Kongamano la biashara kati ya Uingereza na Tanzania kufanyika Dar kesho
Tanzania inataraji kufanya Kongamano la kibiashara baina yake na Nchi
ya Uingereza hapo kesho dhamira ikiwa kuendeleza mahusiano makubwa yaliopo kati
ya nchi hizo mbili.
Kongamano hilo litafanyika
kwa mara ya kwanza jijini Dar es Salaam ambapo mada mbalimbali zitazungumzwa
huku Tanzania ikipanga kupigia debe biashara ya nyama ambayo bado haina soko la
kutosha nje ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri wa
biashara na viwanda Prof. Kitila Mkumbo
amesema kwa mujibu wa takwimu za Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) Nchi
ya Uingereza ni ya pili kwa uwekezaji ikiwa na miradi 945 yenye thamani ya Dola
za Marekani 5.42 bilioni na kutoa ajira 275,384.
Aidha takwimu za Serikali ya Uingereza zinaonyesha
jumla ya thamani ya biashara baina ya nchi hizi mbili kwa mwaka 2021 ilikuwa ni
pauni za Uingereza 156 milioni, huku nchi hiyo ikiuza hapa nchini bidhaa zenye
thamani ya Pauni 127 milioni, na Tanzania ikiuza Uingereza bidhaa zenye thamani
ya Pauni milioni 29.
Kwa upande wake, Balozi wa Uingereza nchini,
David Concar amesema kongamano hilo lina umuhimu kwa nchi zote kwani linakwenda
kufungua fursa mpya za uwekezaji zilizopo.
Kongmano hilo limeratibiwa na Wizara ya Viwanda na Biashara kwa
kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Ubalozi wa Uingereza hapa
nchini pamoja na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).
Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Uingereza (Tanzania - UK
Business Forum) litarajiwa kufanyika Novemba 16, 2021 katika Kituo cha
Kimataifa cha Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.
Kongamano hilo litafunguliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.), na kuhudhuriwa pia na Mjumbe
Maalumu wa masuala ya Biashara wa Waziri Mkuu wa Uingereza, Bw. Lord John
Walney. Aidha, washiriki takriban 200 kutoka Serikali na Sekta Binafsi za nchi hizi
mbili watahudhuria Kongamano hilo na
wengine wengi zaidi watashiriki kwa njia ya mtandao (virtually).
Kongamano hilo ambalo limeandaliwa kwa namna ya kipekee
linatarajiwa kuwa na makundi matatu yatakayofanya mijadala kwa wakati mmoja,
yaani, majadiliano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Uingereza
(Government to Government-G2G), majadiliano baina ya Sekta Binafsi ya Tanzania
na Sekta Binafsi ya Uingereza (Business to Business-B2B) pamoja na mdahalo kati
ya Serikali na Sekta Binafsi (Government to Business-G2B).
Kauli mbiu ya Kongamano hilo ni "Kuimarisha Ustawi Endelevu
wa Kiuchumi kati ya Tanzania na Uingereza" (Strengthening Mutual
Sustainable Economic Prosperity).
Pamoja na mambo mengine, inatarajiwa kuwa Kongamano hilo litatoa
fursa kwa washiriki kujadiliana kwa kina na kubaini fursa mpya za ushirikiano
baina ya nchi hizi mbili.
Aidha, kupitia majadiliano
hayo, pande zote mbili zitaweza kupanua zaidi wigo wa ushirikiano katika maeneo
ya biashara na uwekezaji – hususan katika sekta za nishati, madini,
miundombinu, kilimo, uchumi wa buluu na utalii.
Inatarajiwa pia kupitia
Kongamano hilo, changamoto mbalimbali za kisera zilizokuwa zikiwakabili
wawekezaji kutoka Uingereza zitajadiliwa na kutafutiwa ufumbuzi.
Nchi ya Tanzania na
Uingereza zina mahusiano ya karibu ya muda mrefu ambayo yamekuwa yakiimarika
siku hadi siku kutokana na mashauriano ya mara kwa mara baina ya Serikali za
pande zote mbili.
Hivyo, Kongamano hili linalenga, pamoja na mambo mengine, kujadili
na kuridhia mikakati ya pamoja itakayolenga kupunguza pengo hilo kubwa la urari
wa biashara kwa kukuza zaidi mauzo ya bidhaa za Tanzania nchini Uingereza.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni