NATAMANI KUMTENGENEZEA RAIS SAMIA MIWANI
Adeladius
Makwega
Siku
moja nilipokuwa natoka nyumbani kwangu huko kwa akina yakhe nilipata usafiri wa
haraka wa kwenda kwa akina pangu pakavu tia mchuzi, nilipoingia katika daladala
nilikaa jirani na mama mmoja ambaye alikuwa na wajihi unaofanana sana na Mheshimiwa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bi Samia Suluhu Hassan. Ama kweli
duniani wawili wawili.
Nilimpenda sana mama huyu namna alivyokuwa akizungumza, kwani nadhani alikuwa akitokea Zanzibar. Nilivutiwa sana na mama huyu kwani alikuwa amependeza sana na miwani yake ilikuwa na rangi nyeusi.
Miwani
ile ilifanya aonekane amependeza mno, nikasema kwa hakika na mimi nitaweka oda
na mimi nitengenezewe miwani kama hiyo.
Nikiwa
nimeketi katika kiti cha mbele cha dereva na mama huyu akiwa kiti cha dirishani
nilimwambia umependeza sana alicheka tu na mwisho alisema asante. Akaniuliza
kitu gani kilichokuvutia mno, nikamjibu kuwa haswa hiyo miwani. Alitabasamu
huku safari yetu ikiendelea.
Nilimuuliza
hiyo ni miwani ya macho au ya urembo? Alinijibu kuwa yeye anavaa miwani ya aina
mbili nayo ni ya urembo na pia anayo ya kuona mbali. Nilimuuliza kumbe hivyo
ndiyo ilivyo kwa wote wanaovaa miwani? Alinijibu kuwa ni kweli. Nikamuuliza
kumbe hata waheshimiwa wengi wanavaa miwani kumbe mingine ya urembo na mingine
ya macho? alinijibu kuwa ni kweli kabisa.
Kumbuka
tupo katika daladala na hayo mazungumzo yanapamba moto huku dereva
akitusikiliza kwa makini akidhani kuwa mie na huyu mama tunafahamiana kumbe
wala, ilinijia picha ya uvaaji wa miwani ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu,
Marehemu Magufuli alikuwa akivaa miwani, na hata Mheshimiwa Rais Jakaya
Kikwete, Marehemu Rais Benjamin Mkapa, Mheshimiwa Rais Ali Hassani Mwinyi na
Marehemu Rais Julius Nyerere.(haya niliyafikiri kwa sekunde kadhaa) Alafu
nikamwambia huyu mama kumbe mnaovaa miwani mnaona karibu na mbali vizuri sana.
Akasema
ehh! tunaona karibu na mbali vizuri sana, wewe uoni Mheshimiwa Samia anavaa
miwani anaona kote vizuri sana. Alipoyasema haya kama aliingia katika akili
yangu kile nilichokuwa nakifikiria.
Nikamwambia
kumbe, ngoja nimnunulie zawadi ya miwani Mheshimwa Rais Samia Suluhu miwani
mizuri sana, miwani imara, miwani ya kudumu. Mama huyu alicheka sana, akasema
wewe unataka kumchokoa pweza. Nikamjibu hapana nampa kama zawadi Mheshimiwa
wetu. Nikamwambia miwani hii itakuwa na mishikio iliyotengenezwa kwa mti wa
mpingo. Mti huu wa mpingo utakuwa umeshikilia miwani yote tangu flemu zake hadi
mishikio, sifa yake kubwa hata ikiangushwa haitoweza kuvunjika.
Mama
huyu alicheka akasema kuwa haiwezi kumuumiza Mheshimiwa? Nilijibu kuwa
itatengenezwa vizuri sana na haiwezi kumletea madhara Mheshimiwa.
Miwani
yangu hii itakuwa na lenzi mbili yaani lenzi mbonyeo ya kuona mbali na ile lenzi
mbinuko ya kuona karibu. Pale atakapotaka kuona karibu ataweza kuiona karibu
kwa haraka na hata akitaka kuona mbali ataweza kufanya hivyo kwa haraka kwa
kutumia kipachiko chake maalumu kuruhusu hali anayotaka kwa wakati husika.
Mama
huyu aliniambia kweli hiyo miwani yako itakuwa hatari, nikasema itakuwa maalumu
kwa ajili ya Mheshimiwa Rais tu. Miwani yangu hii itafungwa na kamba maalumu ya
iliyotengenezwa kwa ngozi laini lakini imara ya twiga ili Mheshimiwa
akiining’iniza haitoweza kuanguka. Mama huyu alicheka na kasema kwanini
usitengeneze kwa ngozi ya mnyama mwingine nilimjibu kuwa nampenda sana twiga
huwa hana papara na miwani hiyo itamuwezesha Mheshimiwa kuona bila papara.
Nilimwambia mama huyu kuwa nitamtengenezea pia mkebe mzuri uliotengenezwa kwa
mpingo ambapo utatumika kuhifadhi miwani hiyo.
Nikaulizwa
ehh, hiyo miwani itamfikiaje Mheshimiwa? Ah dereva wa daladala aliingilia kati
akasema kaka hiyo miwani yako itakuwa tabu mno kumfikia mheshimiwa. Mama huyu
akasema nitakupa namba yangu ukishatengeneza nitampatia. Mama huyu ambaye
alikuwa abiria mwezangu akasema kuwa mie nitamsubiria Mheshimiwa akienda kwetu
Zanzibar akiwa anatoka msikitini nitamsalimia nitamkabidhi zawadi hiyo ya
miwani.
Miwani
yangu hii itakuwa na sharti moja tu hakuna atakayeruhusiwa kuijaribu isipokuwa
yeye mwenyewe tu. Nilimuuliza mama huyu je miwani yangu itafika salama kwa Mheshimiwa
na kuelezwa masharti ya miwani hii? Dereva wa daladala hii alisema kuwa kama
mama huyu namna alivyo nina hakika kuwa akikabidhiwa miwani hiyo itamfikia Mheshimiwa
salama salimini.
Mara
daladala yetu ilizimika gafla dereva akasema kuwa gari imeishiwa mafuta kwa
hiyo konda alishuka na kidumu cha lita tano ili akachuke mafuta na mie
nilichukua namba ya simu ya mama huyu na
kuondoka zangu kwenda huko madongo poromoka na kuwaacha abiria wengine, yule
mama na dereva wakimgonja konda arudi na mafuta ili waendelee na safari.
Kwa
hiyo kwa sasa nipo katika kazi yangu ya kuitengeneza miwani hiyo
itakapokamilika nitawasiliana na mama huyu ambaye alikuwa abiria mwenzangu
niliyekutana naye katika daladala hiyo ili nikamilishe zoezi langu.
0717649257
Hakuna maoni
Chapisha Maoni