Waziri Mkuu Majaliwa kufungua Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Uingereza
Isack Magesa
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anatarajia
kufungua Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Uingereza litakalofanyika
Novemba 16 mwaka huu katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano wa Mwalimu Julius
Nyerere, Dar es Salaam.
Balozi wa Uingereza nchini Tanzania David William Concar akizungumza na waandishi wa habari (hawamo pichani,) kuhusu kongamano hilo.
Hayo yamesemwa leo jijini humo na Waziri wa
Viwanda na Biashara Profesa Kitila Mkumbo wakati akizungumza na wanahabari
kuhusu kongamano hilo.
Amesema kuwa kongamano hilo litafunguliwa na
Waziri Mkuu Majaliwa na kuhudhuriwa na Mjumbe Maalumu wa Uingereza wa Masuala
ya Biashara wa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Lord Walney na kwamba washiriki
takribani 200 kutoka Sekta Binafsi za nchi mbili watahudhuria huku wengine
watashiriki kwa njia ya mtandao.
"Kongamano hili limeandaliwa kwa namna ya
kipekee ili kuongeza tija ya matokeo tarajiwa ambapo limegawanyika katika
makundi matatu yatakayofanya mijadala kwa wakati mmoja, yaani majadiliano kati
ya Serikali ya Tanzania na ya Uingereza, baina ya sekta binafsi ya nchi hizo
mbili pamoja na mdahalo kati ya Serikali na sekta hiyo," amesema Waziri Profesa
Mkumbo.
Amebainisha kuwa kauli mbiu ya kongamano hilo
ni Kuimarisha Ustawi Endelevu wa Kiuchumi kati ya Tanzania na Uingereza, hivyo
litatoa fursa kwa washiriki kujadiliana kwa kina na kubaini fursa mpya za
ushirikiano baina nchi hizo mbili.
Amesisitiza kuwa kupitia majadilainao hayo
pande zote mbili zitaweza kupanua zaidi wigo wa ushirikiano katika maeneo ya
biashara na uwekezaji hususan sekta za nishati, madini, miundombinu, kilimo,
uchumi wa bluu na utalii.
Ameongeza kuwa kwa mujibu wa takwimu za Kituo
cha Uwekezaji nchini (TIC) Nchi ya Uingereza ni ya pili kwa uwekezaji hapa
nchini ikiwa na miradi 945 yenye thamani ya Dola za Marekani 5.42 bilioni
na kutoa ajira 275,384.
Pia amesema kuwa takwimu za Serikali ya
Uingereza jumla ya thamani ya biashara baina ya nchi hizi mbili kwa mwaka 2021
ilikuwa pauni za Uingereza 156 milioni, huku nchi hiyo ikiuza hapa nchini
bidhaa zenye thamani ya Pauni 127 milioni, na Tanzania ikiuza Uingereza bidhaa
zenye thamani ya Pauni milioni 29.
Kwa upande wake, Balozi wa Uingereza nchini,
David Concar amesema kongamano lina umuhimu kwa nchi zote kwani linakwenda
kufungua fursa mpya za uwekezaji zilizopo.
Balozi huyo amesema katika kongamano hilo
kutakuwa majadiliano baina ya Serikali ya Tanzania na UIngereza, sekta binafsi
pamoja wawkilishi wa makampuni hivyo fursa mbalimbali za uwekezaji
zitajadiliwa.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni