Rais Samia: Michezo Inakuza Jina la Nchi Yetu
Na. Paschal Dotto-MAELEZO
Rais wa Jamahuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Samia Suluhu Hassan ameiagiza Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo
kuhakikisha maandalizi ya kushiriki Mashindano ya Jumuiya ya Madola
yatakayofanyika mwaka 2022, Jijini Birmigham Nchini Uingereza yakamilike mapema
kwa kuchagua wanamichezo wenye weledi na ushindani mkubwa.
Akizungumza katika Hafla ya Mapokezi ya
Kifimbo cha Malkia Yaliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, Rais Samia amesema
kuwa michezo inaleta heshima na kukuza jina la Tanzania kwani ushiriki wa Watanzania
katika Michezo hiyo umekuwa ukionekana
vizuri.
“Katika Michuano hii, nakumbuka kaka yetu,
Titus Simba alipambana katika hali ngumu na alifanikiwa kutuletea medali ya
kwanza ya dhahabu baada ya kumshinda mpinzani wake John Conte, lakini mwaka
1974 Filbert Bay pia alituheshimisha kwa kutulea medali ya dhahabu na
kuitangaza nchi yetu, hii inafanya nchi yetu kujulikana duniani huko”, Rais
Samia.
Rais Samia alisema kuwa vyama mbalimbali
nchini vimeanza maandalizi ya kushiriki Mashindano ya Madola mwaka 2022, na
hapa akaigiza Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo kusimamia kikamilifu
maandalizi hayo ili Tanzania iweze kurejesha heshima yake ya kutwaa medali
katika michezo mbalimbali kama ilivyokuwa hapo awali.
Aidha, Rais Samia alieleza na kutambua
ushiriki wa Tanzania katika Michezo hiyo kwani Tanzania imekuwa mshiriki mzuri
ambapo mpaka sasa ina medali 21 katika michezo mbalimbali zikiwemo sita za
dhahabu (6), sita za Fedha (6) na tisa za shaba (9).
“Natambua Tanzania katika Michezo ya
Jumuiya ya madola haijawahi kurudi bila kupata medali tangu tuanze kushiriki,
isipokua miaka mitatu, 2010, 2014, 2018,
hii inamaana kwamba leo siyo tu tunapokea kifimbo, lakini pia ni wakati wa
kilitafakari hili, kifimbo hiki sasa iwe kama kengele tunapigiwa kinakuja kitu
tujitayarishe kwa hiyo twende tukajitayarishe vizuri”, Rais Samia.
Rais Samia amewataka Watanzania kuiunga
mkono timu ya taifa katika mchezo wake dhidi ya Madagascar kufuzu kucheza
michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2022 nchini Qatar, amesema Watanzania wasife
moyo kwani Timu ina nafasi ya kushinda.
Pia alimpongeza Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa, Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, TFF na Wadau wa Michezo kwa
kuonyesha ari na hamasa kubwa wakati wa maandalizi ya mchezo wa Taifa Stars na
Timu ya Taifa ya DRC Congo ambapo Tanzania ilipoteza mchezo huo.
Kwa upande wake Waziri wa Sanaa, Utamaduni
na Michezo, Mhe. Innocent Bashungwa amesema kuwa Wizara iko tayari kuhakikisha
washiriki wa Michezo ya Jumuiya ya madola mwaka 2022 wanashiriki michuano hiyo
vizuri.
“Nikushukuru Mhe. Rais kwa kuendelea
kutuheshimisha sisi wanamichezo na leo tena tuko hapa nikuhakikishie wasaidizi
wako katika sekta ya michezo tayari tumeshachukua hatua za kuimarisha sekta hii
ili kuweza kuwa na wachezaji mahiri wengi watakao tuwakilisha katika mashindano
mbalimbali ya kimataifa yakiwemo haya ya
Jumuiya ya Madola.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni