NAIBU WAZIRI GEKUL NA MAFANIKIO YA WUSM
Adeladius Makwega
Dodoma-WUSM.
JUMAMOSI ya Novemba 13, 2021 Mheshimiwa Innocent Bashungwa Waziri
wa Utamaduni, Sanaa na Michezo aliwakilishwa na Naibu wake Bi Pauline Gekul kuzungumza na wanabari juu ya wizara
hii yenye sekta kongwe tatu ambazo zilikuwepo tangu Serikali ya Awamu ya Kwanza
wakati wa Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961 chini ya Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere licha ya kuwa sekta hizo zimekuwa zikiwekwa katika wizara mbalimbali.
Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliwahi kusema, “Utamaduni ni kiini
ama roho ya taifa lolote, taifa lisilo na utamaduni ni sawa na mkusanyiko wa
watu wasio na roho.”
Wizara hii tangu Uhuru mwaka 1961 imekuwa kinara wa kusimamia na
kuhakikisha taifa linaendelea kuenzi utamaduni imara wa Mtanzania, kuwa na kazi
bora za sanaa na taifa lenye umahiri mkubwa katika michezo. Mwaka 1962 Serikali
ya Kwanza iliunda Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana hatua inayodhihirisha
kuwa ni sekta nyeti na muhimu katika kusimamia masuala ya utamaduni wa nchi.
Wizara hii inaundwa na sekta tatu ambazo ni Utamaduni, Sanaa na
Michezo, akizungumza na vyombo vya habari Jijini Dodoma Waziri Bashungwa
ameyataja baadhi ya mafanikio ya sekta zote tatu ambayo amebanisha kuwa
yameliweka taifa letu katika ramani ya dunia.
Katika sekta ya Utamaduni; “Matumizi ya Kiswahili katika maendeleo
ya teknolojia, tunapozungumzia mafanikio ya Kiswahili hatuna budi kuzungumzia
mafanikio yake katika uga wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Kampuni ya Microsoft na Linux zimetayarisha programu za kompyuta kwa lugha za
Kiafrika, Kiswahili kikiwamo. Programu hizi zitajenga ushirika wa kibiashara na
kuwawezesha Waafrika wakiwamo Waswahili kutumia kompyuta katika kazi zao za
kila siku. Mathalani, hivi sasa
watumiaji wa programu za Microsoft wataweza kupata nakala za Microsoft Windows,
Office, Windows Vista, Windows XP, Office 2003, Office Standard, Edition 2007,
Word, Excel, Powerpoint na Outlook. Matumizi ya Kiswahili katika kompyuta
yameongeza msamiati wa Kiswahili katika uwanja wa Kompyuta.”
Mafanikio mengine ni kuwa kwa sasa Kiswahili kinatumika katika
mitandao ya simu na kwenye mashine za kutolea fedha (ATM) za Benki mbalimbali.
Pia, Kiswahili kinatumika katika baadhi ya ndege zinazotoa huduma katika nchi
za Afrika Mashariki.
Tatu ni kupatikana kwa huduma za ukalimani, tafsiri na ithibati.
Tanzania imewezesha lugha mbalimbali za kimataifa kutafsiriwa na kufanyiwa
ukalimani kwa Kiswahili. Kutolewa kwa huduma hii kumewezesha ujumbe na maarifa
yaliyomo katika lugha hizo kuwafikia wananchi kwa Kiswahili. Baadhi ya lugha
hizo ni Kiingereza, Kifaransa, Kigiriki, Kicheki, Kireno, Kirusi, Kichina,
Kijapani, Kituruki, Kiarabu, Kipolishi, Kihispaniola, Kiitaliano, Kilatini,
Kijerumani, Kidachi, Kikoatia, Kisebu, Kibulgaria, Kinorwei, Kidenishi na
Kiswidi. Aidha, nyaraka mbalimbali za Kiswahili vikiwamo vitabu vya kiada na
ziada vinavyotumika katika ngazi mbalimbali za elimu vimepata ithibati ya
matumizi ya lugha. Mafaniko yanayotokana
na kazi hii kuwapo kwa ufasaha na usanifu katika mafunzo ya ngazi mbalimbali za
elimu zinazotumia Kiswahili.
Mh.Gekul hakuishia hapo, alitaja mafanikio mengine katika sekta
hii ya utamaduni ni kuanzishwa kwa programu maalum ya kuenzi historia ya
ukombozi wa nchi yetu. Mwaka 2011 Umoja wa Afrika uliridhia Programu ya Urithi
wa Ukombozi wa Bara la Afrika kutekelezwa nchini. Programu hii inalengo la
kutambua, kuhifadhi na kuendeleza urithi wa ukombozi uliotokana na mapambano ya
kufauta uhuru. Aidha, inalenga kuenzi watu walishiriki katika vita vya ukombozi
kwa kujenga minara ya kumbukumbu na kuandika upya historia ya ukombozi wa nchi
yetu na kurithisha kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Tano ni kuanzishwa kwa vituo mbalimbali vya Kiutamaduni (Cultural
centers) nchini. Vituo hivi vimeendelea kutumika kwa ajili ya uendeshaji wa
shughuli za utamaduni ikiwemo matamasha ya utamaduni ili kuwawezesha wananchi
waendelee kujivunia na kusherehekea Utamaduni wao pamoja na kuuza kazi za
mikono za kiutamaduni (cultural handcrafts) kwa minajili ya kujipatia
mapato.Hayo ni baadhi tu ya mafanikio zaidi ya 20 na ushehe ya sekta hiyo.
Wizara hii imetaja mafanikio ya sekta ya sanaa tangu kupatikana
kwa Uhuru wa iliyokuwa Tanganyika .
“Kuanzishwa kwa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ambapo Mwaka
1984 Serikali ilitunga Sheria ya Baraza la Sanaa la Taifa Nambari. 23 ambayo
ilianzisha Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA). Pamoja na majukumu mengine
husajili Wasanii, kutoa vibali vya shughuli za sanaa, kuwatetea wasajiliwa
wake, kuwatafutia masoko ya kazi zao na kusimamia uanzishwaji wa mashirikisho
ya sanaa nchini. Kuwepo kwa baraza hili kumeifanya sekta ya sanaa kushamiri
hadi kufikia sekta kuongoza katika ukuaji kwa mwaka 2018/2019 kwa asilimia
13.7. “
Pili, kuanzishwa kwa taasisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) mwaka
1999 kwa Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki Namba 7 ambapo pamoja na mambo
mengine huwalinda na kuwatetea wabunifu dhidi ya matendo ya uharamia na
kusaidia kukusanya mirabaha itokanayo na matumizi ya kazi zao.
Tatu, Ongezeko la ajira kupitia sekta ya sanaa nchini, ambapo
kufikia Novemba 2017; Zaidi watu milioni 5.5 walikuwa wameajiliwa kupitia sekta
ya Sanaa.
Nne, mafanikio mengine ni uanzishwa kwa Taasisi ya Sanaa na
Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) ambayo ni Kituo kilichotukuka Afrika Mashariki
katika mafunzo ya sanaa na utamaduni.
Historia ya chuo cha Sanaa Bagamoyo ilianzia mnamo mwaka 1962
ambapo kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanganyika iliundwa Utamaduni wa
Taifa na Vijana.
Mheshimiwa Gekul pia alitazama mafanikio ya sekta ya michezo
ambapo alibainisha kuwa Tanzania imefanikiwa kupata jumla ya Medali 16 katika
michezo mikubwa kabisa duniani ambayo ni ya Olympic (2), Jumuiya ya Madola (7)
na Michezo ya Bara la Afrika (7) na kwamba timu zetu zimeshiriki katika michezo
hii mikubwa bila kukosa tangu tupate uhuru wetu.
Pili, Tanzania imefanikiwa kuwa na wachezaji wakulipwa katika nchi
mbalimbali tangu uhuru, kwa sasa inajumla ya wachezaji 54 wakulipwa katika nchi
mbalimbali ambapo (28) ni wachezaji wa mpira wa miguu, (16) mpira wa kikapu,
(4) mpira wa wavu, (2) Kabbadi, (2) Netiboli (1) kuogelea na (1) mchezo wa
Roliball.
Tatu, Tanzania imeshinda vikombe mbalimbali katika mashindano ya
kimataifa tangu kupata uhuru wake ambapo kwa upande wa mpira wa miguu kwa
wanawake Tanzania imechukua vikombe vitano (5) katika mashindano mbalimbali ya
kimataifa ikiwa ni pamoja na COSAFA, EAst Afriaca, CECAFA. Aidha kwa upande wa
mpira wa miguu kwa wanaume timu zetu zimefuzu kushiriki kwenye mashindano
mbalimbali ambapo Taifa stars imefuzu mara 2 kushikiri fainali za kombe la
Afrika AFCON 1980 na 2019 vile fainali za mashindano ya wachezaji wa ndani CHAN
mara mbili.
Nne, Wanawake hawakuwa wanashiriki katika baadhi ya michezo kabla
ya uhuru lakini sasa kumekuwa na ongezekzo kubwa kushiriki katika michezo
mathalan mpira wa miguu ambapo sasa ligi ya mchezo huo imeanzishwa na Timu za
Taaifa za mchezo huo zimeundwa.
Tano, Watalaam wa michezo wameongezeka kwa kuongeza udahili katika
vyuo vinavyo fundisha fani ya michezo ikiwa ni pamoja na Chuo cha Maendeleo
Malya na Chuo Kikuu cha Dar es salaam. Malya kilidahili wanafunzi 40 mwaka 2013
hadi na kufikia wanafunzi 137 mwaka 2020. Aidha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
kilidahili wanafunzi 14 mwaka 1997 hadi kufikia wanafunzi 105 mwaka 2020.
Sita, Kwa upande wa mchezo wa ngumi pia kumekuwa na mafanikio
makubwa ambapo mabondia wetu wameshinda katika mapambano mbalimbali na
kujinyakulia ubingwa wa Bara la Afrika, mabara mengine na dunia, baadhi ya
mabondia hao ni pamoja na Hassan Mwakinyo ambaye ni bingwa wa uzito
walterweight, Bruno Melchony aliyenyakua mkanda wa International Super
Featherweight, Tony Rashid mkanda wa Super Bantaman, Abdalah Shaban Pazi mkanda
wa Asia Pacific Superweight na Salin Jengo world Supe featherweight.
Saba, Kwenye michezo ya walemavu, Tanzania ilishiriki katika
mashindano mbalimbali ya kimataifa, mathalan mwaka 2015 ilishiriki katika
mashindano ya Special Olympics yaliofanyika Los Angeles Marekani. Pia kwenye
mchezo wa riadha Tanzania ilifanikiwa kupata jumla ya medali 10 (Dhahabu 3,
Fedha 4 na Shaba 3).
Nane, Mwaka 2019 Tanzania
imeshiriki mashindano ya special Olympic yaliyofanyika Abu-Dhabi na Tanzania
kupata jumla ya medali 16 katika mashindano ya Riadha (12 Dhahabu, 1 Fedha na 2
Shaba) mwaka 2020 Tanzania imeshiriki Special Olympic iliofanyika Misri na
Tanzania kupata medali 11 (Dhahabu 6, Fedha 3, na Shaba 2). Timu ya mpira wa
miguu kwa watu wenye ukemavu kwa mara ya kwanza walishiriki mashindano ya Bara
la Afika kwa michezo hiyo na kushika nafasi ya 4.
Akihitimisha kuyaeleza mafanikio hayo yaliyosomwa na Naibu Waziri
wa Utamaduni Sanaa na Michezo Bi Pauline Gekul kwa niaba ya Waziri wake
Innocent Bashungwa alimshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bi
Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwapa ushirikiano na kuwaamini.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni