fatma alisisitiza kuwa wanawake ni muhimu sana kujua stara ya kisheria wanayotakiwa kuivaa ili kupata radhi za Mola wao.
Hata hivyo alisema Mwenyezi Mungu alizungumzia vazi la stara kama sehemu tu katika stara, kwani stara imebeba vitu vingi.
Aliongeza kuwa mwanamke anapovaa vazi sahihi la hijabu ni dalili ya utii kwa Muumba, kwani anakuwa ameonyesha utiifu mkubwa kwa Mola wake, lakini pia anakuwa amekubali na kufuata mafundisho yake.
Aliongeza kuwa vazi la stara pia ni kinga juu ya ngozi na ulinzi kutokana na miale mikali ya jua, vumbi na kubaki katika uzuri wa asili, lakini pia ni kinga juu ya macho ya watu.
Akiendelea kuchambua vazi la stara, Ukht. Fatma ameeleza kuwa mwanamke kujistiri kunamtwaharisha moyo wake kutokana na mambo maovu.
Alisema Mtume (s.a.w) anasema mwanamke yeyote ambaye hachungi vazi la stara, anakuwa amekiuka sharia na taratibu za dini yake hivyo anaenda kinyume na kufanya hivyo ni chukizo mbele ya Mola wake.
Kwa upande wa Ukht. Mwajabu Mbwambo, akiwasilisha mada juu ya nafasi ya mwanamke katika jamii, alisema mwanamke ana haki ya kupata elimu, ana haki ya kumiliki mali na vyote vinavyoendana na uchumi.
Ukht Mwajabu alisema haki ya kwanza kwa mwanamke ni usawa baina ya mwanamke na mwaname, katika kutimiza majukumu yao katika maisha na malezi.
Haki nyingine ni mtoto wa kike baada ya kuujua Uislamu, ana haki ya kuolewa na mwanaume anaye mpenda kwa kufuata sharia kanuni na za dini.
Alitaja haki nyingine ya mwanamke ni kuweza kumuacha mwanamme ambaye hawezi kutekeleza mambo yake ya ndani.
Lakini pia alielezea juu ya haki ya mwanamke kushiriki katika mambo ya siasa madhali tu, hatoki nje ya mipaka ya dini.
Mwanamke apewa haki ya kumiliki mali na uchumi. Mfano mzuri ni Bi. Khadija, Mke wa Mtume ambaye alitumia mali zake kuisimamia dini.
“Mwanamke ana uhuru wa kutafuta elimu na tumeambiwa na Mtume (s.a.w) tutafute elimu bila kubagua jinsia zetu. Hadithi hii haijaainisha elimu hii ni kwa mwanaume au mwanamke. Mwanamke amepewa haki ya kufanya kazi muhimu, pia kazi iwe sio ya kumdhalilisha. alifafanua zaidi Bi. Mwajabu.
Alisema mwanamke amepewa haki ya kuheshimiwa, hata kama mwanamke huko nyuma alikuwa na maovu mengine, hivyo anatakiwa asitiriwe kwa maovu aliyoyafanya huko nyuma.
Aidha alisema mwanamke anapaswa kushirikishwa katika mambo ya familia na katika jamii pia na kwamba, ana haki ya kuthaminiwa na kushauriwa na amepewa haki ya kufanyiwa uadilifu.
Ukht. Mwajabu amewataka wanawake wazitambue nafasi zao, wajue thamani yao na waitumie vyema nafasi hiyo, ili kuileta familia katika msingi ulio bora zaidi.
Lakini pia amesema kuwa mwanamke ndio kiigizo chema kwa watoto wake. Kwamba mama ambaye ndiye mlezi mkubwa wa watoto akiwa mtu mzuri na watoto wataiga tabia nzuri ya mama yao.
Akiwa ni kinyume chake pia matokeo yatakuwa vivyo hivyo kinyume.
Hivyo akina mama wakaaswa wajitahidi kuwa na tabia njema, ili watoto wao waige kitu kilicho bora kutoka kwao.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni