Zinazobamba

WAJASIRIAMALI KOTE NCHI WAMETAKIWA KUWA WABUNIFU NA KUWA NA NIDHAMU YA FEDHA.

Na Vicent Macha, Dar es salaam

Wajasiriamali kote nchini wametakiwa kuwa wabunifu katika biashara zao ili waweze kukabiliana na ushindani wa bidhaa zao na siyo kuigana hali inayowafanya kulalamika kuwa biashara ni ngumu.

Mwanaharakati Msafiri Mwajuma akitoa mafunzo wa washiriki wa semina za jinsia na maendeleo (GDSS).

Hayo yameelezwa mapema jana Novemba 03, 2021 na Mwanaharakati wa Masuala ya kijinsia Ndugu Msafiri Mwajuma katika semina za Jinsia na Maendeleo(GDSS) zinazofanyika kila siku ya jumatano makao makuu ya TGNP Mabibo jijini Dar es salaam.

Ambapo somo la wiki hii lilikuwa likisema “Usimamizi wa fedha, uwekaji kumbukumbu na taarifa za kifedha katika biashara”.

Aidha amesema kuwa kitu cha kwanza kabla ya kuanza biashara ni lazima uwe na bajeti ambapo bajeti hiyo pia inahitaji ubunifu kwa kufanya kitu cha tofauti na wengine, lakini pia uweze kuweka kitu ambacho watu wanakihitaji kwa muda huo ili usije kupoteza nguvu bila mafanikio.

Ameendelea kusisitiza umuhimu wa kutunza kumbukumbu za biashara ili mjasirimali/mfanyabishara aweze kuwa na takwimu sahihi za biashara yake kama inakua ama inashuka, pia amewataka wajasiriamali hao kuweza kuwa na madaftari kabisa ya kuweza kuandika kila kinachofanyika katika biashara zao.

Lakini pia amewaeleza kama unataka kuwa mjasiriamali mzuri ni vema kuweka malengo ambayo utatamani kufikia baada ya kipindi fulani, kwani kujiwekea dira ni njia nzuri ya kufikia mafanikio na pia ni kipimo kizuri cha ukuaji wa biashara unayofanya.

Na mwisho amewataka washiriki hao kuweza kuwa na nidhamu ya fedha siyo kwa kuwa biashara ya kwako basi unachukua fedha mda wote na kufanyia matumizi mengine ambayo ni nje ya biashara hiyo, hii inaweza kukufanya ukafilisi biashara inachotakiwa ni wewe mwenyewe kufanya kama biashara siyo yako ikiwezekana ujulipe mshahara kabisa ili usiingilie mahesabu ya biashara hiyo.

Kwa upande wake Anamerania Mgwasi amesema kuwa amefurahishwa sana na mafunzo na hakutarajia kukipata alichoweza kukipata kwa siku ya leo kwani mwalimu alijaribu kuchambua kipengere kimoja baada ya kingine ili mradi washiriki waweze kupata kitu kizuri.

Lakini pia ameongeza kwa kuwashauri wafanyabiashara wengi hasa wa vyakula kuweza kuwa wasafi ili waweze kuwavutia watu walio wengi kununua bidhaa zao, Na pia amewataka wajasiriamali hao kuweza kuwa na lugha nzuri Pamoja na ubunifu kwenye kazi yao.

Naye Anna Samweli amesema kuwa yeye kwa upande wake amebarikiwa sana na hili somo na anatamani somo hili lingepewa muda wa kutosha ama lirudiwe juma lijalo ili waje kujifunza wakiwa kamili na kuwaonyesha walimu namna wao wanavyofanya huko mitaani je ni sawa au wanakosea.

Ameongeza kuwa yeye kama yeye anafanya biashara ya kuuza karanga na alianza na mtaji wa shilingi elfu kumi na mpaka sasa aoni mtaji wake kuyumba ingawa  mahitaji ya nyumbani yote yanatoka hapo hapo, hivyo anaomba ushauri Zaidi ili ajue anakosea wapi.

Muwezeshaji wa semina Msafiri Mwajuma akitoa ufafanuzi wa jambo fulani mbele ya wanaharakati mbalimbali ambao hawapo pichani mapema jana jijini Dar es salaam.

Washiriki wa semina wakifuatilia mafunzo kwa umakini.
Mshiriki wa semina za GDSS Mzee Abdallah Imba akitoa ufafanuzi wa jambo fulani mapema jana jijini Dar es salaam.
Baadhi ya Washiriki wa semina wakiwa katika kazi ya kikundi.
Mfanyakazi wa TGNP, Flora Kamamy akiwasilisha kile walichokijadili katika kazi za vikundi.
Semina ikiendelea.

Hakuna maoni